Idadi kubwa ya wajawazito katika Tarafa ya Mwese, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi, wanalazimika kutohudhuria kliniki na kujifungulia nyumbani, kwa madai ya kukataliwa kuhudumiwa katika kliniki ya eneo hilo, wanapokwenda bila ya wenza wao.
Inadaiwa kuwa wanaume wengi katika Tarafa hiyo ya Mwese, wanakataa kuwasindikiza kliniki wenza wao kwa hofu kuwa watalazimishwa kupima afya zao, hususani Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).
Diwani wa Viti Maalumu wa Kata ya Mwese, Theodola Kisesa alibainisha hayo wakati akichangia katika Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmshauri ya Wilaya ya Mpanda kilichoketi juzi mjini hapa.
Akifafanua, alisema wajawazito katika tarafa hiyo wamekuwa wakikataliwa kupimwa afya zao na watoa huduma katika kliniki, wanaposhindwa kuongozana na wenza wao wa kiume ili nao waweze kupima afya zao.
“Watoa huduma katika kliniki hii ya Tarafa ya Mwese wanawataka wajawazito kuandamana na wenza wao ili nao waweze kupima afya zao katika jitihada za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama na mtoto… sasa wanaume wengi wamekuwa wanasita.
“Hivyo baada ya kukataliwa wajawazito wengi wamekuwa wakilazimika kujifungulia nyumbani au kwa wakunga wa jadi ambao hawana ujuzi wa kutosha hivyo kusababisha maisha ya mama na mtoto ambaye hajazaliwa kuwa mashakani, “ alisisitiza.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk Joseph Msemwa akichangia alisisitiza kuwa jukumu la kupimwa afya, sio la mama peke yake, bali kwa wenza wote.
Alisema anazo taarifa kuwa mama akipimwa na kugundulika hana maambukizi ya VVU, mwenza wake anaamini naye yuko salama, jambo alilosisitiza kuwa halina ukweli.
Aidha, aliagiza wajawazito wahudumiwe katika vituo vya kutolea huduma bila ya ubaguzi, hata kwa ambao hawakuongozana na wenza wao.