![]() |
Shekhe Ponda Issa Ponda akihubiri katika moja ya mihadhara yake. |
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imempiga marufuku Katibu wa Jumuiya ya Taasisi ya Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda, kuendesha mihadhara ya kidini katika ardhi ya Zanzibar yenye mwelekeo wa kuleta mifarakano, chuki na uhasama.
Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, alitangaza marufuku hiyo wakati akiahirisha jana Mkutano wa Bajeti wa Baraza la Wawakilishi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.
Alisema mahubiri ya sura ya uchochezi yenye lengo la kuiingiza nchi katika machafuko ya kidini, hayatavumiliwa kwa kuwa madhara yake ni makubwa.
Kwa mfano, alisema Shekhe Ponda amekuwa akitumia wananchi wa Zanzibar kuendesha mihadhara yenye mwelekeo wa vurugu na chuki, hivyo wananchi wanatakiwa kutambua, kwamba vurugu zinapoibuka, waathirika ni Wazanzibari wakati Ponda akikimbilia Tanzania Bara.
"Huyu Shekhe anakaanga mbuyu kuwaachia wenye meno watafune ... yakizuka machafuko yeye hayupo nchini, kazi inabaki kwa wananchi wa Zanzibar ambao ndio waathirika wakubwa," alisema.
Balozi Seif alisema Wazanzibari wamechoka na mifarakano inayotokana na mivutano ya kisiasa, ambayo ilizuka tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992.
Alikumbusha wajumbe kuwa juhudi za kuleta amani na utulivu zimechukua muda mrefu, huku zikiacha makovu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo wananchi wasikubali kurejea matukio hayo.
Balozi Seif alisema Serikali isilaumiwe kwa hatua itakazochukua kwa viongozi wa aina hiyo, na kutaka wananchi wasiunge mkono uchochezi kama huo.
"Serikali inapiga marufuku mahubiri ya kiongozi huyo ambayo yanaonekana kuwa na mwelekeo wa chuki na uhasama isilaumiwe kwa hatua itakazochukua," alionya.
Balozi Seif alisema Zanzibar haina migongano ya kidini na waumini wake ambao wamekuwa wakishirikiana katika mambo mbalimbali na waumini wengine wa dini tofauti.