Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4593

NDESAMBURO ATILIA SHAKA MALALAMIKO YA CHADEMA KUIBIWA KURA...

$
0
0
Philemon Ndesamburo.
Mmoja wa wafadhili wa Chadema, Philemon Ndesamburo, ametilia shaka madai ya muda mrefu ya chama hicho kuibiwa kura kwenye uchaguzi.
Ndesamburo,  ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Mjini na Mwenyekiti wa  Chadema wa Mkoa wa Kilimanjaro, alielezea shaka yake hiyo jana wakati akifungua kikao cha siku mbili cha vijana wa chama hicho mjini hapa.
“Tuache kulalamika kila mara kwamba kura zimeibwa, huo wizi unafanyika wakati gani, kama upo kwa nini na sisi tusiibe?” Alihoji kiongozi huyo anayeheshimika ndani ya Chadema.
Kauli hiyo ya Ndesamburo inapingana na kauli iliyozoeleka ya viongozi wa Chadema kwamba katika uchaguzi mkuu uliopita, kura za mgombea urais wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa, ziliibwa.
Mbali na uchaguzi mkuu uliopita, pia katika uchaguzi mdogo katika maeneo mbalimbali nchini, Chadema iliposhindwa, imekuwa ikilalamika kura za wagombea wake kuibwa na wakati mwingine kuhamasisha vijana kufanya vurugu kulinda kura zisiibwe.
Bila kutaja idadi ya wanachama wa Chadema kwa sasa, Ndesamburo aliazima mbinu ya CCM aliposema, ili Chadema iunde Serikali baada ya uchaguzi wa mwaka 2015, inahitaji idadi ya wanachama milioni 10 nchini, na wote kwa pamoja wakipiga kura watakiwezesha chama hicho kushinda uchaguzi mkuu wa 2015.
“Mimi nina imani kwamba tunaweza kuunda Serikali  mwaka 2015 kama tutajipanga vema, naomba mkaimarishe chama tupate wanachama milioni 10 … wapiga kura nchini kote hawazidi hapo, mfano hai ni uchaguzi mkuu uliopita,” alisema.
Kauli hiyo haitofautiani na ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za mwaka 2010, ambapo aliwaambia wanachama wa CCM waliokuwa zaidi ya milioni tano mwaka huo, kwamba kama kila mmoja akimshawishi rafiki yake mmoja aipigie kura CCM, watakuwa wameshashinda uchaguzi.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema huu ni wakati wa Chadema kujiimarisha na kutaka vijana wasijitumbukize katika malumbano yanayoonekana sasa, kwani chama   hakina nia ya kumjenga mtu mmoja mmoja bali maslahi ya chama yatangulie.
“Hapa mtakutana kwa siku mbili, mtaelimisha masuala na mbinu sahihi za kujenga chama kuanzia ngazi ya tawi hadi Taifa, asije mtu akawaeleza mjiunge na kundi lolote la wanaotaka kujipatia umaarufu, akianza kueleza hivyo mtoeni nje ya kikao,” alisema.
Katika hatua nyingine, aliyekuwa Katibu wa Sekretarieti na Mwenyekiti  wa  Chadema, Lindi,  Ally Chitanga amesema kadri viongozi wa chama hicho wanavyozidi kudai kutomtambua, atazidi kutoa siri nyingi juu ya chama hicho.
Chitanga amesema amekitumikia chama hicho kwa miaka 10, katika nafasi za ndani hivyo anajua maovu mengi ya viongozi na kwamba ataweka wazi mambo yote wakiendelea kumchokonoa.
Aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na gazeti hili, akidai kushangazwa na kauli za Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Slaa kwamba hawezi kuzungumzia chochote kuhusu kujiuzulu kwake kwa kuwa (Chitanga) ni mtu mdogo sana ndani ya chama.
"Nimeshangazwa na kauli hii, anasema mimi ni mtu mdogo, ni sawa, lakini ninachotaka wana Chadema na Watanzania wafahamu juu ya ulevi wa madaraka na ukubwa vinavyomtafuna Dk Slaa, kama mimi Mwenyekiti wa Mkoa na Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa na Katibu wa Sekretarieti ni mtu mdogo na hawezi kunizungumzia, hao wanachama wa kawaida atawaitaje!" alihoji Chitanga kwa mshangao.
Alisema ulevi wa madaraka wa Dk Slaa aliouonesha pia kwa David Kafulila alipoamua kuhama Chadema na kujiunga NCCR-Mageuzi.  "Dk Slaa alitoa kauli kama hii akimwita kuwa ni nyenyere, lakini mwisho wa siku tulipoteza majimbo yote ambayo uwezo wa kushinda uliokuwapo katika uchaguzi mkuu wa 2010 Kigoma," aliongeza.
Alisema amefanya kazi na Dk Slaa ofisi moja makao makuu ya chama na hata Septemba alifuatana naye katika ziara ya Pemba kusikiliza maoni ya Katiba akiwa msaidizi wake, hivyo haoni kama ni sahihi kumwita mtu mdogo.
