Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4593

MWAKYEMBE AWATIMUA KAZI WATUMISHI WA WIZARA TATU

$
0
0
Watumishi 13 wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam, wametimuliwa kazi na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kwa tuhuma za kuchafua sura ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa, kuendekeza rushwa na kunyanyasa raia wa kigeni.
Watumishi hao ambao hawatakiwi kufanya kazi uwanjani hapo tena, sita wanatoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, watano wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakati watumishi wawili ni wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.  
Kutokana na tuhuma hizo, Dk Mwakyembe amewarudisha watumishi hao kwenye wizara zao ambazo ndio mamlaka zilizowaajiri, kwa ajili ya kuchukuliwa hatua zaidi za kinidhamu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Dk Mwakyembe alidai vitendo vilivyofanywa na watumishi hao ni vya ovyo na kipuuzi na vinasababisha wageni wanaofika nchini  kudhani kwamba vitendo hivyo ndio tabia ya Watanzania.
Watumishi wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika wanaodaiwa kuendekeza rushwa ni Teddy Mwasenga, Esther Kilonzo, Rehema Mrutu, Mary Kadokayosi, Kisamo Samji na Aneth Kiliyanga.
Watumishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ni Agness Shirima, Hamis Bora, Valeri Chuwa, Elingera Mghase na Remedius Kakulu. Watumishi wawili wanaotoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ni Eshi Ndosi na Anne Setebe.
"Ikifika saa sita leo mchana (jana) sitaki kuwaona watumishi hao kwenye uwanja wa JNIA, nimeagiza waondolewe katika uwanja kuanzia muda huo, wizara zao nimewapelekea ushahidi wa vitendo vichafu wanavyofanya vya rushwa na kunyanyasa raia wa kigeni uwanjani hapo ili wachukue hatua," alisema Dk Mwakyembe.
Abiria wanaodaiwa kunyanyaswa na watumishi wa wizara hizo tatu ni raia kutoka nchi za India, China na nchi za Uarabuni, ambao Dk Mwakyembe alisema kutokana na manyanyaso hayo kuongezeka, baadhi ya raia kutoka nchi hizo walienda ofisini kwake kumlalamikia kuhusu suala hilo.
Waziri huyo alisema baada ya kulalamikiwa na raia wa nchi hizo kuwa wanabaguliwa na wanakaguliwa sana kuliko abiria wanaotoka nchi zingine, alienda uwanjani hapo na kuagiza Idara ya Usalama kukagua kamera za usalama (CCTV) zilizoko uwanjani hapo, ili kubaini watumishi wanaoendesha vitendo vya rushwa na unyanyasaji kwa raia wa kigeni.
Alisisitiza kuwa alilazimika kutoa agizo hilo, kwa vile vitendo hivyo vichafu vinaharibu sura ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa na mgeni yeyote akifika uwanja wa ndege na kukuta taratibu za ovyo zinafanyika, atachukulia kuwa nchi hiyo inaendeshwa kwa taratibu hizo za ovyo.
 “Kama ni mwekezaji sura ya nchi anaanza kuipata uwanja wa ndege, akifika pale akanyanyasika na kudaiwa rushwa, mtu huyo atachukulia kuwa ndio tabia Watanzania na anaweza kufikiria kuhamisha fedha zake na kuzipeleka nchi nyingine," alisema Waziri huyo.
Alitoa mfano kuwa Wahindi, Waarabu na Wachina kwamba wamekuwa na tabia ya kuingiza bidhaa za vyakula kutoka katika nchi zao na wanapofika uwanjani hapo, maofisa kilimo na uvuvi wamekuwa wakiwanyang'anya kwa maelezo kuwa bidhaa hizo zimepigwa marufuku kuingizwa nchini.
