Katika tukio lisilo la kawaida, watu 15 wa familia moja juzi walivamia katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Mbeya wakipinga hatua ya taasisi hiyo kumshikilia mwanamke Elines Mlelwa kwa saa 46 katika mazingira ya kutatanisha.
Habari za kuaminika zilisema mwanamke huyo alikamatwa na kushikiliwa na Takukuru kwa siku zote hizo tatu kama njia ya kumshinikiza mumewe, Fulco Mlelwa kujisalimisha kwa taasisi hiyo kwa kile kinachodaiwa kukabiliwa na tuhuma za rushwa.
Hata hivyo, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Mbeya, Daniel Mtuka akizungumza na mwandishi jioni juzi, alisema kukamatwa kwa mwanamke huyo hakuhusiani na tuhuma zinazomkabili mumewe, bali ni kutokana na yeye pia kukabiliwa na tuhuma ambazo hata hivyo hakuweza kuzieleza.
Chanzo cha habari cha kuaminika kilimdokeza mwandishi jana juu ya tukio la kushikiliwa kwa mwanamke huyo aliyekamatwa na maofisa wa Takukuru wakishirikiana na askari wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kuanzia Julai 16 hadi Julai 18, mwaka saa 10 jioni akiwa amekaa mahabusu kwa zaidi ya saa 46, kitendo kinachoelezwa kuwa ni ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa kijinsia.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, Elines alikamatwa kwa kile alichoelezwa kuwa ni kutokana na kumficha mumewe ambaye ni mfanyabiashara anayemiliki Kampuni ya uwakala wa ukusanyaji wa mapato ya Aggressive Agency International Ltd ya jijini Mbeya, anayedaiwa kuwa na mashitaka yanayohusishwa na vitendo vya rushwa.
Hatua ya kukamatwa na kushikiliwa kwa siku tatu kwa Elines kuliifanya familia ya Mlelwa juzi mchana kuandamana kwenda katika ofisi za Takukuru za Mkoa ili kushinikiza ama kuachiwa au kupelekwa mahakamani kwa mwanamke huyo.
Akizungumza na mwandishi katika eneo la Uhindini jijini Mbeya muda mfupi baada ya kuachiwa kwa dhamana, Elines alisema maofisa hao wa Takukuru walimkamata kwa kile walichomueleza kuwa ni tuhuma za rushwa zinazomkabili mumewe na kwamba wanafanya hivyo ili kushinikiza mumewe huyo aliyepo safarini nje ya Mbeya kujitokeza.
"Ilikuwa jioni saa 11 nilipofika nyumbani kwangu kabla ya kuingia ndani nilizuiwa na maofisa wa Takukuru walionitaka kuingia kwenye gari lao kwa madai kuwa nimemficha mume wangu. Nilikataa kwa kuwa sikuambiwa hata kosa la mume wangu ni lipi. Kila nilipowauliza hawakunipa jibu bali walitaka tu niingie kwenye gari lao twende ofisini kwao.
"Niliendelea kugoma mpaka walipokwenda kuwachukua FFU watatu mmoja wa kike na wawili wa kiume ndipo wakanichukua kwa nguvu na kuniingiza katika gari lao na kunipeleka ofisi za Takukuru eneo la Uzunguni. Tukiwa hapo askari yule wa kike alianza kunihoji, hata hivyo niliomba nihojiwe na maofisa wa Takukuru ili wanieleze kosa la mume wangu ni lipi, " alisema.
Elines alisema baada ya kukataa ilipofika saa mbili usiku, askari huyo kwa kushirikiana na maofisa wa Takukuru walimpeleka Kituo Kikuu cha Polisi na kumweka mahabusu hadi juzi Julai 18 sasa kumi jioni alipoachiwa kwa dhamana. Alisema kinachomsikitisha ni kushikiliwa kwa saa zote hizo pasipokujua kosa lake wala la mumewe waliyedai amemficha.
"Leo (juzi) saa sita mchana walinifuata pale Central (Kituo Kikuu cha Polisi) wakanipeleka Takukuru. Hakuna mazungumzo yoyote yaliyofanyika hadi alipokuja Mwanasheria wa kampuni yetu na kuniwekea dhamana. Na nimeambiwa nirudi tena kesho (jana) asubuhi," alisema.
Mama mdogo wa Elines, Zawadi Mwambene alisema kwenda kwao ofisini hapo kulilenga kwenda kupata jibu ni kwa nini ndugu yao aliendelea kushikiliwa, lakini walitimuliwa na kulazimika kukaa nje ya ofisi hizo tangu saa sita mchana hadi saa 10 jioni wakati ndugu yao huyo alipoachiwa.
Awali alipozungumza na mwandishi kwa njia ya simu kutoka Dar es Salaam, Kamanda wa Takukuru wa Mkoa wa Mbeya, Daniel Mtuka, alikiri kuwepo kwa tukio hilo lakini alimtaka mwandishi kufika katika ofisi za Takukuru ili aweze kupewa maelezo ya kina kwa suala hilo.
Hata hivyo hata baada ya mwakilishi huyo kuhoji kuhusu sakata hilo, awali Mtuka alikataa kulizungumzia akisema walikuwa bado wanamhoji mwanamke huyo na hivyo asingeweza kutoa maelezo yoyote. Ilipofika saa mbili usiku Mtuka alimpigia simu mwakilishi huyo na kukiri kwamba alikuwa amemshikilia mwanamke huyo kwa saa hizo 46.
Hata hivyo katika maelezo yake Mtuka alikana mwanamke huyo kushikiliwa kutokana na tuhuma za mumewe anayetafutwa na taasisi hiyo na kueleza kuwa kila mmoja ana tuhuma zinazomkabili na kuongeza kuwa wataendelea kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mwanamke huyo wakati wakimtafuta pia mumewe.
Akizungumza na mwandishi kwa njia ya simu, Mlelwa alisema kwa muda mrefu sasa amekuwa na uhusiano mbaya na baadhi ya maofisa wa Takukuru akisema kuwa ulisababishwa na kampuni yake kudai ushuru wa maegesho kwa pikipiki na magari binafsi ya maofisa wa Takukuru hatua iliyowachukiza.
"Nina uhusiano mbaya na Takukuru kwa zaidi ya miaka miwili sasa unaotokana na chuki zao dhidi ya kazi yangu. Tuliwahi kukutana na kuyazungumza chini ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya (Juma Idd), na tukapatanishwa kwa kila upande kuagizwa kuheshimu kazi za mwenzake lakini nikaambiwa baadaye kwamba wameapa kuniangamiza kwa mbinu yoyote," alisema Mlelwa.