![]() |
Mitungi ya gesi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. |
Mitungi ya gesi ya kupikia kutoka kwenye kampuni zinazotambulika inadaiwa kuhujumiwa na baadhi ya watu kwa kuifungua na kupunguza malighafi hiyo kisha kuifunga kienyeji.
Watumiaji wa gesi wamehadharishwa juu ya hilo ikielezwa baadhi wamejikuta wakinunua gesi pungufu huku mitungi husika ikifungwa bila kuzingatia utaalamu jambo ambalo limetajwa kuwa ni hatari.
Kampuni ya gesi ya ORYX imekiri kuwepo hujuma hiyo hususan kwa mitungi yake na kusema kwa kushirikiana na vyombo vya Dola na Wakala wa Vipimo, wamekamata watu 15 katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Arusha wakituhumiwa kufanya vitendo hivyo.
Meneja Masoko wa Kampuni ya ORYX, Maulid Mahfudh, alisema wateja wamekuwa wakijikuta wakinunua gesi pungufu kutokana na watu hao wasio waaminifu kuipunguza na kuweka kwenye mitungi mingine.
“Jambo hilo hatari kwani linaweza kusababisha milipuko kutokana na gesi kuvuja kwani baadhi ya waliokamatwa walibainika kutumia vifaa vya kichina ambavyo havina ubora,” alisema Mahfudh.
Kwa mujibu wa Mahfudh, watu hao ambao walikamatwa walikuwa na sehemu yenye vifaa hafifu wakipunguza gesi huku wengine wakidiriki pia kubadilisha rangi za mitungi.
Alisema wanaofanya hivyo hawana vyombo vya usalama wala wataalamu jambo ambalo ni hatari kwani inaweza kusababisha madhara kwa wananchi wa maeneo husika kutokana na gesi kulipuka.
Inadaiwa kumekuwepo malalamiko kutoka kwa watumiaji wa gesi wakidai mitungi kuvuja na mingine ikidaiwa kuisha muda wa kutumika.
Kampuni hiyo ya gesi inasema idadi ya watumiaji wa gesi imeongezeka kutoka 300 mwaka 2006 hadi watu 3,000 mwaka huu.