Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

LWAKATARE WA CHADEMA BADO ASHIKILIWA NA POLISI...

$
0
0
Advera Senso.
Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare bado anashikiliwa na Polisi.
Hadi jana saa 10 jioni, wakili wa mtuhumiwa huyo, Nyaronyo Kicheere alisema  mteja wake bado alikuwa kwenye Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam.
Alipoulizwa kama mteja wake anatendewa haki na maofisa hao wa Polisi, Kicheere alisema, "Polisi wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, wanamshikilia na kumhoji kwa mujibu wa sheria...hakuna tatizo,  tunasubiri uamuzi utakaofikiwa hata kama ni kwenda mahakamani,  tuko tayari kwenda."
Kicheere alisema jana  polisi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) na maofisa kutoka ofisi ya Mwendesha Mashitaka  Mkuu wa Serikali  (DPP) walikuwa na kikao makao makuu ya Polisi huku mteja wake akisubiri uamuzi wa kikao hicho.
"Watakapomaliza kikao watatwambia hatua gani inafuata; lakini kwa sasa bado mteja wangu anashikiliwa hapa Kituo Kikuu cha Polisi nami niko naye hapa," alisema wakili huyo.
Lwakatare alikamatwa juzi akituhumiwa kupanga mikakati ya kuteka na kutesa baadhi ya watu wakiwamo waandishi wa habari nchini. Miongoni mwa watu ambao tayari wamevamiwa na kutekwa ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda ambaye amelazwa Afrika Kusini akipata matibabu baada ya kuvamiwa na kuumizwa na watu wasiojulikana.
Lakini pia Lwakatare kwa mujibu wa video iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, anadaiwa kupanga mikakati ya kuteka Mhariri wa gazeti la Mwananchi tukio ambalo halijatokea. Hata hivyo, gazeti la Mwananchi jana lilimtaja Mhariri Mtendaji wake, Dennis Msaky.
Msemaji wa Polisi Advera Senso alinukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa kigogo huyo wa Chadema anashikiliwa kutokana na picha hiyo iliyoko kwenye mtandao.
Katika picha hiyo inayodaiwa kuwa ya Lwakatare, anaonekana akitoa maelekezo kwa mtu ambaye haonekani, namna ya kumfuatilia mwandishi wa Mwananchi anayedaiwa kuwa karibu na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe na ikiwezekana amdhuru kwa vile anashiriki kuihujumu Chadema.
Hata hivyo, kwenye picha hiyo ya video  mtu huyo anayedaiwa ni Lwakatare amejikita kutoa maelezo ya kufuatilia mwandishi huyo wa Mwananchi kama ana gari na mtu ambaye anapenda kuwa naye kwenye gari wakati anatoka kazini na hakuna sehemu anayotajwa Kibanda.
Lakini pia picha hiyo inaonekana kumwelekeza mtu kuwa atafute dawa za usingizi kwa ajili ya kumpa mwandishi huyo na atakapokuwa anazinduka, ajikute yuko sehemu ambayo haitambui, lakini sauti ya video hiyo inaelekeza kusiwepo tukio la mauaji.
Polisi licha ya kumshikilia Lwakatare, tayari wamepekua nyumbani kwake na Kicheere alikiri kuwa polisi bado wanafanya mahojiano ya kina na mteja wake huyo.
Jana hakuna  ofisa wa ngazi ya juu wa Polisi aliyepatikana kuzungumzia suala hilo, si Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wala Senso. 
Gazeti moja jana lilimnukuu Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akielezea tukio hilo kuwa linadhihirisha kuwapo njama chafu zenye lengo la kukichafua chama hicho mbele ya jamii.
Dk Slaa alidai njama hizo zinaratibiwa na kigogo aliye ndani ya Serikali ambaye analitumia Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Dola kuidhoofisha Chadema. "Ikiwa kweli anashikiliwa kutokana na video hiyo, ni furaha kwetu, kwa sababu ukombozi wa nchi umekaribia," Dk Slaa alinukuliwa na gazeti hilo akitamba.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4503

Trending Articles