![]() |
Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete. |
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa wiki ijayo kuongoza Kamati Kuu ya chama hicho kujadili Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyozinduliwa hivi karibuni.
Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana alisema msimamo wa chama juu ya rasimu hiyo utajulikana baada ya kikao hicho.
Alisema kwa sasa hawawezi kupinga wala kupongeza mpaka watakapoijadili kwa pamoja.
Alisema hayo wakati akizungumza katika mahojiano naÊ waandishi wa habari jijini Dar es Salaam baada ya kufanya mazungumzo na wajumbe wa Chama cha Kikomunisti cha Vietnam waliowasili nchini juzi kwa malengo ya kuimarisha uhusiano na CCM.
Kwa mujibu wa Kinana, baada ya kuchambua kifungu kwa kifungu, chama hicho kitatoa msimamo wake. Alisema katika suala hilo siyo vizuri kutoa msimamo bila kushirikishana kwani bahati nzuri chama hicho kina vikao halali vya kujadili masuala mbalimbali.
Kikao hiki cha Kamati Kuu kitafanyika Jumatatu ijayo chini ya Mwenyekiti wake Rais Kikwete kisha kupata msimamo wa chama chetu, alisema Kinana.
Kinana alisema watajadili kwa kuzingatia hali halisi ya sasa kwa taifa la leo na lijalo ili kuweka kuunga mkono rasimu hiyo au kuipinga.
Rais kama mfalme
Katika kujadili rasimu hiyo ya Katiba, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dk Hadji Semboja amehadharisha kuwa mfumo wa serikali tatu utaifanya Serikali ya Muungano isiwe na nguvu kiuchumi kitendo kitakachofanya Rais wake asiwe na nguvu hivyo kumfanya aongoze nchi kama mfalme.
Mchumi huyo alisema vyanzo vya mapato ya Serikali ya Muungano vitaifanya Serikali ya Muungano kutegemea mapato kutoka katika michango ya nchi washirika jambo ambalo alisema nchi washirika kama Tanzania Bara, rais wake atakuwa na nguvu kubwa ya kiuchumi.
Rasimu ya Katiba inaeleza kuwa vyanzo vya mapato ya Serikali ya Muungano vitakuwa ni ushuru wa bidhaa, maduhuli yatokanayo na taasisi za muungano, mchango kutoka kwa washirika wa muungano na mikopo kutoka ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano.
Kwa mujibu wa rasimu hiyo rais wa muungano atakuwa ni rais mtendaji, lakini hata hivyo Dk Semboja anaonya kuwa kwa kukosa nguvu ya kiuchumi anaweza kugeuka rais mfalme asiyemtendaji kama ilivyo kwa malkia wa Uingereza.
"Tunaweza kujikuta huyu rais wa muungano akawa ni ceremonial (hana nguvu) maana hana fedha za serikali yake atategemea nchi washirika, je nchi mojawapo wakikwaruzana na akagoma kutoa huo mchango itakuwaje? Hili ni jambo la kuliangalia kwa makini sana," alisema.
Mtaalamu huyo wa mambo ya uchumi alisema kama Rasimu ya Katiba itabaki kama ilivyo, uongozaji wa Dola utaegemea zaidi maelewano kati ya viongozi hao watatu, lakini ikitokea kusiwepo maelewano ni wazi kuwa Serikali ya Muungano inaweza ikanyimwa fedha na washirika wake.
"Kwa rasimu ilivyo hii Serikali ya Muungano itakuwa ni mzigo wa nchi washirika ndio maana nasema huyu rais utendaji wake utakamilika iwapo tu atakuwa na maelewano na wakuu wa nchi washirika, lakini kukitokea mikwaruzano hapo ndipo tutaona gharama za serikali tatu," alisema Dk Semboja.
Katika rasimu hiyo, serikali ya nchi mshirika wa muungano itakuwa na mamlaka ya kukopa fedha ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharimia shughuli zilizo chini yake. Endapo mkopo huo utahitaji dhamana ya serikali, Serikali ya Muungano itashauriana na nchi mshirika wa muungano na wakikubaliana wanaweza kutoa dhamana kwa mkopo unaoombwa.
Dk Semboja katika maoni yake anakiri kuwa serikali tatu itakuwa ni gharama kuziendesha lakini hata hivyo anasema kwa kuwa tayari wananchi wenyewe ndio wametaka, "Hizo ndizo gharama za demokrasia."
"Itabidi tuwe na marais watatu, makamu marais watatu kama Zanzibar itakubali kubaki na makamu mmoja. Kwa sasa tuna marais wawili na makamu marais watatu naona hakuna tofauti hata hizo serikali tatu zikianzishwa," alisema Dk Semboja.
Alisema gharama za serikali zitabainika ndogo kutokana na mambo yatakayoainishwa katika Katiba ya Tanzania Bara na marekebisho ya Katiba ya Zanzibar ili kuona ukubwa wa serikali zao. "Kama wote wataendana na Rasimu ya Katiba ya Muungano ni wazi kuwa hata serikali zao zitakuwa ndogo."
Viongozi wapigwa kufuli kufungua akaunti nje
Katika rasimu hiyo ya Katiba mbunge, waziri au mtumishi mwingine wa umma ni marufuku kufungua akaunti nje ya nchi isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu. Hata zawadi ambazo watapewa viongozi katika shughuli za kiserikali sasa kuwa mali ya Jamhuri.
Rasimu hiyo inaeleza Bunge litatunga sheria ya kuanzisha mitaala inayohusu maadili na uraia shuleni na vyuoni na uanzishaji wa mitaala inayo katiba mashuleni na vyuoni.
Mfumo wa sasa wa wabunge kuteuliwa kushika nyadhifa za ukuu wa wilaya na mikoa, umepigwa marufuku katika rasimu hiyo ya Katiba ambako inaeleza kuwa kiongozi wa umma hataruhusiwa kushika nyadhifa mbili au zaidi au kutumikia mihimili ya Dola zaidi mmoja kwa wakati mmoja.
Rasimu hiyo ya Katiba inapiga marufuku mtu, kikundi au taasisi ya dini kutumia uhuru wa kutangaza dini kwa kukashifu imani na dini nyingine, kujenga chuki au kuchochea vurugu na ghasi kwa madai ya kutetea imani au dini.
Pia inaelezwa kuwa dini na imani ya dini haitatumika kwa namna yoyote itakayowagawa wananchi, kuleta uhasama au kuharibu amani miongoni mwa wananchi.
Tume ya Mahusiano ya Uratibu wa Serikali
Rasimu mpya ya Katiba inaelekeza kuwa Tume ya Mahusiano kazi yake ni kusimamia na kuratibu mahusiano kati Serikali ya Muungano na washirika, wajumbe wa tume hiyo ni Makamu wa Rais wa Muungano, Marais wa Nchi Washirika, Mawaziri Wakaazi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Muungano.