Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

KAMATI NANE ZA BUNGE KWENDA MAFUNZONI NG'AMBO...

$
0
0
Kikao cha Bunge mjini Dodoma.
Kamati nane za Bunge zinatarajiwa kwenda nje ya nchi kwa ziara za kikazi na mafunzo, huku zingine nane zikiendelea na shughuli mbalimbali nchini ikiwamo kutembelea miradi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Deogratius Egidio, alisema Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala iko Nairobi, Kenya na baadaye itakwenda Ghana kwa  mafunzo.
Alisema kamati zingine zinazokwenda nje ya nchi ni pamoja na ya Maendeleo ya Jamii ambayo iko Malaysia kwa mafunzo ya hifadhi ya jamii, na itarejea nchini Novemba 26 na kuendelea na shughuli zingine za kawaida.
“Pia Kamati ya Miundombinu itaondoka kwenda Malaysia Novemba 22 (kesho), ambako itajifunza masuala ya maendeleo ya miundombinu,” alisema Egidio.
Alisema Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa pamoja na kuwa na ziara ya Uingereza na Ireland kujifunza masuala ya serikali za mitaa, itakuwa na ziara Mtwara kutembelea miradi ya halmashauri mbalimbali.
Alisema pamoja na Kamati hiyo, ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC)   iko Dubai kwenye mkutano wa kamati zinazosimamia serikali na baadaye nayo itakwenda Uingereza.
Aidha, alisema Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo ilianza shughuli zake juzi nayo inatarajiwa kwenda India kupata mafunzo kuhusu huduma za jamii huku Kamati ya Ukimwi ikienda Afrika Kusini.
Kamati ya Katiba, Utawala na Sheria Mwenyekiti wake ni Pindi Chana na Makamu ni William Ngeleja ambayo ina wajumbe takribani 17.
Kamati ya Maendeleo ya Jamii inaongozwa na Jenister Mhagama na Makamu Said Mtanda ina wajumbe 21, wakati Kamati ya Miundombinu chini ya Peter Serukamba, ina wajumbe 20.
Aidha, LAAC chini ya Rajaab Mbarouk Mohamed ina wajumbe 18, wakati ya Huduma za Jamii ya Margareth Sitta ina wajumbe 21.
Kamati ya PAC chini ya Zitto Kabwe ina wajumbe 18 huku ya Ukimwi inayoongozwa na Lediana Mng’ong’o ikiwa na wajumbe 22.
Kamati ya Uchumi, Viwanda na Biashara ambayo inaongozwa na Mahamoud Mgimwa yenye wajumbe 22 inakwenda nje wakati wowote kwa mafunzo lakini ratiba yake haijakamilika.
Egidio pia alisema kamati zingine ikiwamo ya Bajeti, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Ulinzi na Usalama na Kilimo, Mifugo na Maji, zitaendelea na shughuli zao Dar es Salaam.
Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira iko katika programu maalumu ya kushughulikia sakata la mgogoro wa Operesheni Tokomeza.Shughuli za kamati zilianza rasmi juzi na zinatarajiwa kukamilika Novemba 29 ambapo mkutano wa 13 wa Bunge unatarajiwa kuanza rasmi Desemba 3.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

Trending Articles