Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

HIVI NDIVYO JAMBAZI ALIVYOSHAMBULIA BASI LA MAGEREZA

$
0
0
Basi la Magereza linalobeba mahabusi na wafungwa, jana lilishambuliwa kwa risasi na jambazi na kusababisha askari wawili na mahabusi mmoja kujeruhiwa. 
Shambulio hilo lilifanyika saa 7:50 mchana katika Barabara ya Mwai Kibaki, eneo la Hoteli ya Regency, wakati basi hilo likitokea Mahakama ya Kawe, kwenda Mahakama ya Kinondoni kabla ya kurudi katika Gereza la Segerea.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura alisema jana kuwa pamoja na shambulio hilo, hakuna mahabusi yeyote aliyetoroka.
“Mtu asiyefahamika alishambulia kwa risasi gari la Magereza kulia na nyuma na baadaye kutoweka bila kufahamika, watu watatu wamejeruhiwa,” alisema.
Aliwataja watu hao kuwa ni dereva wa gari hilo Sajenti Msofe aliyechubuka kiganja cha mkono wa kulia, askari wa kike Koplo Doto aliyepata majeraha kifuani upande wa kulia na mahabusi wa kike aliyechubuka kwenye paji la uso. 
Wambura alisema Polisi imeanzisha uchunguzi kubaini muhusika huyo na nia yake ya kushambulia basi la mahabusi.
Mashuhuda wa shambulizi hilo, walidai kuwa majambazi walikuwa wanataka kumdhuru mtu aliyekuwa kwenye gari iliyokuwa mbele ya basi la magereza.
“Walipoliona basi hilo walidhani kuna askari mwenye silaha, wakaanza kushambulia,” alisema shuhuda ambaye hakutaka  jina lake liandikwe gazetini.
Wakati huo huo, watu watatu wamekufa katika matukio tofauti yaliyotokea jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Englbert Kiundo alisema katika tukio la kwanza, mkazi wa Yombo Vituka wilayani Temeke, Baraka Nyaulo (20), alikutwa  amekufa baada ya kujinyonga kwa kutumia mkanda wa begi.
Nyaulo aliyepanga katika nyumba ya Veronica Landa, alitundika mkanda wa begi kwenye kenchi na kujinyonga na kwenye simu yake ya mkononi, kulikutwa ujumbe usemao; “Bora tufe ugonjwa umekua mbaya sana”.  
Tukio la pili ni la ajali, ambapo dereva asiyetambulika alimgonga mpanda baiskeli Salum Omary (32), mkazi wa Tandika katika eneo la Mtongani na kufa papo hapo. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke na dereva anatafutwa.
Katika tukio linguine nalo la ajali, dereva Joseph Dastan (36) aliyekuwa anaendesha daladala lenye namba T 698 CNZ, aina ya Toyota Costa linalofanya safari zake Ilala-Buguruni Malapa, alimgonga mtembea kwa miguu katika barabara ya Uhuru eneo la Buguruni Rozana na kusababisha kifo chake
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema mtu huyo anayekadiriwa kuwa na kati ya miaka (20-25) aligongwa na basi hilo wakati anavuka barabara na kufa akiwa njiani kupelekwa hospitali na mwili umehifadhiwa Hospitali ya Amana.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

Trending Articles