Magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yaliyokuwa yamewekwa katika orodha ya Urithi wa Dunia ulio hatarini kutoweka, yamerudishiwa hadhi yake ya awali ya Urithi wa Dunia.
Uamuzi wa kuyarudishia hadhi magofu hayo yaliyopo Kilwa, mkoani Lindi, umefikiwa wakati wa Mkutano wa 38 wa Kamati ya Urithi wa Dunia unaofanyika Doha, Qatar.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamati ya Urithi wa Dunia imeridhika na juhudi zilizofanywa kuyaboresha maeneo hayo na hivyo kutangaza rasmi kuwa hayako tena katika hali hatarishi.
Aidha, kutokana na juhudi hizo, wajumbe wa kamati hiyo wamepongeza Serikali kwa juhudi kubwa iliyofanyika na imekuwa mfano mzuri katika kutekeleza makubaliano ya kimataifa hususani uendelezaji na uhifadhi wa maeneo ya urithi wa Dunia.
Kwa upande wa Serikali inayowakilishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahamoud Mgimwa, Katibu Mkuu Tarishi Kibenga na Mkurugenzi wa Malikale, Donatius Kamamba katika mkutano huo, imesema ili kuhahakisha eneo hilo halirudi tena katika orodha hiyo, Wizara itaendelea kulipa umuhimu mkubwa.
Magofu hayo yaliingia katika orodha ya kuondolewa mwaka 2004 katika mkutano uliofanyika Sozhou, China. Ilielezwa kuwa, sababu za magofu hayo kuingizwa katika orodha ya maeneo yaliyo hatarini ni kutokana na kuwa katika hali ya kuharibika na kuoza hivyo kusababisha sehemu ya majengo ya kihistoria kudondoka.
Wataalamu waliainisha visababishi kama vile kukosekana kwa mipaka ya eneo husika na kinga ya eneo, (Mpango wa Usimamizi wa Ardhi), na Usimamizi stahili, kuharibika kwa miundo la kiujenzi, mmomonyoko kutokana na athari za bahari, ujenzi wa nyumba za wananchi kwa kutumia matumbawe, kutokuwa na kamati ya mashauriano imara katika maeneo na kutosimamiwa ipasavyo kwa mpango wa uhifadhi na usimamizi.