Mkazi wa Mji Mpya, mjini hapa Charles Kanyemba (30), ameuza redio yake ili kumwezesha kupata fedha za kugharimia mavazi, pete ya harusi na kufunga ndoa na Honoratha Juma (28).
Bwana harusi huyo aliuza redio hiyo kwa Sh 70,000 baada ya kukosa chanzo kingine cha fedha za kumwezesha kutimiza lengo lake la kufunga ndoa baada ya kuishi uchumba kwa miaka 11.
Hivyo alitumia fursa ya msamaha kwa wachumba sugu uliotolewa na Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro kwenye jumuiya zake ambapo Kanyemba alifunga ndoa hiyo Juni 8, siku ya sherehe ya Jumuiya ya Mtakatifu Boniface, Mji Mpya.
Akizungumza na mwandishi juzi nyumbani kwake Mji Mpya, Kanyemba alisema aliuza redio ili kupata fedha za kununua mahitaji muhimu yakiwamo mavazi ya siku ya ndoa baada ya kukaa uchumba na mkewe huyo kuanzia mwaka 2002.
“Baada ya msamaha huo kwa wachumba sugu na ubatizo wa watoto waliozaliwa nje ya ndoa, nilikwenda kuandikisha na ndoa ikatangazwa katika Kanisa Kuu Katoliki la Mtakatifu Patrice kwa majuma matatu kulingana na utaratibu wa Kanisa,” alisema Kanyemba.
Alisema ndoa yake ilifungishwa na Paroko Msaidizi wa Parokia ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Patrice, Padri Fidelis Mwesongo.
“Licha ya kutangaziwa msamaha kwa wachumba sugu ... ni mimi pekee katika kata ya Mji Mpya niliyejitokeza kujiandikisha na kufunga ndoa,” alisema Kanyemba.
“Nilichukua uamuzi kutokana na kuishi muda mrefu na kuzaa watoto wawili, hakukuwa na haja ya kujitumbukiza katika gharama kubwa ...jambo la msingi ni kufunga ndoa na si kuangalia gharama za harusi,” alisema.
Hata hivyo, alisema hakuwa na fedha za kukodi ukumbi, matarumbeta siku ya ndoa kwenye kigango cha Jumuiya hiyo kilichoko umbali wa meta 100 kutoka nyumba wanamopanga.
Alisema baada ya kufunga ndoa, shangazi yake aliyemtaja kwa jina la Mwalimu Paula Jaka aliwaandalia sherehe fupi nyumbani kwake mtaa wa Kiswanya A, kata ya Uwanja wa Taifa.
“Nilikodi teksi kwa Sh 5,000 iliyonipeleka mimi, mke wangu na jirani yetu mmoja kwa shangazi alikoandaa chakula; ni watu wachache sana walioshiriki chakula na vinywaji...sherehe ilidumu kwa saa mbili tu,” alisema na kuongeza:
“Wakati wa kurudi nyumbani, nilirudishwa na gari la binamu yangu wa kike- mtoto wa shangazi-namshukuru Mungu kwa kufanikisha ndoa ambayo ni tendo muhimu kwa binadamu,“ alisema.
Hivyo alisema kutokana na umuhimu wa ndoa ndiyo sababu akauza redio, na fedha iliyopatikana alinunua nguo na vitu vingine.
“Nilidhamiria nifunge ndoa, sikuwa na fedha ... nikawaza ni bora niuze redio yangu nipate fedha, nikaiuza kwa Sh 70,000, nikakaa chini na kuweka bajeti ya mahitaji muhimu hasa vitu vyangu na vya bibi harusi, viligharimu Sh 65,000,“ alisema.
Alitaja vitu vilivyonunuliwa na gharama kwenye mabano, kuwa ni suruali ya Jeans ya mtumba (Sh 8,000), shati la dukani (Sh 10,000) na viatu vya mtumba (Sh 10,000).
Vingine ni vya bibi harusi ambavyo ni gauni (Sh 10,000) na viatu (Sh 13,000), pete mbili zilichongwa kwa sonara kwa Sh 4,000 baada ya kuyeyushwa mkufu wa dhahabu aliokuwa nao bibi harusi ikiwa na uzito wa gramu 1.5 na Sh 5,000 zilitengwa kwa ajili ya kulipia picha tano za ukumbusho.