"Lakini cha ajabu abiria hao wakitoa rushwa, wanarudishiwa bidhaa hizo na wale wasiotoa rushwa bidhaa hizo zinachukuliwa na maafisa hao na kwenda kula vyakula hivyo. Iweje iwe haramu kuingizwa nchini lakini wao waende kula vyakula hivyo?
"Ni kweli kuna vyakula haviruhusiwi kuingizwa na  vinapokamatwa ni lazima viteketezwe, lakini maofisa hawa hilo hawalifanyi, wanachofanya ni kula rushwa na mwenye bidhaa anaposhindwa kutoa rushwa, bidhaa zake wanachukua wenyewe kwa matumizi yao," alisema Dk Mwakyembe.
Alisema kwa upande wa maofisa kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wamekuwa wakitumia Chanjo ya Homa ya Manjano kuwanyanyasa abiria wa kigeni. "Nimeambiwa kuwa ili wapate rushwa baadhi ya wageni hao wanatishiwa kuchomwa sindano na anapotoa rushwa, anaachiwa."
Alisema suala la homa ya manjano katika nchi zingine sio ugonjwa tena, hivyo wageni wanashangaa wanapofika uwanjani hapo kukuta wanadaiwa kadi hizo na wale ambao hawana, watumishi wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, wanatumia fursa hiyo kufanya vitendo vya rushwa.
"Watanzania wanapoenda nje ya nchi, hawadaiwi jambo hilo kwa sababu kila nchi inaamini kuwa hadi mtu asafiri ni lazima ametekeleza agizo hilo, lakini sisi tunatumia mwanya huo kuharibu sura ya nchi mbele ya wageni, kwa kweli hili sitakubali liendelee kufanyika," alisema Waziri huyo.
Dk Mwakyembe alitumia fursa hiyo kutoa onyo kwa watumishi wengine wa wizara hizo waliobakishwa uwanjani hapo ambao alisema hata wao sio wasafi licha ya kubakizwa, akaongeza kuwa ameanza na hao ambao walikithiri kunyanyasa wageni.
Amesema kama kutajitokeza vitendo hivyo tena, hatawarejesha kwenye wizara zao kuchukuliwa hatua, bali atakachofanya ni kuwapeleka kwanza mahabusu na baada ya wiki tatu ndio atawarejesha kwenye wizara zao ili hatua za kinidhamu zichukuliwe.
Aliagiza pia watumishi wengine wa wizara hizo watakaopangiwa  kazi uwanjani hapo, wahakikishe wanalinda sura ya nchi mbele ya jumuiya ya kimataifa na sio kuichafua nchi kwa kuendekeza rushwa, hongo na vitendo vingine vya kipuuzi.
Pia aliagiza watumishi hao kuvaa sare zao kama wanavyofanya watumishi wa Polisi, Uhamiaji. "Kama hawana, wavae sare zingine zinazovaliwa na watumishi wa idara zingine ili watambulike kwa shughuli wanazofanya."
Alitaka mtumishi asiyefuata agizo hilo aondolewe kwenye ofisi za uwanja huo na asikanyage tena katika eneo hilo kwa shughuli za kikazi.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Dk Mwakyembe alifanya ziara ya kushitukiza uwanjani hapo baada ya kupata tuhuma hizo, ambapo aliagiza maofisa usalama kupitia matukio ya miezi mitatu yaliyorekodiwa na kamera za kiusalama za CCTV, kubaini wafanyakazi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kwa wageni ili wachukuliwe hatua.
Dk Mwakyembe tangu ateuliwe kuwa Waziri wa Uchukuzi, amekuwa mwiba kwa vigogo na wafanyakazi wa kawaida waliokutwa na tuhuma mbalimbali katika utendaji kazi.
Miongoni mwa watendaji waliokwishaonja joto ya Dk Mwakyembe wamo vigogo 23 wa Mamlaka ya Bandari (TPA).
Vigogo hao walikutwa na tuhuma za kuwa na mgongano wa kimaslahi katika utendaji wao kwa kuwa baadhi walibainika kuwa na kampuni zao ndogo zinazohudumia bandari ambayo pia ni viongozi.
Kwa mujibu wa Dk Mwakyembe, kampuni hizo zilipochunguzwa kwa Msajili wa Makampuni (Brela), ilibainika ni kampuni za mfukoni kwa kuwa hazikuwa na usajili.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4593

Trending Articles