![]() |
Shekhe Ponda Issa Ponda. |
Polisi Zanzibar inamsaka Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Ponda Issa Ponda, kwa tuhuma za kuendesha mihadhara ya kidini katika misikiti kisiwani hapa, yenye kuashiria uvunjifu wa amani.
Ponda anatafutwa kwa tuhuma hizo, wakati akiwa katika kifungo cha nje cha miezi 12, alichohukumiwa Mei 10, katika kesi iliyokuwa ikimkabili ya kula njama, wizi wa mali yenye thamani ya Sh milioni 59.6, uchochezi na kuingia kwa jinai katika ardhi inayomilikiwa na kampuni ya Agritanza Limited kwa nia ya kujimilikisha isivyo halali.
Katika kesi hiyo, Mahakama ilimkuta Shekhe Ponda na hatia katika kosa la kuingia kwa nguvu eneo hilo la ardhi isiyo yake, na kumhukumu kifungo hicho cha nje, lakini kwa masharti ya kutofanya kosa lolote katika miezi hiyo.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Victoria Nongwa, katika hukumu hiyo alisema ametoa hukumu hiyo, kwa kuwa Shekhe Ponda hana rekodi ya makosa ya jinai na kwamba alikaa rumande kwa muda mrefu (miezi 7), baada ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuzuia dhamana yake, hivyo ni haki kuangalia muda huo.
“Hivyo Mahakama chini ya kifungu cha 25 (g) cha kanuni za adhabu, mshitakiwa unaachiwa kwa masharti ya kutotenda kosa kwa miezi 12. Unatakiwa ulinde amani na kuwa na tabia njema katika jamii. Ukishindwa hiyo, utarudi hapa kwa adhabu nyingine inayokufaa,” alisema Hakimu Nongwa.
Pamoja na kuwa chini ya kifungo hicho, Kamishna Mkuu wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alidai kuwapo taarifa za Shekhe Ponda kuendesha mihadhara ya uchochezi.
“Tumepata taarifa za kuwapo kwa Shekhe Ponda katika kisiwa cha Unguja, akitoa mihadhara yake mbalimbali...sisi tunamtafuta kwa mahojiano zaidi,” alisema Kamanda Mussa.
Alisema kabla ya kuingia kwa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, alihadharisha na kutaka viongozi wa dini kuacha kutoa kauli na mihadhara yenye mwelekeo wa uchochezi.
Awali kabla ya kauli hiyo ya Polisi, CCM Zanzibar, iliitisha mkutano na waandishi wa habari na kutaka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Shekhe Ponda, kutokana na kauli zake zenye uchochezi na kutaka kugawa Wazanzibari.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu, alitoa madai hayo katika ofisi ndogo za CCM, Kisiwandui na kuongeza kuwa, Shekhe Ponda amekuwa akitoa mihadhara ya kidini katika nyakati tofauti Unguja, yenye mwelekeo wa kujenga chuki na uhasama kwa wananchi.
Kwa mujibu wa madai ya Waride, katika mihadhara hiyo Nungwi katika mkoa wa Kaskazini Unguja na kwenye Msikiti wa Kwarara, Ponda amekuwa akihamasisha Wazanzibari kuandamana ili kuishinikiza Serikali kuachia huru mashekhe sita wa Jumuiya ya Uamsho.
Huku akionesha kanda tatu zenye hotuba ya mihadhara ya Katibu huyo wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Waride alisema Shekhe Ponda anataka Wazanzibari waandamane kama wanavyofanya wananchi wa Misri kudai haki zao.
“Tunao ushahidi wa kutosha, kwamba Shekhe Ponda yupo Zanzibar akiendesha mihadhara katika misikiti vijijini, akihamasisha Waislamu kuandamana kuiga kinachofanyika Misri,” alidai Waride akionesha kanda hizo.
Waride alidai pia kuwa miongoni mwa kauli za Shekhe Ponda katika mahubiri hayo, alitaka wananchi kuacha kuunga mkono CCM, kwa madai kwamba atakayefanya hivyo, hawezi kupata radhi ya Mwenyezi Mungu.
“Hizo ni baadhi ya sehemu za kauli zake ambazo zingine huwezi kuzitamka hadharani, lakini ukisikiliza, zinaashiria chuki kati ya wananchi na viongozi walio madarakani...kauli hizi ndizo chanzo cha vurugu na fujo, kama ilivyokuwa kwa upande wa Uamsho,” alisema.