Alisema anauthibitishia umma wa Tanzania kuwa Mungu aliwanusuru sana katika uchaguzi mkuu wa 2010 maana kwa upande wao, waliokuwa wakifanya kazi karibu na viongozi hao wameshuhudia vitu vingi vya Dk Slaa ukiwamo ubinafsi na tamaa.
Aidha, alisema hoja iliyotolewa na Msemaji wa Chama hicho, Tumaini Makene, ya kumtaka aoneshe barua ya uteuzi wa kuwa Katibu wa Sekretarieti, haina mantiki bali ni udhaifu wa utendaji kazi wa Dk Slaa, kwa kuwa alishika nafasi hiyo tangu mwaka 2010 kutokana na aliyetakiwa kufanya kazi hiyo Zitto Kabwe kuwa na majukumu mengi, hivyo kupendekeza ateuliwe na sekretarieti ikabariki.
"Nina uthibitisho wa kutosha kuitumikia nafasi hiyo, nina baadhi ya maelekezo niliyokuwa nikipewa na Dk Slaa. Zaidi ya hilo kama sikuwa na wadhifa huo, kwenye vikao vya sekretarieti nilikuwa naingia kufanya nini?" Alihoji Chitanga.
Akizungumzia ukabila na udini ndani ya chama hicho alisema, majibu yaliyotolewa na Makene hayajitoshelezi, kwani wakurugenzi watatu kati ya sita ni wenyeji wa Kilimanjaro na hakuna Mwislamu.
Alisema hana maana ya kuleta ubaguzi wa kidini au ukabila isipokuwa hiyo ni hali halisi ndani ya chama hicho huku akitolea mfano Tundu Lissu kupewa ukurugenzi wa sheria na Katiba wakati kuna watu wenye uwezo kuliko yeye, mfano Profesa Abdallah Safari.
"Lissu hamwingii hata kidogo Profesa Safari, lakini kutokana na udini na ukabila ndani ya chama hiki kitengo hiki akapewa Lissu," aliongeza.
Dk Slaa na Mwenyekiti Freeman Mbowe wana jukumu la kusimamia haki na ukweli kama kweli wana upendo na uchungu na chama hicho vinginevyo watakiua, aliongeza.
"Kila mmoja anaujua uhasama kati ya Zitto na viongozi hawa, uliokuja baada ya kuamua kugombea uenyekiti wa Chadema mwaka 2009 na uhasama huu kukua zaidi kadri siku zinaposogea kuelekea uchaguzi mkuu ndani ya chama.
Wakati huo huo, Polisi  jijini hapa inaendelea kuwahoji mlinzi, Kitumbizwi Bahati (42) mkazi wa Olasiti na Katibu Muhtasi Jenifer Mwasha (25) ambao walikuwa wafanyakazi wa ofisi ya Chadema iliyoungua moto.
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha,   Japhet Lusingu alisema Polisi inaendelea kuhoji watu hao ili kubaini ukweli wa tukio hilo.
Alisema  uchunguzi uliofanywa na Polisi kwa kushirikiana na Kikosi cha Zimamoto umebaini kuwa ofisi hizo zinalindwa na walinzi wa chama hicho ambapo siku hiyo mlinzi Bahati aliingia kazini Desemba 2 saa 12 jioni na kutoka Desemba 3 saa 12 asubuhi huku Jenifer akiingia kazini saa 1.30 asubuhi kila siku lakini siku ya tukio aliingia saa 4 asubuhi.
Pia uchunguzi umebaini kuwa hakuna mahali palipovunjwa katika uzio wa ofisi hiyo wala mlango wa nyuma wa ofisi hizo ila kwenye veranda kuligundulika tundu darini likiwa na upana na urefu wa futi moja na nusu ambalo ni dogo mtu kupenya na kuingia ndani ya ofisi hizo.
Alisema bafuni yalikutwa majivu sakafuni na juu ya sinki yakiwa bila maji maji, kuta hazikuwa zimeungua, huku eneo la dari ambalo moto ulionekana kulikuwa na dalili za kuungua kwa chini. 
Pia kipande cha chuma kilichokuwa na karatasi zilizoungua na kochi vilipatikana eneo la tukio.
Hali hiyo imesababisha utata mkubwa baada ya Kamanda Lusingu kuliambia gazeti hili, kwamba mlinzi wa ofisi hizo aliondoka lindoni bila kukabidhi.
“Kitu cha kushangaza na kutia shaka ni mlinzi kuondoka saa 12 kabla ya kukabidhi lindo kwa mhudumu wa ofisi hizo ambaye naye kwa kawaida hufika saa 1.30 asubuhi inashangaza kidogo,” alisema Kamanda Lusingu.
Utata mwingine ni Jenifer kuchelewa kufika ofisini hapo kama anavyopaswa kufika mapema saa 1.30 asubuhi ambapo kwa siku hiyo alifika saa 4 asubuhi muda ambao ni tofauti na kawaida yake.
Pia utata mwingine unatokana na madai kuwa tukio hilo lilisababishwa na hitilafu ya umeme akisema si kweli kwa kuwa wakati tukio hilo linatokea hakukuwa na umeme kwenye ofisi hizo kutokana na LUKU siku hiyo kwisha.
Pia wawashaji wa moto huo walitumia kochi kubwa na ndoo ya ofisi hiyo kupandia juu nje ya ofisi hizo na kutoboa sehemu ya dari na kuwasha moto huo.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4593

Trending Articles