Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4580

MWILI WA ALIYEKUWA MKUU WA MKOA WA MARA KUAGWA LEO...

$
0
0
Askari wa FFU wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa John Tupa tayari kwa kusafirishwa.
Mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Tupa unaagwa leo katika ibada itakayofanyika viwanja vya Nyerere Square, mjini Dodoma.

Taarifa ya Kamati ya Uratibu ya Msiba ya Mkoa wa Dodoma, ilisema baada ya ibada hiyo wananchi watapata nafasi ya kumuaga.
Mkuu huyo wa mkoa alifariki dunia ghafla Jumanne wiki hii akiwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, akipokea taarifa tayari kwa ajili ya kufunga mafunzo ya mgambo katika kijiji cha Nyamwaga.
"Shughuli nzima itaanza saa tatu kamili asubuhi na kukamilika saa nane kamili mchana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Kesho ndiyo safari ya kwenda Kilosa, Morogoro kwa ajili ya maziko ya mkuu huyo wa mkoa aliyefariki ghafla.
Mwili wake uliwasili mjini Dodoma jana jioni kwa ndege ukitokea mkoani Mara kupitia Mwanza.
Ulipokewa na viongozi na wananchi na kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Katika hatua nyingine, Spika wa Bunge,  Anne Makinda  amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu  Mizengo Pinda  kutokana na kifo hicho cha mkuu wa mkoa.
“Kwa niaba ya wabunge wote, napenda kutoa salamu za  rambirambi kwako, familia ya marehemu na wananchi wote wa Mkoa wa Mara kutokana na msiba huu mkubwa,” alisema Makinda.
Katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa, Makinda alisema Tupa atakumbukwa kama kiongozi shupavu, mwadilifu na mchapa kazi katika nyadhifa mbalimbali alizowahi kuzitumikia wakati wote wa uhai wake.
Mbunge wa  Tarime, Nyambari Nyangwine alimwelezea Tupa, kuwa mzalendo na kiongozi aliyejituma katika kazi zake.
“Mkoa wa Mara tumepoteza kiongozi  makini, mwadilifu, muwazi na asiyependa makuu,” alisema Nyangwine na kuongeza kwamba katika miaka mitatu aliyofanya kazi mkoani humo, ametatua matatizo na migogoro mingi vijijini.
Kwa mujibu wa mbunge huyo, baadhi ya migogoro ilikuwa imeshindikana. Pia alisimamia kwa makini, kukomesha uhalifu katika maeneo mbalimbali ikiwemo wilaya ya Tarime.
Tupa alizaliwa Januari mosi,  1950. Amewahi kuongoza Wilaya za  Chunya, Mwanga, Bukoba, Muleba na Dodoma kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara mwaka 2011. Ameacha mjane na watoto watano.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4580

Trending Articles