Hata hivyo, alisema uvumilivu kati yake na mkewe umemwezesha kudumu kwa miaka hiyo, kwani wakati wakianza kuishi uchumba walipanga nyumba ya udongo eneo hilo la Mji Mpya na kulalia godoro chini na baada ya kupata fedha kidogo, hivi sasa wamenunua baadhi ya vitu na kupanga chumba chenye sakafu na kununua vifaa muhimu vya ndani.
"Sikuona umuhimu wa kuliweka jambo hili la ndoa hadharani kwa ndugu zangu...sikuwa na kianzio cha fedha...watu wanawezaje kukuchangia wakati huna kianzio?
“Nikaona tendo kubwa ni ndoa na kujinunulia mwenyewe na mke wangu mavazi ...hata watoto sikuwanunulia nguo walitumia zao za zamani kwani zilikuwa bado mpya," alisema.
Kanyemba ambaye ni mzaliwa wa Mhonda, Turiani wilayani Mvomero, baada ya baba yake mzazi kufariki dunia mwaka 1985 akiwa mdogo, alichukuliwa na kulelewa na shangazi yake na kuhitimu darasa la saba mwaka 1996 shule ya msingi Mafiga, mjini hapa.
Mwaka 1999 alihitumu mafunzo ya uchoraji katika chuo cha Tushikamane cha Kanisa Katoliki Jimbo la Morogoro na mwaka 2000 alijifunza udereva katika chuo cha Veta Kihonda na kuendesha teksi kwa muda, kabla ya kwenda kufanya kazi kiwanda cha vifaa vya michezo cha Mazava mjini hapa ambako aliacha kazi Februari.
Kuhusu maisha ya baadaye, alisema anatarajia kufanya biashara ya nguo za mitumba baada ya malipo yake kutoka NSSF kutokana na kipindi alichofanya kazi Mazava. Mbali na kujihusisha na biashara hiyo, alitaja shughuli nyingine kuwa ni kilimo cha nyanya nyumbani kwa mkewe Mongwe, Mlali wilayani Mvomero.
Hivyo alishauri vijana na watu wengine kutambua kuwa wawili wanapoamua kufunga ndoa si gharama, bali ni hiari yao na wao wanaweza kuifanya ndoa hiyo isiwe na gharama, tofauti na ilivyo sasa ya kujiongeza mzigo.
Honoratha alisema ameona fahari kubwa kufunga ndoa baada ya kuishi uchumba muda mrefu na kupata watoto wawili wa kiume. Alitaja watoto aliozaa na mumewe kuwa ni Adriano (11) anayesoma darasa la tano shule ya Msingi Kaloleni na Adolf mwenye umri wa zaidi ya mwaka moja.
“Tumependana, ndiyo maana ndoa yetu tumeifunga kwa hiari yetu na kwa kiwango tulichokuwa nacho... nimepuuza maneno ya baadhi ya wanawake wanaodai kwenda na wakati,” alisema na kuongeza:
“Nimeshuhudia ndoa nyingi za kifahari zinafungwa, lakini hazidumu, ndoa za watu wanyonge na masikini ndizo zinadumu kwa kuwa wana upendo wa dhati wakati wa shida na raha,” alisema Honoratha.
Mwanajumuiya ya Mtakatifu Boniface, Magdalena Yohana (70) aliyezungumza na gazeti hili baada ya kushuhudia kufungwa kwa ndoa hiyo, aliwapongeza kwa uamuzi wa kufunga ndoa isiyokuwa na gharama za kutisha.
Hivyo alisihi vijana na watu wengine kuiga mfano huo wakitambua kuwa ndoa ni ya watu wawili wapendanao na kwamba ndoa za aina hiyo zinapata baraka kubwa ya Mungu na kudumu, tofauti na zinazotumia gharama kubwa zikiwaacha wanadoa bila kitu. Magdalena ni miongoni mwa viongozi wa kigango hicho ambako ndoa ya Kanyemba ilifungwa, huku yeye na mumewe Joseph Raymond (80) wakibariki miaka 57 ya maisha yao ya ndoa.