![]() |
Kamanda Marietha Minangi. |
Tukio hilo lilitoka nje ya lango la nyumba yao Amana, Ilala karibu na Hoteli ya MM na baa maarufu kama Klabu ya Wazee.
Munisi ambaye ni mkazi na mfanyabiashara wa magari Mwanza alifanya tukio hilo jana asubuhi wakati wanafamilia hao wakitoka nje ya lango la nyumba yao.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Noel Gerald alidai kuwa Munisi alifika nje ya nyumba hiyo mapema asubuhi akiwa kwenye teksi na kusimama kama mtu anayesubiri kitu.
Alisema ghafla geti la nyumba hiyo lilifunguliwa na gari aina ya Toyota Surf lilitoka lakini kabla halijafika mbali Munisi alilisimamisha na kuwaamuru wafungue vioo vya gari.
Lakini kabla hawajafungua vioo, Munisi alipiga risasi na vioo kuvunjika kisha akapiga risasi na kujeruhi watu waliokuwa wamekaa viti vya mbele.
Alisema kisha alielekea kwa waliokaa viti vya nyuma na kuwamiminia risasi mfululizo ambapo mama wa makamo alishuka na kukimbilia uvunguni mwa gari huku akiomba msaada kwa watu waliokuwa wakipita maeneo hayo.
Gerald alisema baadaye alimfyatulia risasi mdogo wa Christina ambaye alikuwa akifunga lango na kumwua papo hapo.
Alisema baada ya kuona damu nyingi zimetapakaa katika maeneo hayo naye alijipiga risasi kichwani na kudondoka na kukata roho papo hapo.
"Mwuaji huyo alifyatua risasi zaidi ya nane na kujeruhi watu na kisha kujiua, yaani watu katika maeneo hayo hasa waliokuwa wakinywa supu Klabu ya Wazee walikimbia ovyo," alisimulia.
Ilidaiwa kuwa waliojeruhiwa katika tukio hilo ni aliyekuwa dereva wa gari hilo, Francis Nshumila, Christina Alfred ambaye alikuwa mpenzi wa Munisi na mama mzazi wa Christina, Hellen Elieza.
Nshumila alijeruhiwa kifuani huku mama yake Christina akijeruhiwa begani na hali zao si nzuri wakiwa wamelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Christina ambaye alijeruhiwa mkononi na mguuni alitibiwa katika Hospitali ya Amana na kuruhusiwa huku mdogo wake Alfa Alfred ambaye ni mfanyakazi wa benki ya Barclays, Dar es Salaam, akifariki dunia kabla ya kufikishwa hospitalini.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana eneo la tukio, Munisi alifika eneo hilo akiwa na magazini mbili za bastola zilizojaa risasi na wanafamilia hao walikuwa wakimsindikiza Christina kwenda uwanja wa ndege ambako alikuwa akisafiri kwenda kisiwa cha Cyprus.
Ilielezwa kuwa Munisi na Christina walikuwa wachumba wa muda mrefu wakati Munisi akiishi Mwanza Christina Dar es Salaam na kufanya kazi katika benki ya Barclays.
Hivyo kwa wiki Munisi alionekana akizunguka karibu na nyumba hiyo kama anayechunguza kitu na inadaiwa kuwa wiki hii Christina alimweleza kuwa angesafiri kwenda Kilimanjaro.
Ilidaiwa kwamba baada ya kufuatilia Munisi aligundua kwamba hajasafiri na badala yake yuko kwa mama yake, ambapo alimpigia simu mama mkwe huyo kumweleza taarifa za mpenzi wake, lakini alionekana kumtetea mtoto wake.
Ilielezwa kuwa Munisi alibaini kuwa jana Christina alitarajia kwenda Cyprus na mpenzi mwingine raia wa Kenya ambaye inadaiwa alikuwa pia ndani ya gari hilo na katika tukio la jana alijeruhiwa.
"Inaonekana Munisi alikuwa na mtu aliyekuwa akimpa taarifa za uhakika kuhusu nyendo za mchumba wake, hivyo kumvizia getini na kufanya ukatili huo uliosababisha kuua mdogo wake ambaye hakuwa na hatia yoyote," kilisema chanzo cha habari hii.
Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, alionekana akiingia katika Hospitali ya Amana kwa gari namba T 176 BCA kwa ajili ya upelelezi.
Akizungumza akiwa Amana walikopokewa majeruhi na maiti, Mkuu wa Kitengo cha Dharura katika hospitali hiyo, Dk Christopher Mzava, alikiri kupokea majeruhi watatu; wanawake wawili na mwanamume.
Alisema mwanamke anatibiwa kwenye hospitali hiyo huku wengine wawili wakikimbizwa katika Hospitali ya Muhimbili huku wakipokea maiti za wanaume wawili.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema Munisi na Christina walikuwa na uhusiano ya kimapenzi na kitendo hicho kilifanyika wakati wanafamilia hao wakielekea kazini saa moja asubuhi.
Kamanda Minangi alipoulizwa kuhusu uhusiano wa dereva wa gari hilo na familia hiyo, alisema bado wanaendelea na upelelezi kubaini uhusiano wao.