Quantcast
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

UCHAGUZI MKUU ZIMBABWE NI KICHEKESHO KIKUBWA...

Image may be NSFW.
Clik here to view.
Rais Robert Mugabe (kushoto) na Morgan Tsvangirai.
Wakati upinzani nchini ukidai kuwa uchaguzi uliofanyika juzi ulikuwa kichekesho kikubwa, chama tawala kimedai kuwa mgombea wake, kiongozi mkongwe Robert Mugabe, amepata ushindi wa kishindo.
Mwanachama mwandamizi wa ZANU PF, amesema chama hicho kimeshinda kwa kiwango kikubwa katika uchaguzi huo mkali kupata kutokea nchini.
“Tumeshinda kote, urais na ubunge,” mwanachama huyo aliiambia AFP jana akisema Mugabe amemshinda mpinzani wake wa muda mrefu, Morgan Tsvangirai na kwamba chama hicho kimetetea viti vingi vya ubunge maeneo ya mijini.
“Tumeshinda kwa kishindo cha kuridhisha. Tumeishinda MDC.” Alisisitiza mwanachama huyo ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake.
Kura bado zinahesabiwa, ambazo zinaweza kushuhudia utawala wa Mugabe ambao umedumu kwa miaka 33 ukiendelea baada ya kushinda uchaguzi huo ambao ulidaiwa kugubikwa na udhaifu wa hapa na pale madai ambayo yalitolewa na MDC.
Hata hivyo, Tsvangirai alisema uchaguzi huo ulikuwa kichekesho, akidai kuwa ulijaa udanganyifu uliofanywa na kambi ya Mugabe.  Akizungumza na waandishi wa habari, Tsvangirai alisema uchaguzi huo ni haramu.
Kundi kubwa la waangalizi wa uchaguzi lilidai mapema kwamba watu takriban milioni moja walizuiwa kupiga kura. Chama cha Mugabe-ambacho tayari kinadai kushinda-kilikanusha madai hayo, kikisema uchaguzi ulikwenda vizuri.
Kiongozi wa waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU), Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, alisema tathmini yake ya awali inaonesha, kwamba uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki. Waangalizi wengine walipongeza utulivu uliooneshwa wakati wote wa kupiga kura.
Kazi ya kuhesabu kura ilianza juzi usiku, huku Tume ya Uchaguzi Zimbabwe (ZEC) ikiwa na siku tano za kutangaza mshindi.
Polisi nayo imetangaza kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayevujisha matokeo. Ni kinyume cha sheria matokeo yasiyo rasmi kutangazwa.
Akizungumza katika makao makuu ya MDC jijini hapa, Tsvangirai alisema: “Hitimisho letu ni kuwa hiki kimekuwa kichekesho kikubwa. Heshima ya uchaguzi huu imechafuliwa kutokana na ukiukwaji kiutawala na kisheria na hivyo kutibua hata uhalali wa matokeo yenyewe. Ni uchaguzi wa maigizo ambao hauoneshi matakwa ya watu.”
Tsvangirai alizungumza muda mfupi baada ya waangalizi kutoka Mtandao wa Uchaguzi Zimbabwe (ZESN) kusema uchaguzi huu “ulipangwa.”
Katika taarifa yake, ZESN ilisema wapiga kura waliotarajiwa hawakujitokeza katika asilimia 82 ya vituo vya kura kwenye maeneo ya mijini ambako Tsvangirai alikuwa na uungwaji mkono mkubwa.
Vijijini, ambako kunaonekana kuwa ngome ya Mugabe, asilimia ilikuwa 32, kundi hilo lilisema na kuongeza kuwa matokeo yake watu kama milioni moja kati ya milioni 6.4 waliokuwa na sifa za kupiga kura walizuiwa kupiga.
Juzi, wanavijiji, mawakala wa uchaguzi wa MDC na ZESN walisema uchaguzi uligubikwa na udanganyifu hususan katika maeneo ya vijijini katika jimbo la Masvingo.
“Haitoshi uchaguzi kuwa wa amani ni halali,” Mwenyekiti wa ZESN, Solomon Zwana aliwambia waandishi wa habari. “Unapaswa kuwapa wananchi wote … fursa sawa ya kupiga kura.”
Walidai kuwa viongozi wa kijadi na wakuu wa vijiji walipanga watu na kuwalazimisha kwenda katika vituo vya kura na kuwapa namba za kura kwa nia ya kuangalia ni nani wamempigia.
Walidai pia kuwa katika maeneo hayo, watu wanaojua kusoma walilazimishwa  kujifanya hawajui kusoma wala kuandika na hivyo kusaidiwa kupiga kura kwa ajili ya ZANU-PF.
Msemaji wa Zanu-PF, Psychology Maziwisa alikanusha madai kuwa wapiga kura wengi walizuiwa kwa makusudi kujiandikisha. Hata hivyo alikubali kuwapo kwa upungufu lakini akasisitiza kuwa vyama vyote viwili viliathirika.
Uchaguzi huu unahitimisha serikali ya umoja wa kitaifa kati ya ZANU-PF na MDC, ambayo iliundwa kutokana na wapatanishi baada ya uchaguzi uliobishaniwa mwaka 2008 na kugubikwa na ghasia.
Ili mshindi wa urais apatikane, anahitaji zaidi ya asilimia 50 ya kura. Kama hakutakuwa na atakayefikisha kiwango hicho, marudio ya upigaji kura yatafanyika Septemba 11.
Uchaguzi huu umefanyika kwa mara ya kwanza chini ya Katiba mpya iliyoidhinishwa kwa kura ya maoni Machi.
Marekani, ambayo imemwekea vikwazo Mugabe, nayo ilieleza wasiwasi wake kabla ya juzi juu ya uhalali wa uchaguzi, ikielezea jinsi ZANU-PF inavyopendelewa na vyombo vya habari vya Serikali na vikosi vya usalama.
Hali ilivyo inaweza kusababisha kujirudia kwa ghasia za mwaka 2008 kwani chanzo cha juu cha ZANU-PF ambacho hakikutaka kutajwa jina, kiliiambia Reuters kwamba chini ya saa 15 baada ya uchaguzi kumalizika, matokeo yalishaanza kuonekana.
“Uchaguzi huu ni wetu. Tumeizika MDC. Hatukuwa na wasiwasi wowote wa kushinda,” chanzo hicho kilisema lakini hakikutoa idadi ya kura.
Wakati huo huo, Zanu-PF imetangaza kuondoa ujumbe wake usio rasmi kwenye mtandao wa Twitter uliokuwa ukidai kupata ushindi wa kishindo. Badala yake jana chama hicho kilituma ujumbe mwingine kikisema kinasubiri tangazo la matokeo kutoka ZEC. Lakini mashahidi walisema kura zilizobandikwa nje ya vituo katika mji wa Mbare jijini hapa, ilipo ngome ya Tsvangirai tangu mwaka 2002, zinaonesha Mugabe ameshinda.
Walisema katika jimbo la Manicaland lililoko Mashariki mwa nchi, Tsvangirai alipata viti vinne kati ya 26 vya Bunge.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles