![]() |
Askari wa moja ya kampuni za ulinzi wakiwa kwenye gwaride kujiweka sawa. |
Licha ya kuwepo utitiri wa kampuni za ulinzi binafsi nchini, imeelezwa kuwa uanzishwaji wake umekiuka Katiba ya nchi na uwepo wa kampuni hizo zisizopungua 705 ni kinyume cha sheria.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebaini kuwa hadi mwezi jana, Dar es Salaam pekee ilikuwa na kampuni za ulinzi binafsi zilizosajiliwa 297 ambapo katika hizo, 150 ni za Kinondoni, 102 Ilala na 45 Temeke. Nyingine zinaendelea kusajiliwa.
Aidha, imeelezwa kuwa kutokuwepo sheria inayosimamia uanzishwaji wa kampuni hizo, kukosekana kwa bodi inayodhibiti utendaji katika sekta binafsi ya ulinzi na kutokuwepo sera, kanuni na au tangazo la Serikali kuhusu mambo ya sekta hiyo, ndiyo vyanzo vya matatizo yanayoonekana ndani ya ulinzi binafsi.
Matatizo hayo ni pamoja na kuwa na walinzi ‘wazee’ wasiomudu kazi ya ulinzi kutokana na umri mkubwa, ulinzi wa kutumia fimbo, virungu, manati na usiozingatia umuhimu wa viatu (buti) kutokana na kuwepo na walinzi wanaovaa kandambili na makubadhi wakiwa kazini, uwepo wa walinzi wanaoshiriki uhalifu kama ujambazi na kutoa siri kwa wahalifu kuhusu mali za wanaolindwa.
Hata hivyo, kumekuwa na maelezo yanayokinzana kuhusu sheria inayosimamia ulinzi binafsi ambapo Mkuu wa Polisi Jamii nchini, Kamishna Msaidizi Michael Kamuhanda alieleza kuwa ipo na kwamba inaelekeza umri wa askari wa ulinzi huo kufanya kazi lindoni ni miaka 45, na si vinginevyo.
Kamuhanda alisisitizia gazeti hili kuwa mlinzi aliyezidi umri wa miaka 45 au chini ya miaka 18 anakiuka sheria ya ulinzi ambayo hata hivyo, hakuitaja, kwa kuwa hana nguvu za kupambana na wahalifu lindoni na badala yake anahatarisha maisha yake.
Alikiri kuwapo askari walinzi binafsi wanaosinzia lindoni kutokana na umri mkubwa, magonjwa na njaa. “Wanakuwa dhaifu na kushindwa kutimiza matakwa ya kazi ya ulinzi wa watu na mali katika majengo wanayoaminiwa kulinda.
“Sheria inaeleza wazi kuwa wazee na watoto hawapaswi kushiriki ulinzi lindoni. Lakini kwa sababu waajiri hawazingatii sheria, wanaruhusu ‘wazee’ na watoto wakeshe kwenye malindo, huku wakijua kuwa hawamudu kazi hiyo. Wanapaswa kuwapa buti pia, lakini si ajabu kukuta hawana viatu vya kazi yao,” Kamuhanda alisema.
Aliongeza kwamba Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema alipata kutoa mwongozo wa nini walinzi binafsi wanatakiwa kuvaa, ikiwa ni pamoja na umri unaofaa kulinda.
“Kuna mambo mengi yanakosewa, ndiyo maana tumeagiza makamanda wa Polisi wa Wilaya wawe wanafanya ufuatiliaji kuhakikisha sheria na taratibu za ulinzi binafsi hazikiukwi. Hao ndio wako karibu na kampuni hizo Dar es Salaam na mikoani, kwa hiyo ni rahisi kufanya ufuatiliaji wa karibu,” Kamuhanda alisema.
Alitaja udhaifu unaofanywa na waajiri wa walinzi hao kuwa ni kutowabadilishia majukumu wafikiapo umri wa kuacha ulinzi lindoni hasa wanapoona kuwa bado wanawahitaji.
Kukubali malindo mengi kwa sababu ya fedha na kusahau kuwa hawana walinzi wa kutosha na hivyo ‘kuokoteza’ hata wasio na sifa na kuwavisha sare na pia kupenda kulipa mishahara midogo na kukwepa kufuata baadhi ya taratibu.
“Inawezekana kuwabadilishia majukumu wafikiapo miaka 45. Wanaweza kufanya kazi za utawala na si lindo,” Kamuhanda alisema na kuongeza kuwa virungu, manati, fimbo, bastola na silaha za kivita, haviruhusiwi kutumiwa na walinzi hao isipokuwa bunduki walizoelekezwa wakati wakipewa kibali cha Polisi cha kuanzisha kampuni.
Kutokana na maelezo yake, kampuni za ulinzi zinasajiliwa kwa Msajili wa Kampuni (BRELA) na usajili kuhakikishwa na kitengo cha usajili wa kampuni binafsi za ulinzi katika Jeshi la Polisi, chini ya Idara ya Polisi Jamii.
Baadhi ya walinzi waliozungumza na gazeti hili walisema mishahara, sare na vifaa vya kazi wanavyotumia ni duni kiasi cha kushindwa kukidhi matakwa ya kazi hiyo.
Kwa nyakati tofauti, huku wakisita kutajwa gazetini, walinzi hao walisema, wakati mwingine hulazimika kukimbia malindo na kuacha uhalifu utendeke kwa sababu silaha wanazotumia wahalifu huwa ni nzito kuliko virungu wanavyotumia.
Mwenyekiti wa Chama cha Ulinzi Binafsi Tanzania (TSIA), Almas Maige alisema kampuni za ulinzi nchini zinaendeshwa bila sheria na ni kinyume cha Katiba.
Hata hivyo alisema ili kujihalalishia uwepo, kampuni hizo zinatumia sheria ya BRELA na kibali cha Polisi ambacho, tofauti na anavyodai Kamuhanda, hakitaji umri wa askari kufanya ulinzi lindoni.
“Kibali chao hiki hapa (anaonesha nakala) hakina umri wanaotaja, ndiyo maana unaona waajiri wanawaacha lindoni walinzi wao wenye umri mkubwa. Kwa sababu ya kutokuwa na sheria inayosimamia ulinzi binafsi, tunatumia ya ajira inayoeleza wazi umri wa mfanyakazi kustaafu kuwa ni miaka 60.
Kuhusu mishahara, alisema itakuwa sahihi kama kutakuwa na bodi ya kudhibiti na kupanga mishahara ya walinzi kulingana na madaraja.
“Kukiwa na bodi hata kiasi cha tozo anayopaswa kulipa mteja kwa kampuni ya ulinzi kitakuwa kinafuata vigezo, sasa hivi kila mmoja anatoza kiasi chake. Hiyo si sawa,” alisema.