Quantcast
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

SERIKALI YAJIPANGA KWA KATIBA YA TANZANIA BARA...

Image may be NSFW.
Clik here to view.
Jaji Frederick Werema.
Serikali imesema hakuna kipengele chochote katika Rasimu ya Katiba kitakachochelewesha ama kuzuia uchaguzi mkuu wa wabunge na rais mwaka 2015.

Hayo yalibainishwa jana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alipozungumza na mwandishi wa habari hizi kuhusu hatma ya Katiba ya Tanzania Bara, iwapo rasimu hiyo itapitishwa na kukubali ziundwe serikali tatu.
Alisema endapo Aprili 29 mwakani, kipindi kilichopangwa kupata Katiba mpya ya Muungano, wananchi watapendekeza kuwapo kwa Katiba ya Tanzania Bara, ofisi yake itakuwa tayari kutekeleza hilo katika muda uliobaki bila kuathiri uchaguzi mkuu.
“Baada ya kupokea Rasimu, nasi tulikuwa na mtazamo wa kuangalia suala zima la Katiba ya Tanzania Bara hasa kutokana na kuwa Zanzibar tayari wanayo. Wananchi wakitaka hilo tutalifanya ndani ya muda na tunawahakikishia hakuna kitu cha kuchelewesha uchaguzi mkuu,” alisisitiza.
Werema alisema kwa sasa wanasubiri Rais Jakaya Kikwete arejee nchini na kumpa ushauri na mapendekezo yao kuhusu vipengele vya Rasimu hiyo, likiwamo suala la uundwaji wa Katiba ya Tanzania Bara. Kikwete yuko kwenye ziara ya kikazi Japan na Singapore.
“Tumeanza kulishughulikia hili kwa kutoa ushauri na mapendekezo katika vyombo vya uamuzi, kwani baada ya kukamilika mwakani, ni lazima kuwepo na sheria ya mpito ya kuendesha nchi baada ya muda huo.”
Werema aliongeza: “Sheria ya Mpito itasaidia namna ya kuendesha Serikali, kwa sababu Rasimu hii ni ya Katiba ya Muungano, pia kuna vifungu na sheria ambazo zitatakiwa kufanyiwa kazi, kwa mfano namna ya kuachiana majukumu, namna ya kushughulikia wafanyakazi na mawaziri waliokuwa kwenye Serikali ya Muungano, tutayakamilisha Katika hatua nyingine, Rasimu hiyo inalipa Bunge mamlaka ya udhibiti wa mikopo ya Serikali ndani na nje ya nchi.
Mapendekezo ndani ya Rasimu yanataka  Bunge liweke masharti ya Serikali kuzingatia wakati wa kukopa fedha ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na kuitaka itoe taarifa bungeni kuhusu mikopo.
Kutokana na Rasimu hiyo,  ingawa Serikali itakuwa na mamlaka ya kukopa fedha ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kugharimia shughuli zilizo chini ya mamlaka yake, Bunge litatunga sheria juu ya mikopo hiyo ambayo itaweka masharti ya kuzingatiwa na Serikali wakati wa kukopa na kuweka utaratibu wa Serikali kutoa taarifa bungeni kuhusu mikopo.
Taarifa hiyo pamoja na masuala mengine, itaeleza kiasi cha deni lililopo na riba yake, matumizi yaliyofanywa au yatakayofanywa kutokana na fedha za mkopo husika.
Vile vile taarifa itakayopelekwa bungeni, itatakiwa ioneshe utaratibu uliowekwa wa kulipa deni husika na hatua iliyofikiwa katika kulilipa.
Wakati Rasimu imependekeza serikali tatu; kwa maana ya Muungano na mbili ambazo ni mshirika wa Muungano, katika kipengele cha kukopa, inaonesha serikali mshirika itakuwa na mamlaka yake lakini ya Muungano inaweza kutoa dhamana.
Hata hivyo, Bunge litatunga sheria itakayoweka utaratibu wa Serikali ya Muungano kudhamini mikopo ya Serikali za washirika wa Muungano.
Katika kipindi cha miezi mitatu tangu kumalizika kwa mwaka wa fedha, Serikali itachapisha ripoti katika Gazeti la Serikali itakayoelezea mikopo iliyodhaminiwa na Serikali katika mwaka wa fedha uliopita.
Kuhusu maadili ya viongozi wa umma, zawadi kwa watumishi wa umma zimewekewa kibano na Rasimu hiyo.
Rasimu inaelekeza kuwa chochote kitakachotolewa kwa mtumishi kama zawadi, lazima kipitie kwa Katibu Mkuu Kiongozi kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara au taasisi ya Serikali inayohusika.
