Mkazi wa Kijiji cha Masuguru, Kata ya Masagala wilayani Kishapu mkoani hapa, Juma Masalu (25) ameuawa kwa kupigwa risasi akituhumiwa kuvamia Mgodi wa Almasi wa Mwadui kwa lengo la kuiba mchanga wenye madini.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Kihenya Kihenya alisema tukio hilo ni la Juni 13 saa 5 usiku, mwaka huu.
Inadaiwa kijana huyo aliongozana na watu wengine 20 kuvamia ndani ya mgodi huo unaomilikiwa na Kampuni ya Williamson Diamond.
Kwa mujibu wa Kamanda, walinzi wa Kampuni ya Zenith inayolinda, walipambana na kundi hilo kwa kurusha risasi huku ‘wavamizi’ hao wakirusha silaha za jadi, hususani mishale, mikuki na makombeo.
Alisema wakati wengine walikimbia, Masalu alijeruhiwa kwa risasi na kufariki dunia baadaye.
Mtuhumiwa mwingine, Emmanuel Charles (23) mkazi wa Kata ya Majimaji mjini Maganzo, alijeruhiwa na anashikiliwa na polisi wakati akitibiwa kwenye zahanati ya mgodi huo.
Wakati huo huo Kamanda huyo alisema walinzi wa Kampuni hiyo ya Zenith wanaodaiwa kupambana na kundi hilo, walitelekeza silaha na kukimbia kusikojulikana baada ya kusababisha mauaji hayo wakihofu kukamatwa.
Polisi inaendelea kusaka watu wengine wanaodaiwa kuwa miongoni mwa waliovamia mgodi huo.