Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

KATIBU WA CHADEMA, WENZAKE WASHIRIKI MBIO ZA MWENGE

$
0
0
Viongozi wa vyama vya upinzani mjini Morogoro, wameshiriki katika Mbio za Mwenge wa Uhuru.
Viongozi hao walioshiriki katika mbio hizo ni Katibu wa Chadema wa Mkoa wa Morogoro, Ngonyani Boniface, Mwenyekiti wa TLP Wilaya ya Morogoro, Juma Kasielo, Mwenyekiti wa Chama cha Jahazi Asilia, Ismail Rashid  na Katibu wa UDP Wilaya ya Morogoro, Salum Mwandule. 
Viongozi hao kwa pamoja, walipata fursa ya kuushika Mwenge wa Uhuru sambamba na viongozi wengine wa Serikali ya wilaya hiyo na baadhi ya wananchi wa Kata ya Kilakala. 
Kwa upande wake, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Rachel Kassanda, aliwapongeza viongozi hao wa vyama vya  upinzani mkoani Morogoro,  kwa kutambua umuhimu wao wa  kushiriki kikamilifu kwenye mbio za Mwenge wa Uhuru za mwaka 2014. 
Kassanda alitoa pongezi hizo, kabla ya kutoa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru katika Kata ya Kilakala katika Manispaa ya Morogoro, juzi. Alisema hayo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa soko. 
Uongozi wa Serikali ya Wilaya ya Morogoro ukishirikiana na  Manispaa ya Morogoro, ulitoa mwaliko kwa viongozi wa Vyama vya Upinzani ili washiriki mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu. 
Akitoa ujumbe wa Mwenge wa Uhuru  kwa wananchi katika  eneo hilo, Kassanda alisema kuubeza Mwenge wa Uhuru ama kuwatukana waasisi wa taifa hili ni utovu wa nidhamu. 
Alisema inapaswa kila mmoja, kulaani na kuwakemea wale wenye tabia hizo. 
“Nimeambiwa hapa leo kuna viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani...hili ni jambo zuri kwani Mwenge wa Uhuru ni wa Watanzania wote, bila kujali itikadi ya chama, unatuunganisha sisi Watanzania, bila kujali dini, kabila wala itikadi ya chama...unahubiri amani, upendo na umoja “ alisema Kiongozi huyo. 
Aliongeza," Nimefurahi kuwaona viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani  kwenye tukio hili...na hii inaonesha juu ya  umuhimu wa Mwenge wa Uhuru kwa Watanzania". 
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi, viongozi hao waliupongeza uongozi wa Serikali ya Wilaya na Halmashauri ya Manispaa kwa kitendo cha kuwashirikisha kwa kuwapa  mwaliko. 
“ Tumeletewa mialiko, pia tumepewa usafiri, hili jambo linaonesha Mwenge wa Uhuru hauna chama, ni wa Watanzania wote, nasi tunaungana na wana Manispaa kwenye tukio,” alisema Rashid ambaye ni Mwenyekiti wa Jahazi Asilia. 
Kwa upande wake, Ngonyani wa Chadema alisema Chadema haipingi kuwepo kwa mbio za Mwenge wa Uhuru, isipokuwa inahoji juu ya   matumizi ya fedha. 
“Mimi binafsi sina tatizo na Mwenge wa Uhuru kukimbizwa, ndiyo maana leo (juzi) nipo hapa  Kilakala kwenye kata ninayoishi na kushiriki kikamilifu  katika shughuli za kuweka jiwe la msingi la soko,” alisema Katibu huyo wa Chadema wa Mkoa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

Trending Articles