Image may be NSFW. Clik here to view. ![]() |
Balozi Seif Ali Iddi. |
Balozi Iddi amesema kauli hiyo ya Hamad ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ, inalenga kugawa Watanzania.
Katika mkutano wa hadhara visiwani Zanzibar, Hamad alisema Wazanzibari hawataki muundo wa serikali mbili akisisitiza hauwezi kudumisha Muungano uliopo sasa kuwa imara lakini utaufanya Muungano huo kuvunjika.
Aidha alisema CUF itaendelea kushinikiza kuwepo kwa Muungano wa mkataba ambao ndiyo utanusuru Muungano na kufanya wananchi wa Zanzibar kuwa huru zaidi na mamlaka kamili ya dola.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Balozi Iddi alisema, kauli zinazoendelea kutolewa na kiongozi huyo ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa SMZ, zinalenga kugawa Watanzania.
"Wananchi wa Zanzibar wasitishwe na kauli za Maalim Seif, Zanzibar itaendelea kuwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania vizuri wananchi wameanza kugundua kuwa anayosema ni uongo mtupu,” alisema.
Alisema kauli ya kwamba Wazanzibari wote hawataki Muungano wanataka mkataba , siyo sahihi.
"Ni Wazanzibari gani hao wanaowasemea mbona sisi hapa pia ni Wazanzibari na hatuna msimamo huo?
Vilevile kitendo cha baadhi ya viongozi hao wa kisiasa kutaka Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara kuacha shughuli zao za kimaisha za kila siku na kurudi Zanzibar, hii inaashiria viongozi walivyo na nia mbaya katika kutaka kuvunja umoja wa nchi na Muungano," alisema.
Akizungumzia kauli ya Seif kwamba Wazanzibari wafanye kura ya maoni kuhoji uwepo au kutokuwepo kwa Muungano, Balozi Iddi alisema: "Nasisitiza Muungano huu utakuwepo, utadumu na kuendelea kudumu na hakuna atakayeweza kuuhujumu au kuuvunja kwa maslahi yake binafsi, sikatai changamoto za Muungano zipo lakini nyingi zimeshafanyiwa marekebisho au utatuzi.”
Aliendelea kusema, "Jambo ambalo watu hawaelewi ni Zanzibar haina utaifa huwezi kwenda nje ya nchi ukakuta kuna Balozi wa Zanzibar kwani Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano."
Katika mkutano uliofanyika Zanzibar hivi karibuni, Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, alisema chama chake hakiko tayari kujadili mfumo wa Muungano wa serikali mbili kama unavyotetewa na CCM.
Makamu wa Pili wa Rais alisema kazi iliyopo mbele ni kwa Bunge kukaa kama kamati na kujadili kwa kina rasimu na kuweza kubadilisha, kuboresha, kuongoza au kupunguza jambo lolote ambalo wajumbe wataona iko haja ya kufanya hivyo.
Hata hivyo alisema kumekuwepo changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa uvumilivu miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu.
Alisema limekuwa Bunge linalotawaliwa na hisia zaidi badala ya kuweka maslahi ya taifa mbele.
Alisema viko vikundi vya wachache wasiotaka mchakato huo kuendelea kutokana na utashi wao wa kisiasa.
Alisema uvunjifu wa amani umefanya Bunge kushindwa kutekeleza kazi zake kama kawaida hali ambayo haiwezi kustahimilika. Alitaka viongozi kuwa mfano mwema wa matendo mazuri mbele ya jamii ya Watanzania.
"Vitendo vya uvunjifu wa amani kila siku ili Bunge liahirishwe kwa sababu tu za kibinafsi za baadhi ya wanasiasa sio jambo jema hasa kwa kuwa kodi za wananchi zinapotea bila kufanya kazi tuliyokusudia kuifanya," alisema.
Alisema katika mchakato huo wameshuhudia baadhi ya wanasiasa wakionesha nia zao za kutaka kuvunja Muungano kutokana na kauli zao zenye kuchonganisha wananchi wa pande mbili za Muungano.
Alisema makundi yasiyo rasmi yaliyoundwa ndani ya Bunge ambayo ni Uwaka na Tanzania Kwanza ni kwa utashi wa kisiasa.
Alishutumu Ukawa kwamba lina nia ya kuweka misuguano na kujaribu kuleta vurugu ndani ya Bunge.