![]() |
Shekhe Ponda Issa Ponda. |
Wanasheria waliozungumza na mwandishi jana, walisisitiza kuwa licha ya kuwa Ponda anatuhumiwa na Polisi kutenda makosa ya uchochezi akiwa Zanzibar, lakini hukumu ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam dhidi yake, ilihusu kosa la jinai ambalo halina mipaka.
Hukumu hiyo ambayo mfungwa anakuwa nje chini ya uangalizi wa Mahakama kwa mujibu wa wanasheria hao, inaangalia zaidi tabia ya mtuhumiwa katika kipindi chote atakachokuwa anatumikia adhabu yake, na si suala la wapi ametenda kosa hilo kwa mara ya pili.
"Ndiyo maana anaamriwa asitende kosa lolote la jinai katika kipindi hicho, hukumu haisemi asitende ndani ya nchi tu, bali ni kokote atakakokuwa," alisema wakili wa kujitegemea, Emmanuel Makene.
Makene alisisitiza kuwa kama Ponda ametenda kosa la uchochezi Zanzibar, anapaswa kukamatwa, kwani ametenda kosa lile lile la awali na bado akiwa kwenye uangalizi wa kimahakama.
Wakili huyo alisisitiza kuwa hata kama kosa hilo amelitenda Zanzibar, bado Mahakama iliyomhukumu inaweza kutaarifiwa kuwa mtuhumiwa huyo ambaye yuko chini ya uangalizi huo, ameendelea kutenda makosa ya jinai kinyume cha agizo la Mahakama.
Wakili mwingine wa kujitegemea, Sweetbert Mkuba, alisema hukumu ya Ponda ina masharti, ndiyo maana akaelezwa kuwa ndani ya mwaka mmoja asitende kosa la jinai, bila kujali atakuwa sehemu gani ya nchi au ya dunia.
"Akiiba ng'ombe Kenya wakati amehukumiwa Tanzania, amri ya asitende kosa lolote la jinai inaendelea kusimama, Mahakama iliyomhukumu ikitaarifiwa kosa hilo, itafuta hukumu yake ya awali na atatumikia kifungo anachostahili," alisema Mkuba.
Alisema sheria iko wazi kwa kifungo kama alichohukumiwa Shekhe Ponda kuwa akifanya kosa lingine, amevunja masharti ya kuwa nje ya jela, hivyo anatakiwa akamatwe akatumikie kifungo kwa miezi ambayo itakuwa imebaki katika hukumu yake ya awali.
"Hii ni bila kujali mipaka ametenda kosa hilo akiwa wapi, makosa ya jinai hayana mipaka. Hata kama akitenda kosa akiwa Marekani na ukawepo ushahidi kuwa ametenda kosa hilo katika Mahakama iliyomhukumu hapo awali, lazima afutiwe kifungo cha nje," alisema Mkuba.
Alisema jambo la msingi hapo ni Polisi kuijulisha Mahakama, kwani atafutiwa kifungo cha nje tu, iwapo kuna mamlaka itakayokwenda kulalamika mbele ya mahakama husika na si vinginevyo.
Wakili mwigine wa kujitegemea ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, kwa maelezo kuwa kesi ya Ponda si yake, alisema kosa la Ponda ambalo anatuhumiwa kulitenda Zanzibar kisheria, linatoa nafasi ya yeye kufutiwa kifungo cha nje.
"Sawa amelitenda Zanzibar, lakini hili si suala la Mahakama ya sehemu gani ya Muungano; bali ni suala la tabia ya mtuhumiwa ambaye madhara yake ni kwa jamii, haidhuru katenda akiwa Zanzibar au Bara," alisema wakili huyo maarufu nchini.
Alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ikitaarifiwa tu chini ya kiapo na ikathibitika kweli ametenda kosa hilo, Mahakama hiyo itafuta kifungo cha nje kwa vile mtuhumiwa atakuwa amevunja masharti ya kifungo hicho.
Wakili Israel Magesa, alisema Ponda anaweza kushitakiwa tena kwa uchochezi na akahukumiwa kwanza kwa kosa la zamani, na kisha kwa lingine ambalo atakuwa amelitenda akiwa chini ya uangalizi.
"Lakini hii ni pale tu kesi yake itakapofikishwa katika Mahakama ile ile iliyomhukumu," alisema Magesa na kuongeza kuwa kama ametenda kosa Zanzibar, akashitakiwa visiwani, makosa ya Bara hayawezi kuhesabiwa katika mahakama za huko.
Juzi Polisi Zanzibar ilitoa taarifa kuwa inamsaka Shekhe Ponda kwa kuendesha mihadhara ya kidini katika misikiti Unguja, ambayo inaashiria uvunjifu wa amani.
Kamishna Mkuu wa Polisi Zanzibar Mussa Ali Mussa, alisema wana taarifa za Shekhe Ponda kuendesha mihadhara ya uchochezi na wanamtafuta kwa mahojiano zaidi.
Mei 10, Ponda alihukumiwa kifungo cha nje cha miezi 12 kwa mashati ya kutofanya kosa lolote katika miezi hiyo. Alipewa hukumu hiyo kwa vile hakuwa na kumbukumbu za kutenda makosa ya jinai na kwa vile alishakaa rumande kwa zaidi ya miezi saba.
Katika mihadhara yake, Shekhe Ponda anatuhumiwa kushawishi wananchi wa Zanzibar kuitisha maandamano makubwa kama ya Misri, kama njia ya kushinikiza Serikali iwaachie huru mashekhe sita wa Jumuiya ya Uamsho.
Polisi inashikilia mikanda mitatu ikidaiwa kumwonesha Ponda akiendesha mihadhara hiyo katika maeneo tofauti katika kisiwa cha Unguja; yenye mwelekeo wa kujenga chuki na uhasama kwa wananchi.