Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4550

RASIMU SERA YA DIASPORA KATIKA HATUA ZA MWISHO

$
0
0
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amesema Rasimu ya Sera ya Diaspora iko kwenye hatua za mwisho za maandalizi  na muda si mrefu, itaingizwa kwenye utaratibu wa Kiserikali ili iweze kuwasilishwa kwenye Baraza la Mawaziri.
Aidha, amesema Serikali inaandaa kongamano kwa ajili ya kujadili mustakabali wa wanadiaspora wa Tanzania kutoka nchi zote duniani, ikiwa ni pamoja na kuwakutanisha na makampuni na wafanyabishara mbalimbali.
Alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Watanzania wanaoishi nchini Uingereza kwenye mkutano, uliofanyikia Ofisi za Ubalozi wa Tanzania jijini London.
Kwa mujibu wa Pinda, mchakato wa kuandaa rasimu hiyo, ulihusisha wadau wengi kwa kadri ilivyowezekana ili kupata wigo mpana wa suala zima la diaspora.
“Katika hatua za awali, mbali ya ofisi yangu na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, tuliwashirikisha kwa karibu Umoja wa Wanadiaspora waliorudi Tanzania na wanadiaspora kutoka nchi za Uingereza, Marekani, China, Oman, India na Afrika Kusini ili kupata uzoefu wao kutokea huko waliko.
“Baadaye tukawapeleka wataalamu ambao ni Profesa Samuel Wangwe wa REPOA (Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umasikini), Profesa Joseph Semboja wa Taasisi ya Uongozi na Profesa Faustine Kamuzora wa Chuo Kikuu cha Mzumbe kila mmoja kwa wakati wake na kuwaambia waichambue kadri wawezavyo na kisha watupe mrejesho wao,”alisema Pinda.
Aidha, aliwataja wadau wengine muhimu, waliohusishwa kwenye kuichambua rasimu hiyo kuwa ni Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Wahamiaji, ambao wamebobea katika masuala ya wahamiaji katika nchi mbalimbali duniani.
“Kwa mtazamo wangu hii rasimu imekaa vizuri, kwa sababu tumejitahidi kugusa kila eneo ambalo kwenu lilikuwa na umuhimu wa kipekee, sasa hivi imeshawekwa vizuri kimfumo na inasubiri iingie katika utaratibu wa kiserikali,” alisema.
Kuhusu kongamano, alisema litafanyika kwa siku mbili kuanzia Agosti 14 na 15 mwaka huu, likilenga kuitambulisha rasmi diaspora ama jamii ya Watanzania inayoishi ughaibuni, kama wadau muhimu katika kuleta maendeleo nchini.
Mbali na hilo, alisema, Serikali itapenda kujua idadi yao na wanachofanya ili kama Serikali itahitaji ujuzi na utaalamu wao, iweze kujua itakapoupata.
Alisema kaulimbiu ya kongamano hilo ni “Nyumbani ni Nyumbani”. Aliwataka wajitokeze kwa wingi, kushiriki kongamano hilo, ambalo  litaandaliwa mahsusi kwa ajili yao ;na wasipojitokeza kwa wingi, halitakuwa na maana.
Pinda alisema kongamano hilo, limeandaliwa kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya
Waziri Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na
Umoja wa Wanadiaspora waliorudi nchini.
“Kongamano hilo litasaidia wanadiaspora kuweza kuona fursa mbalimbali zilizopo nchini, kuvutia wawekezaji wageni kuwekeza Tanzania, kukuza utalii nchini, kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa Diaspora pamoja na kuunganisha wawekezaji wa Tanzania na wawekezaji walioko nje ya nchi.”

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4550

Trending Articles