Mtumishi husika atakapowasilisha zawadi hiyo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, atalazimika kuainisha aina ya zawadi, thamani yake, sababu ya kupewa na mtu au mamlaka iliyotoa zawadi hiyo.
Aidha, mtumishi wa umma hatafungua au kuendesha akaunti ya benki nje ya nchi isipokuwa tu kwa namna ambayo sheria za nchi zinaruhusu.
Vile vile mtumishi wa umma hatakopa au kupokea mkopo au faida yoyote kwa namna au mazingira ambayo yanashusha hadhi au heshima ya utumishi wa umma.
“Bunge litatunga sheria itakayosimamia, pamoja na mambo mengine, thamani, kiwango, aina na uhifadhi wa zawadi,” inasema sehemu ya mapendekezo.
Mtumishi wa umma aliye katika ajira ya kudumu hataruhusiwa kuingia katika ajira nyingine yenye malipo ya mshahara. Pia hataruhusiwa kuchaguliwa au kuteuliwa kushika madaraka katika chama cha siasa.
Vile vile mtumishi aliyestaafu na anayepokea malipo ya pensheni kutokana na fedha za umma hataruhusiwa kuwa mwenyekiti, mkurugenzi au mtumishi zaidi ya vipindi viwili katika chombo chochote kinachoendeshwa na fedha za umma.
Kiongozi wa umma kwa mujibu wa Rasimu, atalazimika kutangaza, ndani ya siku 80 baada ya kupata uongozi na baada ya kuacha uongozi, mali na thamani zake na madeni yake  katika Tume ya Maadili na Uwajibikaji.
Watu mbalimbali wameendelea kutoa maoni kuhusu Rasimu hiyo miongoni mwao wakitaka litumike jina la Tanganyika badala ya Tanzania Bara.
Mkazi wa Kitunda, Dar es  Salaam, David Msangola ambaye ni fundi mchundo, alisema hatua ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kusema kuwa jina la Tanganyika lilikataliwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, haina mantiki kwani hata suala la serikali tatu alilipinga lakini sasa linarudishwa.
“Kama jina la Tanganyika lilikataliwa na Mwalimu Nyerere, mbona tunarudi kule ambako alikataa? Hivyo ni lazima jina la Tanganyika lirudi, kama ilivyo kwa Zanzibar kwani Tanzania ni Muungano wa Tanganyika na Zanzibar,” alisema.
Msangola pia alipendekeza Sera ya Taifa na kuachana na hali ya sasa ya kutegemea sera za chama ambazo zimekuwa zikibadilika kila mwaka na kuingizwa kwenye sera za Taifa.
Alisema kuwapo sera za Taifa kutasaidia mawaziri ambao watateuliwa wakiwa si wabunge kufanya kazi kwa msingi wa sera za Taifa tofauti na sasa.
“Kwa sasa sera za vyama vya siasa ambazo zinabadilika kila wakati wa kipindi cha uchaguzi, ndizo zinatoa mwanya kuingizwa kwa sera za ujanja ujanja ambazo utekelezaji wake ni wa ufuaji,” alisema.
Msangola aliongeza: “Mfano wa sera ya Kilimo Kwanza iliyotokana na sera ya chama na kuingia kwenye Taifa haionekani kwa mwananchi wa kawaida zaidi ya kushuhudia uletwaji wa trekta. Tukiwa na sera ya Taifa, kila chama kitakuja na njia ya kutekeleza sera hiyo.”
Kuhusu kufutwa kwa uchaguzi mdogo, Msangola alipinga hatua ya chama kuchagua mtu mwingine kushika nafasi wakati hakupata muda wa kunadi sera zake kwa wananchi.
“Unaweza kukuta aliyeshindwa akawa ameshindwa kwa kura chache na kuna watu walimpa kura, sasa hatua ya kukipa chama nguvu kuteua mwingine ambaye hakupata fursa ya kueleza sera zake kwa wananchi na ilhali hawakumchagua, naona haifai,” alisema.
Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alitaka wananchi kusoma kwa kina Rasimu ili kuja na maoni chanya kwa ajili ya kupata Katiba nzuri itakayojali maslahi ya wananchi.
Alisema tangu awali chama chao kimekuwa kinapigania kupatikana kwa Katiba nzuri, hivyo wanachofanya sasa ni kuisoma kwa kina Rasimu, tena neno kwa neno, ili hatimaye kuja na maboresho mazuri kwa ajili ya Katiba ijayo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles