![]() |
Kikao cha Bunge mjini Dodoma. |
Wabunge wameipongeza Serikali kwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa barabara kote nchini kwa ufanisi mkubwa, huku Rais Jakaya Kikwete akipongezwa kwa kutafuta fedha za ujenzi wa barabara hizo.
Katika michango yao kwenye mjadala wa Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2013/14, wabunge hao wakiwamo wapinzani, walieleza kuwa kazi nzuri imefanywa na wizara hiyo katika ujenzi wa barabara.
Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM), aliitaka wizara hiyo kusonga mbele na ‘kukaza buti’ kwa kuwa kazi yao nzuri inaonekana, na kuhakikisha wanakamilisha kazi zote walizoanzisha.
Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agripina Buyogera (NCCR-Mageuzi), alisema: “Kwa mara ya kwanza leo nawashukuru sana. Naipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kazi nzuri, ila naomba wanisaidie kuweka lami barabara za Kasulu.”
Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango-Malecela (CCM), aliitaka CCM itembee kifua mbele kwa sababu imefanya kazi kubwa katika ujenzi wa barabara nchini.
Deo Filikunjombe, Mbunge wa Ludewa (CCM), alisema kwa mara ya kwanza anaunga mkono kwa asilimia 100 bajeti, na kuwa watu wa Ludewa wataendelea kumwombea afya njema Dk Magufuli.
“Watu wa Ludewa tutaendelea kumwombea afya njema Dk Magufuli, wewe ni ‘jembe’ letu. Hata ukiomba nafasi ya juu zaidi, Ludewa tutakuwa pamoja nawe,” alisema Filikunjombe na kuwataka mawaziri wasibebane, bali wakumbuke na wabunge.
Mbunge wa Kwela, Ignas Malocha (CCM), alisema Tanzania sasa ina mtandao mkubwa wa barabara za lami, lakini akaomba wananchi walipwe fidia wanapobomolewa nyumba zao, ili kupisha ujenzi.
Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (Chadema), alimpongeza Dk Magufuli kwa kutenga fedha kwa barabara za jimboni mwake, huku Mbunge wa Lushoto, Henry Shekifu (CCM), akitaka fidia mapema kwa wanaobomolewa nyumba zao.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alitamka bungeni kuwa anampigia saluti Dk Magufuli kwa kazi nzuri, na anashukuru kwa wizara hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), alimsifu Dk Magufuli akisema ni mmoja wa mawaziri ndani ya Serikali wanaofanya kazi nzuri.
“Wapinzani huwa tunapongeza watu wakifanya vizuri, kuna mawaziri wanaofanya vizuri. Waziri wa Ujenzi ni mmoja wa mawaziri wanaofanya kazi nzuri, na wapo wengine wanaofanya kazi nzuri kama ya Magufuli, lakini wapo wengine wanaoshangaashangaa tu,” alisema Mkosamali na kutamka kuunga mkono hoja ya Waziri wa Ujenzi.
Mbunge wa Moshi Vijijini, Dk Cyril Chami (CCM) alitaka kutengenezwa kwa barabara zinazokwenda katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, akisema Mlima huo unachangia asilimia 38 ya mapato yote ya Shirika la Hifadhi za Taifa.
Wabunge wengine waliochangia na kuipongeza bajeti hiyo ya Wizara ya Ujenzi ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki – Chadema), Ramo Makani (Tunduru Kaskazini - CCM), Ezekiel Maige (Msalala- CCM), Kaika Telele (Ngorongoro – CCM), Cynthia Ngoye (Viti Maalumu- CCM) na Jerome Bwanausi (Lulindi – CCM).
Wengine waliopongeza kazi nzuri ya wizara hiyo ni Dk Hadji Mponda (Ulanga Magharibi – CCM), Dk Athuman Mfutakamba (Igalula –CCM), Saleh Pamba (Pangani – CCM), John Cheyo (Bariadi Mashariki – UDP), John Komba (Mbinga Magharibi – CCM) na John Chiligati (Manyoni Mashariki – CCM).
Pia Profesa David Mwakyusa (Rungwe Magharibi – CCM) na Margaret Sitta (Viti Maalumu – CCM). Bunge lilipitisha makadirio ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka 2013/14 na leo ni zamu ya Wizara ya Viwanda na Biashara.
Kwa upande wao, wabunge kutoka mkoani Tabora, licha ya kuipongeza Serikali kwa kazi nzuri, waliitaka ikamilishe ujenzi wa barabara za mkoa huo kwa wakati kama zilivyoelezwa katika mikataba, kwani kumekuwa na uzorotaji katika miradi mingi mkoani humo.
Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Aden Rage (CCM) alisema, “Sina hofu na Kamanda Magufuli, nafahamu wewe unachapa kazi. Kwa watu wa Tabora, tunakuomba usimamie ili kuhakikisha barabara zetu zinakamilika kwa wakati. Nyingi mikataba imekwisha na tunadaiwa fidia kubwa.”
Mbunge wa Nzega, Suleiman Zedi (CCM) na Magdalena Sakaya (Viti Maalumu – CCM), waliungana na Rage kutaka barabara za Tabora zikamilishwe mapema, kwa sababu mkoa wao ‘umefungwa’ na mikoa mingine.
Katika hotuba yake, Dk Magufuli alieleza kuhusu utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za lami nchini, ujenzi wa madaraja na vivuko, na kuliomba Bunge limwidhinishe Sh trilioni 1.226, akachape kazi mwaka 2013/14.
Mbunge wa Viti Maalumu, Sitta (CCM), alitaka wapinzani kushukuru kwa kuwa katika majimbo yao, wamejengewa barabara, wakati Tabora, ambao wote una wabunge wa CCM, hakuna barabara za lami za kuingia makao makuu ya mkoa.