Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4576

PAPA MPYA APIGWA 'STOP' KWENDA KUAGA KWAO ARGENTINA...

$
0
0
Papa Francis I
Baada ya uchaguzi wa Papa mpya, Francis I (76), ambaye jina lake la awali ni Kardinali Jorge Mario Bergoglio, haruhusiwi kurudi nchini au jimboni mwake kama Askofu Mkuu ili kuaga.
Akizungumza na mwandishi jana, Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu wa Jimbo la Rulenge, Mhashamu Severine Niwemugizi, alisema:. “Hakuna utaratibu wa kurudi nyumbani kuaga.
“Kwanza hana nyumbani, maana tayari ni wa Kanisa tangu alipopewa upadri, ataitembelea nchi yake kama Papa katika ziara za kikazi, lakini si kwenda mahsusi kuaga.
“Hata hivyo, anaweza kutuma ujumbe wa salamu; kila kitu anapewa Vatican labda kiwe kitu muhimu ambapo pia atapelekewa na wasaidizi wake,” alifafanua Askofu Niwemugizi.
Alisema nafasi yake katika nchi hiyo, itachukuliwa na mtu mwingine ambaye si lazima apewe ukadinali, lakini atapelekewa majina ya ni nani anafaa kuwa Askofu wa Jimbo Kuu la Buenos Aires, na yeye kwa kuwa anawafahamu, atateua miongoni mwa majina hayo.
Akizungumzia utaratibu uliotumika kumtambulisha Papa Francis I baada ya kuchaguliwa, kabla ya kujitokeza kwa waumini, Askofu Niwemugizi alifafanua, kuwa Papa baada ya kuchaguliwa kwanza huulizwa kama amekubali na pili angependa kuitwa nani.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Method Kilaini, katika hilo alisema haijawahi kutokea Papa akakataa kupokea wajibu huo mkubwa baada ya kuchaguliwa, lakini kwa kuwa mambo hayo hufanywa kuwa siri kubwa, hakuna ajue kama yupo aliyepata kukataa.
Askofu Kilaini ambaye alishukuru Mungu kwa uchaguzi huo, alifafanua kwamba siri kwa makadinali, ni jambo la msingi na anayekiuka, huondolewa katika nafasi ya ukadinali.
Kwa mujibu wa Askofu Kilaini, baada ya Papa kuchaguliwa na kukubali wajibu huo, hupelekwa katika chumba maalumu kiitwacho ‘Chumba cha machozi’ ambako huachwa peke yake.
“Ikiwa kuna jambo linamsonga, anakwenda kulimaliza huko yeye na Mungu, kama ni kulia atalia, kama ni kugaragara atafanya hivyo, ili mradi amalize kila jambo linalomsonga kimawazo, kifikra na hisia kwa wakati huo,” alifafanua Askofu Kilaini.
Askofu Kilaini alisema katika chumba hicho, kuna nguo za ukubwa tofauti za kipapa, viatu na kofia. Papa hutafuta inayomtosha, huvaa na kurejea kwa makadinali kwa ajili ya kupongezwa na kupewa heshima yake.
Baada ya kupongezwa na wenzake, Askofu Kilaini alisema Papa hutokea katika roshani ya Basilica ya Mtakatifu Petro, kwa ajili ya kusalimu, kubariki na kuhutubia waumini. Fundi anayeshona nguo za mapapa hivi sasa anaitwa Gamalieli.
Kwa mujibu wa viongozi hao wa Kanisa, Papa lazima abadili jina, ili asisimame kama yeye katika kutimiza kusudio la Mungu. Hata hivyo, hupewa nafasi ya kuchagua la Mtakatifu au Papa aliyemtangulia.
“Huchagua majina mapya kwa kuwa wanapewa dhamana mpya, tena ya juu kabisa katika Kanisa, hii inamaanisha hawafanyi ya kwao bali ya Mungu, wanachagua majina wenyewe na wanazingatia kama anayemchagua anataka kufanya ama kuwa na maisha kama yake,” alisema Askofu Kilaini.
Katika hilo, aliungwa mkono na Niwemugizi na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Eusebius Nzigirwa.
