![]() |
Majeneza yenye miili ya askari hao. |
Miili ya wanajeshi saba wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), waliouawa jimboni Darfur, Sudan, itaagwa keshokutwa Dar es Salaam, imeelezwa.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Habari na Uhusiano ya JWTZ, ilisema shughuli za kuaga zitaanza saa tatu asubuhi katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga, Dar es Salaam.
Ilisema miili hiyo inatazamiwa kuwasili Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo saa tisa alasiri.
Kwa mujibu wa taarifa, itawasili kwa ndege maalumu katika uwanja huo wa ndege (wa zamani) baada ya hapo itapelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Jeshi ya Lugalo.
Julai 17, Rais Jakaya Kikwete alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Sudan, Omar Bashir, kuhusu kuuawa na kujeruhiwa kwa askari hao wa Tanzania.
Alimtaka Rais Bashir kuchukua hatua za haraka kusaka na kukamata waliohusika na kitendo hicho
kiovu, na kuwafikisha mbele ya sheria haraka iwezekanavyo.
Rais Bashir alikubaliana naye na kumwahidi kuwasaka na kukamata wahusika na kuwachukulia hatua za kisheria.
Alimweleza kuwa binafsi anaamini waliohusika ni wahalifu, na kusisitiza kuwa lazima watasakwa hadi
kukamatwa na kuchukuliwa hatua. Alimpa pole Rais Kikwete kwa tukio hilo.