Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

MVUA YAKWAMISHA ABIRIA WA MIKOANI MASAA 12 NJIANI

$
0
0
Mvua iliyoanza kunyesha mwishoni mwa wiki, imeendelea kuleta kizaazaa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo  kusababisha maelfu ya abiria kukwama kusafiri kati ya Dar es Salaam na mikoa  mingine kupitia Barabara ya Morogoro.
Mawasiliano yalikatika kutokana na  daraja la mto Ruvu, kuzingirwa na maji na lingine lililoko eneo la Visiga, kingo zake kutitia.
Licha ya athari katika miundombinu zilizosababisha magari na abiria kusota katika eneo hilo la Ruvu mkoani Pwani kwa zaidi ya saa 12,  kwa upande wa Mkoa wa  Morogoro vifo viwili vimeripotiwa kutokea baada ya watu wawili kufunikwa na maporomoko ya udongo, yaliyosababishwa na mvua.
Wakati Rais Jakaya Kikwete alikwenda kutembelea maelfu ya abiria waliokwama kwenye daraja la Ruvu,  kwa upande wa Dar es Salaam hali iliendelea kuwa tete, kutokana na nyumba kadhaa kuzingirwa na maji.
Katika harakati za kutaka kwenda kukagua athari za mafuriko katika Jiji la Dar es  Salaam, Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal na viongozi wengine, walinusurika kifo baada ya helikopta waliyotaka kuitumia kuanguka.
Viongozi wengine waliokuwamo kwenye helikopta hiyo ni Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na Kamanda wa Polisi,  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Sadiki alithibitisha kuwepo ajali hiyo jana. Kwa mujibu wake, kulitokea hitilafu wakati ikitaka kuruka kwenye Uwanja wa Julius Nyerere (JNIA) jana asubuhi.
"Wote tumetoka tukiwa wazima na kwenda hospitali. Tumethibitishwa hatujapata madhara yoyote," alisema kwa njia ya simu.
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais, Boniface Makene aliyekuwa kwenye helikopta hiyo, alisema, "Ni kweli tulikwenda uwanja wa ndege (JNIA) kwa sababu tulikuwa na ziara ya kukagua athari za mafuriko, helikopta tuliyokuwa tuitumie, ilipata hitilafu na kuanguka. Hata hivyo hatukupata madhara yoyote."
Kwa mujibu wa Makene, Makamu wa Rais Bilal aliendelea na ziara yake kwa kwenda kukagua Daraja wa Mpiji linalotenganisha Dar es Salaam na Pwani na kujionea athari zilizotokana na mvua zilizonyesha mwishoni mwa wiki.
Habari zilizopatikana zinasema kuwa helikopta hiyo ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), ilishindwa kuruka kwa kwenda mbele na badala yake iliruka kwa kurudi nyuma, hali iliyosababisha panga moja kujipigiza kwenye moja ya paa la karakana ya uwanjani hapo na hivyo kuanguka.
Alipotafutwa, msemaji wa JWTZ, Luteni Kanali Komba kueleza kwa kina chanzo cha hitilafu ya helikopta hiyo, hakupatikana baada ya simu yake ya mkononi kuita bila majibu.
Rais Jakaya Kikwete jana alitembelea abiria waliokuwa wakielekea mikoa mbalimbali baada ya kukwama kutokana na Daraja la Ruvu, kujaa maji ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha nchini.
Awali, Kikwete alitembelea daraja la Maili 35 lililoko Kata ya Visiga wilayani Kibaha, lililotitia na kufanya magari kupita upande mmoja huku yenye abiria kulazimika kuwashusha. Magari ya mizigo hayakuruhusiwa kupita.
Akizungumza na maelfu ya abiria  waliokwama tangu alfajiri huku wengine wakiwa wamekwama tangu jana usiku, Kikwete alisema ni mara yake ya kwanza kuona mafuriko kwenye eneo hilo, ambalo liko kwenye mkondo wa mto Ruvu.
"Poleni sana kwa tatizo lililowakuta, kwani majanga kama haya ni ya asili na hatuna jinsi ya kufanya, tuombe Mungu asaidie ili maji yasizidi kujaa badala yake yapungue ili muweze kuendelea na safari zenu," alisema Kikwete.
Kikwete ambaye alifuatana na Mkewe, Mama Salma  na mbunge mteule wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, alisema mafuriko hayo ni makubwa na yameleta maafa.
Alisema hadi jana watu 10 walikuwa wamepoteza maisha jijini Dar es Salaam.
"Tatizo hili ni mipango ya Mungu hivyo tuwe wavumilivu, tukisubiri maji yapungue ili safari iweze kuendelea kwani wataalamu walisema kuwa endapo maji yataendelea kupungua ikifika saa 10 jioni majAribio ya kupita magari yataanza," alisema Kikwete.
Aidha, alisema kuwa wafanyabiashara wa chakula wanapaswa kutopandisha bei za vyakula ili kuweza kusaidia abiria hao waliokwama tangu alfajiri kwenye barabara hiyo ya Morogoro - Chalinze.
"Wauzaji wa vyakula acheni uroho na msipandishe bei za vyakula, kwani wenzenu wako kwenye matatizo na baadhi yao hawana fedha hivyo hawataweza kumudu gharama kubwa za chakula. Tutahakikisha hali ya hapa inakuwa vizuri,"  alisema Kikwete.