Niwemugizi aliongeza kuwa, Papa amechagua kuitwa Francis kutokana na Mtakatifu Francis wa Xavery, aliyekuwa Mmisionari aliyezunguka duniani kuhubiri habari njema kwa masikini, jambo ambalo ni mwito wa kwanza kwa kila Mkristo. 
Alisema Papa mstaafu Benedict XVI alichagua jina hilo kufuata nyayo za Mtakatifu Benedict aliyeweka nguvu kubwa kujenga imani Ulaya huku John Paul II , akirithi jina la Papa John Paul I, ambaye alifariki dunia siku 33 baada ya kuchaguliwa kuwa Papa.
Jina la Papa John Paul ni mkusanyiko wa majina mawili, Yohana ambaye ni Papa Yohana wa 23 na Paulo Mtume, aliyezunguka pande za dunia kuhubiri Injili, huyu awali aliitwa Sauli.  
Papa Francis aliye na ndugu wanne katika familia yao ya wafanyakazi wastaafu, ni mtu mwenye msimamo wa kupinga ndoa za jinsia moja. Kanisa linamtazamia kusimamia misingi ya imani ya Kanisa la Kwanza la Mitume na pia kutetea wanyonge, kuimarisha imani na amani.
Akitoka katika nchi iliyoko Amerika ya Kusini ambako kuna Wakatoliki kwa asilimia 43 ya zaidi ya bilioni 1.2 duniani, anatarajiwa kuja na nguvu kubwa na mpya ya kiimani hasa changamoto ya kuibuka kwa makanisa mapya ya kiinjili.
Papa Francis I anatoka shirika la Majezuiti, shirika ambalo malengo yake ni kuwa na wafuasi halisi wa Yesu Kristo. Pamoja na mambo mengine, kanuni na utaratibu mwingine, misingi mikuu ya shirika hilo ni kutafuta kuwa mfuasi kamili wa Yesu Kristo.
Askofu Niwemugizi alimzungumzia Papa Francis I kama mtu mwenye welewa mkubwa wa kielimu, mtaalamu mkubwa na mwenye roho ya kichungaji zaidi ya kitawala.
Alisema katika mfumo wa utawala wa Vatican kama nchi kamili, Papa Francis hakuwa kwenye kundi la watawala wa Vatican yaani Curia ya Roma.
Katika Curia, wengi hutazamwa kama watu wenye nafasi kubwa ya kuwa Papa kutokana na kuielewa zaidi Vatican kiutawala.
Matumaini ya wengi katika hili kwa mujibu wa Askofu Niwemugizi, ni kwamba ataleta mapinduzi makubwa katika utawala wa Vatican. Kwa utaratibu wa Kanisa, alipochaguliwa tu, moja kwa moja alikuwa kiongozi wa Vatican.
Kwa mujibu wa Askofu Nzigirwa, Papa haapishwi kwa kuwa ndiye Kiongozi Mkuu wa Kanisa. “Hakuna wa juu yake wa kumwapisha, ila hufanyika Ibada ya Misa maalumu kwa ajili ya kumshukuru Mungu na kumtoa rasmi kuongoza Kanisa.”
Katika hilo, Askofu Nzigirwa alisema hakuna muda maalumu uliowekwa na Kanisa wa kufanya Ibada hiyo na  jopo la makadinali huamua lini misa ifanyike na mara nyingi huiongoza Papa mwenyewe na wakati mwingine, huendeshwa na Mwenyekiti wa Jopo la Makadinali,  Kadinali Angelo Sotano.
Akizungumzia maana ya tukio la kupata Papa wa kwanza kutoka nchi inayoendelea, Askofu Nzigirwa alisema neno Ukatoliki, limetimia.
 “Ukatoliki maana yake ni ‘ya Ulimwengu’, kitu cha kiulimwengu, kwa ajili ya wote na si jambo binafsi. Kutimia kwake kunatokana na mtazamo wa wengi, kwamba Papa alitarajiwa kutoka katika nchi zilizoendelea, kama Ulaya na Amerika, tofauti na ilivyotokea kwamba Papa mpya ametoka nchi zinazoendelea.
“Uongozi wa Papa mpya anayekuwa wa 266 tangu Papa wa Kwanza, Petro, unatarajiwa kuwa wa kusisimua kutokana na misingi yake iliyojengwa katika ukale wa kiimani na utendaji wake kwa nafasi ya ukadinali nchini mwake Argentina, uliozingatia kusaidia masikini, maisha ya kawaida na kurejesha waumini waliokuwa mbali na Kanisa hilo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4576

Trending Articles