
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema maiti ya mtoto mchanga mwenye jinsia ya kike anayekadiriwa kuwa na umri wa siku moja iliokotwa Julai 3 saa 4:30 asubuhi katika eneo hilo la Kigogo Sambusa na aliyeitupa maiti hiyo hajafahamika.
Alisema maiti iligunduliwa na waokota chupa za maji ambazo zimetumika. Maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili upelelezi kubaini aliyefanya tukio unaendelea.
Katika tukio lingine lililotokea Magogoni Kigamboni Wilaya ya Temeke ilikutwa maiti ya Ramadhani Shomari (2) ikielea kwenye bwawa la maji ya mvua.
Kamanda wa Polisi Temeke, Engelbert Kiondo alisema mtoto huyo alikutwa kwenye bwawa lililopo karibu na nyumba ya Choki Abdalah (45) ambaye ni mvuvi.
Alisema maiti iligunduliwa baada ya harufu kali kusikika katika eneo hilo.
Mtoto huyo alitoweka kwao katika mazingira ya kutatanisha tangu Juni 21 mchana alipotumwa kwenda kumwaga maji machafu nje ya nyumba yao. Maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Katika tukio la tatu lililotokea Buyani Ukonga Wilaya ya Ilala ilikutwa maiti ya mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na miaka kati ya miwili na mitatu ikielea kwenye bwawa linalohifadhi maji ya mto Mwizati.
Kamanda wa Polisi wa Ilala, Marietha Minangi alisema maiti ilikutwa haina jeraha na chanzo cha kifo hakijafahamika. Marehemu alipotea kwao tangu Julai 2 saa 5:00 asubuhi hadi maiti ilipokutwa inaelea kwenye maji na iliopolewa na wananchi na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.