Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

ZITTO KABWE NA FILIKUNJOMBE WAIBUKA VIDEDEA KAMATI ZA BUNGE...

$
0
0
Wabunge Deo Filikunjombe (kushoto) na Zitto Kabwe.
Wabunge vijana waliokuwa wanaiongoza Kamati ya Bunge iliyovunjwa ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto na Makamu wake, Deo Filikunjombe, wameng’ara katika uchaguzi wa kamati mpya za Bunge.
Wabunge hao wamejikuta wakirudi madarakani, lakini kupitia Kamati waliyohamishiwa ya Hesabu za Serikali (PAC).
Awali, Kamati hiyo ilikuwa ikiongozwa na Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) ambaye kwa sasa hana kamati anayoongoza.
Hayo yalithibitishwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za Bunge ambaye ni Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel alipozungumzia kukamilika kwa mchakato wa uundwaji wa kamati hizo za kudumu.
Katika uundaji wa kamati hizo, alisema Spika Anne Makinda alimteua Andrew Chenge kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, wakati viongozi wengine wa kamati walipatikana jana baada ya kupigiwa kura.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti alishindwa kupatikana kutokana na kura za wajumbe kulingana, hivyo kufanya uchaguzi wake uahirishwe hadi Jumatatu.
Akizungumza kabla ya kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, Joel alisema: “Kutokana na unyeti wa Kamati ya Bajeti, imeonekana ni busara Spika ateue Mwenyekiti badala ya kutumika mfumo wa kura. Hiyo ndiyo demokrasia tuliyoona itumike sasa.
“Sababu kubwa ya kuchagua mfumo huo ni unyeti wa kamati yenyewe na upya wake na kama mnavyojua, mabunge mengi yana mifumo tofauti ya kupata wenyeviti wa kamati kama hii, tumechagua hiyo mojawapo ya kumpa Spika nafasi ateue Mwenyekiti. Amefanya hivyo na Chenge ndiye amepata nafasi hiyo”.
Mbali na hilo, alisema iliamuriwa pia kuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo apatikane kwa kupigiwa kura na wajumbe.
Akitangaza matokeo ya PAC, alisema Zitto ambaye sasa yuko mafunzoni katika Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti na Filikunjombe alipata kura nyingi za kumthibitisha kuwa Makamu Mwenyekiti.
Kamati nyingine ambazo zilipata viongozi ni ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) itakayoongozwa na Mwenyekiti Rajab Mbarouk Mohammed na Makamu Mwenyekiti Suleiman Jumanne Zedi. Hata hivyo, alioyekuwa Mwenyekiti wa LAAC, Augustino Mrema hakugombea safari hii.
Kamati ya Huduma za Jamii itaongozwa na Margaret Sitta na Makamu wake Stephen Ngonyani ‘Majimarefu’. 
Nyingine ni Kamati ya Mambo ya Nje ambayo Mwenyekiti wake ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa na Makamu wake Mussa Zungu, Mbunge wa Ilala.
Kamati ya Fedha na Uchumi itaongozwa na Mohammed Mgimwa na Makamu wake ni Luka Kitandula, wakati Kamati ya Ulinzi na Usalama iliyotenganishwa na ya Mambo ya Nje, itaongozwa na Anna Abdallah na Makamu wake ni Muhammed Seif Khatib.
Kamati nyingine zilizokamilisha mchakato huo wa uchaguzi ni ya Nishati na Madini ambayo Mwenyekiti wake ni Victor Mwambalaswa na Makamu ni Jerome Bwanausi, wakati kamati inayoshughulika na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) itaongozwa na Hamisi Kingwangallah ambaye ni Mwenyekiti na Makamu wake ni John Lwanji.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ni Hassan Ngwilizi na Makamu wake ni John Chiligati; Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala itaongozwa na Pindi Chana na Makamu wake ni William Ngeleja, wakati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira itaongozwa na James Lembeli na Makamu Mwenyekiti ni Abdulkarim Shah.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu alitangazwa kuwa Peter Serukamba na Makamu wake ni Profesa Juma Kapuya. Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji itaongozwa na Profesa Peter Msolwa na Makamu ni Said Nkumba huku ya Ukimwi akipewa Lediana Mng’ong’o akisaidiwa na Diana Chilolo.
Jenista Mhagama anakuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii na Makamu wake ni Said Mtanda.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles