Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

MADUKA MTAA WA SAMORA YABOMOLEWA HUKU BIDHAA ZIKIWA NDANI...

$
0
0
Mtaa wa Samora, Dar es Salaam.
Nyumba zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam zinazomilikiwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambazo pia zilikuwa na maduka mbalimbali zimebomolewa chini ya ulinzi wa Jeshi la Polisi baada ya kutolewa notisi ya siku tatu kwa wapangaji wake.

Ubomoaji huo ulifanyika jana kuanzia saa 12.30 asubuhi na kampuni ya udalali ya Forsters Auctioneers huku baadhi ya wafanyabiashara wa eneo hilo wakiwa hawajamaliza kuondoa vitu vyao katika baadhi ya maduka.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walilalamikia hatua hiyo kwamba imefanywa kwa ghafla na kusababisha upotevu wa mali zao, na pia kuwapa usumbufu mkubwa kwa sababu hawakupata  muda wa kutosha wa kujiandaa.
"Shirika hili halikutufanyia haki kabisa, haiwezekani itolewe notisi ya siku tatu wapangaji tuwe tumeondoa vitu vyetu, hii sio haki kabisa, ni nani ataingia gharama ya upotevu huu wa mali?" alihoji mfanyabiashara mmoja mwenye asili ya kiasia ambaye hakutaka kutaja jina lake.
Mfanyabiashara mwingine, Ally Mbeshi alisema kuwa pamoja na ubomoaji huo kuwa wa ghafla, alipongeza uamuzi huo kwa sababu nyumba hizo zilikuwa zimechakaa sana na pia zilikuwa zikichukua watu wachache tofauti na yatakapojengwa majengo makubwa na mapya.
Hata hivyo alisema baada ya kampuni hiyo iliyopewa kazi ya kubomoa kutoa tangazo kuwa nyumba hizo zingevunjwa, watu hawakuamini kama kweli hatua hiyo ingetekelezwa na ndiyo maana hawakutoa vitu vyao vyote kama walivyopewa maelekezo.
Mmiliki wa Elgon Training Institution, Yvonne Aloyce, shule ambayo ilikuwa katika moja ya majengo hayo alilalamikia notisi hiyo kutolewa siku chache na kisha nyumba kuvunjwa katika siku za sikukuu.
Alisema yeye alipigiwa simu juzi kuwa duka lake lilivunjwa na vitu kuibwa na vijana wasiofahamika.
"Baada ya kupigiwa simu nilikuja hapa nikakuta mlango umevunjwa na kompyuta sita zimeibwa, wafanyabiashara tulienda polisi lakini tuliambiwa tu tufungue kesi ya wizi na tuweke ulinzi kwa sababu dalali huyo haruhusiwi kuvunja kwa sababu kesi iko mahakamani, lakini nashangaa leo amekuja kuvunja, hatukuwa tumejiandaa kabisa," alisema Aloyce.
Chini ya usimamizi wa askari,  ubomoaji wa nyumba hizo katika mtaa maarufu wa Samora katikati ya jiji uliendelea huku vijana wakipata neema ya kuokota vitu mbalimbali kutoka katika maduka hayo kwa ajili ya kuuza na kujipatia kipato.
Mwandishi alishuhudia vijana wengi wa mtaani wakijishughulisha wakati uvunjaji ukiendelea kwa kujipatia vifaa mbalimbali vya ujenzi, ikiwa ni pamoja na milango iliyotoka katika majengo hayo, madirisha, nondo, mbao, viyoyozi, feni pamoja na mali nyingine.
Mwandishi aliondoka eneo hilo wakati kazi ya ubomoaji ilikuwa bado inaendelea bila vurugu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

Trending Articles