Katika kuongeza idadi ya Watanzania wenye vyeti vya kuzaliwa, Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), imeamua kuzungukia shule kuandikisha wanafunzi wasiokuwa navyo.
Kwa kuanzia, imeandikisha wanafunzi 7, 400 wa shule za msingi Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kwenye Maonesho ya Utumishi wa Umma, Ofisa Habari wa RITA, Jafari Malema alisema wanafunzi hao wameandikishwa chini ya mpango wa uandikishaji watu wenye umri kati ya miaka sita hadi 18 ambao hawakuandikishwa awali.
Alisema tangu kuanza kwa kazi hiyo miezi mitatu iliyopita, wamefanikiwa kuandikisha wanafunzi 7,400 wa shule za msingi 105 wilayani Ilala.
“Tumeshamaliza shule za msingi, tutahamia kwenye shule za sekondari, baadaye tutahamia wilaya nyingine na kukamilisha katika nchi nzima hatua kwa hatua,” alisema.
Taarifa za Msingi za Kidemografia, Kijamii na Kiuchumi zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012, zinaonesha asilimia 15 ya Watanzania walikuwa na vyeti vya kuzaliwa kwa mwaka 2012, Zanzibar ikiwa na asilimia 71 na Tanzania Bara asilimia 13.