Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4679

MWANDISHI WA HABARI MKONGWE AFARIKI DUNIA...

$
0
0
Marehemu Dunia Mzobora.
Mhariri Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani, Dunia Mzobora amefariki dunia.
Mzobora, 49, alifariki dunia ghafla jana saa 12 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikopelekwa kwa matibabu zaidi akitokea Hospitali ya Aga Khan ya Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu aitwaye Musa, Mzobora alianza kujisikia vibaya juzi usiku nyumbani kwake Tabata Mawenzi, na kupelekwa Aga Khan lakini hali ilizidi kuwa mbaya na kuhamishiwa  Muhimbili.
Alifariki dunia muda mfupi baadaye wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.
Mzobora, ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Naibu Msanifu Mkuu wa Uhuru, alifanya kazi hadi kumalizika kwa gazeti la Uhuru toleo la jana, akikaimu nafasi ya Msanifu Mkuu, akiwa na afya njema.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa ndugu wa familia zilisema maziko ya marehemu yatafanyika leo Dar es Salaam.
Mzobora, ambaye alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Shirika la Magazeti ya Chama (leo Uhuru Publications Limited) mwaka 1989 akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu,  Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.
Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa Msanifu Habari wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa Mwandishi wa Habari Daraja II   mwaka 1994.
Mwaka 1995 alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa Habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine-SAUT), Mwanza na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Uandishi wa Habari mwaka 1998.
Baada ya kurejea kazini, alipandishwa vyeo ngazi mbalimbali kuanzia Mwandishi Mwandamizi Daraja II na hadi anafariki dunia alikuwa Mhariri Daraja la II.
Miongoni mwa nyadhifa alizopata kushika ni pamoja na Kaimu Msanifu Mkuu wa Uhuru, Kaimu Mhariri wa Mzalendo na Kaimu Mhariri wa Makala.
Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006 Mzobora alijiunga tena na SAUT  kwa masomo ya Shahada ya Uzamili katika Mawasiliano ya Umma na Uandishi wa Habari.
Rais Jakaya Kikwete jana alimtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo,  Dk Fenella Mukangara, kutokana na  kifo cha  Mzobora. 
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa waandishi wa habari shupavu na mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU, kilichosababishwa na ugonjwa wa shinikizo la damu baada ya kuwa amepelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupatiwa matibabu,” alisema kwa masikitiko Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema binafsi alimfahamu vyema Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma vilivyo katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha umma kwa kutumia vyema kalamu yake, na kwa kuzingatia kikamilifu Maadili ya Taaluma yake ya Uandishi wa Habari.
“Kutokana na taarifa za kifo cha Dunia Mzobora, ninakutumia wewe Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Mheshimiwa Dk. Fenella Mukangara na Wafanyakazi wote wa Kampuni ya Magazeti ya Chama ya Uhuru na Mzalendo na kwa kweli waandishi wote  wa habari nchini, salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa waandishi  ambaye amelitumikia vyema Taifa lake kupitia tasnia ya habari,” alisema.
“Aidha kupitia kwako, naomba unifikishie salamu zangu za rambirambi na pole nyingi kwa familia ya marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza baba, kiongozi na mhimili wa familia,”alisema.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4679

Latest Images

Trending Articles