Aliutaka uongozi wa kikosi cha Ruvu JKT kilichopo Ruvu, kuhakikisha wanaandaa chakula kwa bei nafuu  watu wengi waweze kumudu kukinunua. Aliahidi kama kutakuwa na upungufu, wataongeza ili kiweze kukidhi mahitaji na wawatumie vijana huko kambini, kusaidia kuhudumia abiria hao.
Alisema pia kwamba Daraja la Bagamoyo kwenda Dar es Salaam, limeharibiwa na mvua.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani,  Mwantumu Mahiza alisema walitoa hadhari kwa madereva wa mabasi kutotumia barabara hiyo, lakini asubuhi baadhi  yalipita na kukwama.
"Tuliwaambia wasije kwani kuna lori lilizama lakini wao wakaja na kama mnavyoona hali ndiyo hiyo, ni mbaya sana na tunawaambia wengine wanaotumia barabara hii wasije hadi watakapotangaziwa ili kuwaondolea usumbufu abiria",  alisema Mahiza.
Mmoja wa madereva wa magari ya mizigo la kwenda Zambia, Ally Ahmed alisema  walifika hapo tangu juzi usiku, lakini walishindwa kupita, kutokana na maji kujaa kwa kuwa barabara ilikuwa haionekani.
Kwa mujibu wa abiria, bei ya chakula ilipandishwa kutoka Sh 1,500 hadi Sh 4,000 kwa sahani, hali iliyosababisha waombe serikali iingilie kati.
Baada ya kusota kwa zaidi ya saa 12, magari yalianza kuruhusiwa kupita jana jioni. Kwa upande wa daraja la Visiga, magari yaliruhusiwa kupita upande mmoja wa barabara na kuzuiwa kwenye upande uliotitia.  Hali hiyo ilitokana na kiasi cha mvua iliyonyesha jana kuwa kidogo, ikilinganishwa na ya siku mbili kabla.
Kabla ya mabasi kuruhusiwa kuendelea na safari, pia katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam, abiria  walibaki njia panda bila kujua hatma yao.
Katika lango la kuingilia mabasi kituoni hapo, kulikuwa na mtu mwenye kipaza sauti, akitaarifu abiria kuwa hakutakuwa na usafiri na kuhadharisha wasikate tiketi.
"Mimi nimepewa taarifa na askari wa kituo hiki kuwa nitangaze hakuna usafiri kwa leo (jana), hivyo abiria waliokata tiketi wafuate ofisi za mabasi husika ili waweze kurudishiwa nauli zao," alisema kijana huyo.
Mkaguzi wa magari kituoni hapo, Erasto Bakari alisema alipokea simu kutoka kwa  Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed   Mpinga akitakiwa kusitisha usafiri kwa mabasi ya mikoani, kutokana na kukatika kwa daraja la Visiga na kujaa kwa maji katika daraja la Ruvu, yote ya mkoani Pwani.
Alisema kwa abiria waliotaka kubadilishiwa tiketi waweze kusafiri wakati mwingine, walipaswa kufanya hivyo na walipewa nauli yao na kuondoka eneo hilo.
Aidha alisema kulingana na agizo alilopokea kutoka kwa Kamanda Mpinga haijulikani zuio hilo linachukua muda gani na kwamba hali itakapotengemaa usafiri utarudia kama kawaida.
Katika eneo la Msasani Bonde la Mpunga, Manispaa ya Kinondoni, mwandishi alishuhudia  maji yaliyojaa kwenye makazi ya watu huku wananchi wa eneo hilo, wakilalamikia ujenzi holela, uliosababisha mkondo wa maji kuelekea baharini kuzuiwa.
Kuhusu usafiri wa daladala katika jiji la Dar es Salaam, hali ilikuwa mbaya katika Barabara ya Morogoro  eneo la Magomeni, ambako daraja la Jangwani lilifurika maji.
 Daladala zinazokwenda Posta na Kariakoo kupita njia hiyo, zililazimika kuzungukia Kigogo katika Manispaa ya Ilala  kupitia Jengo la Yanga na hivyo kuwepo msongamano mkubwa.
Aidha, ofisi za kampuni ya Strabag inayojenga miundombinu chini ya Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) zilizoko eneo Jangwani, zilizingirwa na maji.
Watu wawili wa familia moja katika Kata ya Mlimani  Manispaa ya Morogoro, wamekufa baada ya  kuangukiwa na maporomoko ya udongo yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku tatu mkoani Morogoro.
Waliofariki ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Bungodimwe, Walda Abdul (15) na dada yake, Salma Abdul (18) waliokutwa na maafa hayo wakiwa nje ya nyumba yao.
Diwani wa Kata hiyo, Husseis Ramia, alisema hayo jana mjini Morogoro na kusema vifo hivyo vilitokea juzi.
Kwa mujibu wa diwani,  mmoja alifia eneo la tukio na mwingine alifia kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro,  alikokimbizwa kupatiwa matibabu.
Kwa mujibu wa baba mlezi wa watoto hao,  Juma Rashid,  walikuwa wanaishi na   bibi yao hadi pale walipokutwa na mauti.
Mganga aliyekuwa zamu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro, Dk Francis Msagati, alisema vifo vyao vilitokana na kukosa hewa baada ya kuangukiwa na udongo.
Akielezea mazingira ya ajali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya  Morogoro, Said Amanzi alisema udongo huo ulisombwa na maji kutoka mlimani na kisha kuwafunika watu hao.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles