Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa ameelezea kusikitishwa kwake na utendaji usioridhisha wa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, akitolea mfano kushindwa kutekeleza maamuzi ya vikao vya Baraza la Madiwani.
Miongoni mwa maamuzi ambayo hayajafanyiwa kazi ni kuhamishia familia 53 katika shamba la Ugoro, lililokuwa linamilikiwa na mwekezaji.
Lowassa ambaye ni `mchungu’ katika suala la uuzaji ardhi wilayani humo, aliyasema hayo juzi akiwa katika Kijiji cha Lekruko Kata ya Nanja alikokwenda kuzindua Bwawa la Migwara, lilijengwa na Kampuni ya Meeri, ambako alitumia fursa hiyo kuwalaumu madiwani wa Monduli kwa kufanya kazi kwa kasi ndogo mithili ya konokono.
Bwawa hilo lililogharimu Sh milioni 870 linatarajiwa kuhifadhi maji yenye lita za ujazo 218,381,000.
Aidha, kukamilika kwa bwawa hili kutaongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya maji Monduli kutoka asilimia 53.85 Desemba mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 58.9 mwezi huu.
“Madiwani mnachelewa kutekeleza maamuzi yanayochukuliwa, angalia tangu tulipokubaliana kuchukua shamba la mwekezaji wa Ugoro pale Makuyuni mpaka leo hakuna kilichofanyika.
“Tulipitisha azimio kwamba familia 53 zinazoishi maeneo ya Jeshi la Wananchi zihamie katika shamba hilo, lakini hadi leo hii hakuna kilichofanyika. Madiwani mnafanya uamuzi pole pole kama konokono,” alisema Lowassa.
Katika harakati hizo za kupigania ardhi isiendelee kununuliwa na watu wachache kisha kutotumiwa, Lowassa alisema haiingii akilini kuona Halmashauri imechukua baadhi ya mashamba kwa ajili ya manufaa ya wananchi, kisha haiyaendelezi au kushindwa kupangia matumizi mengine.
Akizungumza kuhusu suala la maji wilayani Monduli, alisema maji wilayani humo, yameendelea kuwa changamoto na hasa katika namna ya kuyapata licha ya kuchimba visima.
“Ndugu zangu kuna maneno yanaendelea huko nje, eti maji Monduli ni machafu, naomba niwaambie haya ndio aina ya maji yanayopatikana Monduli tangu wakati wa Utawala Hayati Edward Sokoine, aliyewahi kuleta watu wa kuchimba visima vya maji hakufanikiwa.
“Nimejaribu pia hata mimi kuendelea kutafuta maji ya chini bado hakuna maji chini ya ardhi ndio maana tukaamua kuja na njia mbadala ya kujenga mabwawa ili tuvune maji ya mvua, hao wanaosema tunaowamba walete nguvu zao nao kujaribu kuchimba badala ya kusema tu,” alisema Lowassa.