Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

KILA MTANZANIA SASA NI MSHUKIWA WA DAWA ZA KULEVYA...

$
0
0
Mtumiaji dawa za kulevya.
Biashara ya kusafirisha dawa za kulevya imeanza kutia doa taswira ya Watanzania kimataifa.

Hali hiyo inathibitishwa na kwamba katika baadhi ya nchi, kila Mtanzania anayeingia, hivi sasa anachukuliwa kama mshukiwa wa moja kwa moja wa dawa hizo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally, alisema jana kuwa Watanzania waliokamatwa wakifanya biashara hiyo, wametia doa taswira ya nchi.
"Watanzania wanaokwenda nchi zenye watu wetu wengi waliokamatwa kwa tatizo hili, ni washukiwa wa moja kwa moja, inachafua taswira ya nchi," alisema Mkumbwa alipozungumza na mwandishi.
Alisema kazi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni kufuatilia mwananchi alipo na si kuzuia kukamatwa na nchi nyingine, wanaokutwa na hatia wananyongwa au kufungwa maisha, kwingine kama kuna mkataba, hubadilishana wafungwa.
Mkumbwa alishauri elimu ya umma kuhusu madhara ya biashara hiyo iongezwe bila kuchoka na kila mtu ahusike kunusuru Taifa.
"Wanaosafirisha wanapaswa kuona hatari kubwa si tu kukamatwa, bali afya zao pia na mamlaka za kudhibiti zinapaswa kuimarishwa zaidi," alisema.
Mwito huo umetolewa, huku kukiwa na ongezeko la Watanzania kukamatwa na dawa za kulevya ndani na nje ya nchi.
Katika kuthibitisha usumbufu unaowapata Watanzania hivi sasa waendapo nje ya nchi, hivi karibuni msanii wa kizazi kipya, Madee, alipekuliwa na kukalishwa kwa takriban dakika 45 katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg, Afrika Kusini alipokwenda kwa shughuli zake halali.
Kamanda wa Polisi wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa, alisema hivi sasa mikakati zaidi imewekwa ikiwa ni pamoja na mikutano ya mara kwa mara baina ya nchi na nchi kote duniani.
Nzowa pamoja na kukiri kuwa huenda vifaa katika baadhi ya maeneo wanayopenya ni duni, lakini alisisitiza kuwa mapambano yanaendelea kwa lengo la kuzuia na kusaka wafanyabiashara wakubwa, wanaodaiwa kutuma vijana wakiwamo wasanii, kusafirisha dawa hizo.
"Mapambano yanaendelea, tukimkosa nchini kutokana pengine na changamoto zilizopo, tutampata nje ya nchi, tunafanya kazi pamoja kwa sasa dunia nzima.
"Tutaendelea kukamata mpaka 'mateja', hata tusipowakuta na dawa, ili watueleze wanapewa na nani, tungekuwa hatuendi vizuri tusingesikia mambo haya kwa wingi hivi leo, tutapambana tu," alisisitiza Kamanda Nzowa.
Katika kuthibitisha kuwa kikosi hicho na Jeshi zima la Polisi wako tayari wakati wote, alisema katika siku mbili za Ijumaa na Jumamosi zilizopita, walikamata watu watano wakiwa na gramu zaidi ya tano za heroine, wakiuziana na inasadikiwa huenda walikuwa na gramu nyingi walizokwishauza.
Alitaja waliokamatwa kuwa ni Neema Mponji (36) aliyekamatwa Mbagala Rangitatu, Charambe nyumbani kwake.
Wengine ni Issa Rashid (31), Idd Abdallah (25), Abdu Kibindu (35) na Time Mohamed (18) waliokutwa wakiuziana kati ya saa moja na mbili asubuhi nyumbani kwa wazazi wa Time, ambaye ni binti, Tandika wilayani Temeke.
Kamanda Nzowa alisema watuhumiwa hao, watafikishwa katika Mahakama ya Wilaya leo kujibu mashitaka.
Wiki iliyopita, Mtanzania Jackline Mollel (35), inadaiwa alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Harare, Zimbabwe, akiingiza shehena ya dawa za kulevya zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 72.
Kabla ya tukio hilo, Julai Watanzania wawili, Agnes Gerald 'Masogange' (25) na Melisa Edward (24), walikamatwa Oliver Tambo, wakidaiwa kuingiza dawa za kulevya kutoka Tanzania zikiwa na thamani ya mamilioni ya fedha. Walifikishwa mahakamani Johannesburg.
Pia Polisi, Kikosi Maalumu cha Kupambana na Dawa za Kulevya, kinashilikia watu watano, wakiwamo wanawake wawili, baada ya kukamatwa Ijumaa na Jumamosi  wakiuza dawa za kulevya aina ya heroine, Temeke, Dar es Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi, alipata kusema Serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha sheria itakayokuwa na meno, ili kubana wafanyabiashara tofauti na ilivyo sasa.
Mwishoni wa Juni, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alinukuliwa akieleza kuwa dawa za kulevya ni janga la Taifa kutokana na idadi kubwa ya vijana kuathirika na kwamba Serikali imejipanga kushirikiana na wadau wote wa ndani na nje ya nchi, kupambana na tatizo hilo na kusaka vigogo wanaotajwa kujihusisha na biashara hiyo.
Takwimu zinaonesha kuwa katika miaka mitano, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kuhusika na dawa za kulevya na kwa mwaka mmoja, Watanzania zaidi ya 250 walikamatwa. Wengi hukamatwa China, Brazil, Pakistani na Afrika Kusini.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles