![]() |
Miili ya askari hao ikishushwa kwenye ndege mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JKN, Dar es Salaam jana. |
Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal jana aliongoza umati wa Watanzania, wakiwemo viongozi, ndugu, jamaa na marafiki waliojitokeza kupokea miili ya wanajeshi saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa Jimboni Darfur, Sudan.
Ndege maalumu iliyokuwa imeandikwa Atlantis, B737-4000 Combi iliyobeba miili hiyo iliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu J.K. Nyerere - Terminal One (Air Wing) saa 10:39 jioni na mara baada ya kusimama, Makamu wa Rais alisogea eneo ilipo ndege kusubiri miili ya mashujaa hao wa amani kushushwa.
Viongozi wengine waliofuatana na Makamu wa Rais ni Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Saidi Mwema, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiq, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahaman Kinana na mke wa Rais, Mama Salma Kikwete.
Mara baada ya viongozi kusogea karibu na ndege, miili hiyo ilishushwa mmoja mmoja, ikibebwa na askari wenzao, huku wengine wakiwa wamejipanga upande mmoja, na upande wa pili wakiwa wamesimama ndugu na jamaa waliokuwa wamegubikwa na majonzi na wengine wakilia.
Kila jeneza moja lililobeba mwili liliingizwa katika gari moja la Jeshi na mara baada ya miili yote saba kupakizwa katika magari msafara ulianza kuipeleka miili hiyo kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi, Lugalo, jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi wa Habari Jeshini, Meja Joseph Masanja alisema baada ya mapokezi hayo yaliyofanyika jana na miili kuhifadhiwa Hospitali ya Lugalo, kesho saa 2:30 shughuli za kuwaaga marehemu zitafanyika katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Meja Masanja alitoa mwito kwa ndugu, jamaa na marafiki kushiriki kuaga miili ya mashujaa hao waliopoteza maisha wakitetea amani duniani na kwamba mara baada ya kuagwa marehemu watasafirishwa kwa ajili ya maziko katika maeneo yao husika.
Wanajeshi waliofikwa na mauti kwa kushambuliwa na waasi huko Darfur ni Sajenti Shaibu Shehe, Koplo Oswald Chaulo, Koplo Mohammed Ally, Koplo Mohammed Chukilizo, Private Rodney Ndunguru, Private Fortunatus Msofe na Private Peter Werema.