![]() |
James Hassan. |
Wakati akisikiliza kesi hiyo jana Hakimu Janeth Kinyage na Mwendesha Mashitaka wa Serikali Ester Martin, walitoa nafasi ya ushahidi kutolewa ambapo shahidi namba moja Inspekta Gabriel Chiguma alielezea jinsi alivyomkamata mshitakiwa huyo aliyekuwa amevalia nguo za kiaskari maeneo ya Kinyerezi Mnara wa Voda.
Inspekta Chiguma alisema kuwa mnamo Agosti 14, mwaka huu, akiwa amevalia mavazi ya kiaskari akielekea kazini akiwa na gari lenye namba za usajili T 576 ACP, alipofika maeneo ya Kinyerezi Mnara wa Voda alimkuta James akiwa amevalia mavazi ya kiaskari akiwa amesimama chini ya mwembe huku ameshikilia jalada hatua iliyoashiria kuwa alikuwa katika utekelezaji wa majukumu yake.
Alisema hata hivyo mavazi ndiyo yaliyofanya kugundua kuwa James hakuwa askari polisi kwani alivaa shati ambalo limedariziwa kwa vifungo vya kawaida vya nguo wakati sare za Jeshi la Polisi shati huwa na vifungo vya chuma.
Alisema mbali ya alama hiyo pia James alionekana kuwa alivaa sare zake kwa haraka baada ya kushindwa kuvaa ipasavyo mkanda wa filimbi na kusababisha mkanda huo kuning'inia.
Alisema pia kuwa maeneo ambayo James alisimama hayakuwa ya kikazi kwani hapakuwa kituo cha kusimamia askari huyo.
Mbali ya alama hizo, pia alisema alimtilia mashaka askari huyo kwani wakati wanasalimiana hakutoa heshima kuashiria kuwa anazungumza na mkuu wake na pia alipoulizwa jina lake hakutaja cheo chake na kuishia kutaja jina lake.
Alisema alipomhoji mahali anapofanyia kazi, James alisema anafanya kazi Kituo Kikuu cha Usalama Barabarani (Central), kituo ambacho yeye pia (Inspekta Chiguma) anafanyia kazi na hivyo kudhihirisha hakuwa askari kutokana na kuwajua kwa sura askari wote wa usalama barabarani wa Mkoa.
Mbali ya ushahidi huo, Inspekta Chiguma aliionesha mahakama hiyo picha za mshitakiwa huyo aliyekuwa amevalia sare hizo batili za askari wa usalama barabarani.
Hata hivyo, mshitakiwa alitoa pingamizi kuhusu picha hizo akiiambia Mahakama kwamba kupitia kifungu cha sheria za Jeshi la Polisi (SPA) Namba 289 kifungu cha kwanza iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 picha zote zilitakiwa kuwekwa katika kurasa (page).
Hata hivyo, Mwendesha Mashitaka Martin alisema hoja za mshitakiwa hazina msingi na kwamba alikuwa ameidanganya Mahakama kwani vifungu alivyovitaja havizungumzii suala alilolisema.
Aliporuhusiwa kumuuliza maswali shahidi, mshitakiwa alimhoji shahidi huyo kuwa wakati alipomkamata alimshirikisha kiongozi gani, ambapo Inspekta Chiguma alisema alimshirikisha askari kanzu Isack ambaye alikuwa naye kwenye gari hilo.
Mshitakiwa pia alimuuliza shahidi huyo endapo kama ana ushahidi kuhusiana na maelezo aliyoiambia Mahakama kwamba alikiri kufanya kitendo hicho kutokana na ugumu wa maisha, swali ambalo shahidi alisema ni tukio lililotokea wakiwa katika mazungumzo ndani ya gari. Kesi hiyo itasikilizwa tena Desemba 10 mwaka huu.
Mshitakiwa alifikishwa mahakamani hapo Agosti 14, mwaka huu, kujibu mashitaka ya kujifanya askari wa kikosi cha usalama barabarani baada ya kukutwa Kinyerezi Mnara wa Voda Wilaya ya Ilala ambapo alikana mashitaka hayo.