Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

MAGUFULI AWASHITAKI KWA RAIS KIKWETE WANAOKATAA FIDIA...

$
0
0
Dk John Magufuli.
Serikali imeonya kuwa haitaruhusu watu wachache wakwamishe juhudi za Serikali za kuunganisha nchi na mtandao wa barabara za lami.

Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo jana katika eneo la Omugakorongo Kata ya Ndama, wilayani Karagwe, wakati akiweka jiwe la msingi katika barabara ya Kyaka –Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Alitoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kumuomba amuunge mkono wakati wa kupambana na wananchi wanne, waliokataa kupokea fidia na kubomoa nyumba zao, ili kupisha ujenzi wa barabara hiyo.
Dk Magufuli alisema watu hao, akiwemo mzee marufu wa Wilaya ya Karagwe, Nehemia Kazimoto, wanataka fidia zaidi, la sivyo nyumba zao hazibomolewi au watakwenda mahakamani.
Alisema wananchi 400 waliokumbwa na athari za kubomolewa nyumba kupisha ujenzi wa barabra hiyo, wamelipwa fidia Sh bilioni 2.8 kwa mujibu wa sheria, isipokuwa wananchi wanne tu akiwemo Kazimoto, ambao wamegoma kupokea fidia.
“Hata wakienda mahakamani, sisi hatutaingilia Mahakama, bali barabara itaendelea kujengwa ikipitia katika maeneo yaliyoainishwa,” alisema Dk Magufuli.
Akitoa mfano wa mzee huyo aliyewahi kuwa kiongozi katika vyama vya wafanyakazi nchini, Dk Magufuli alisema amegoma kupokea fidia yake ya Sh milioni 101, ambazo zilitolewa na Serikali huku akidai kuwa hazitoshi na wala hatokubali nyumba yake ibomolewe kupisha barabara.
Akijibu maombi hayo, Rais Kikwete alimtaka Waziri Magufuli aendelee na kasi ya kutekeleza mipango yake ya ujenzi wa barabara ya Kyaka Bugene, ili ikamilike kwa wakati, ingawa kuna changamoto zinazokabili mradi huo kutoka kwa baadhi ya wananchi ambao si wapenda maendeleo.
“Hatutaruhusu watu wachache wazime na kukwamisha maendeleo ya Watanzania walio wengi, Waziri nimekusikia, endelea na mipango na kazi yako ya kujenga barabara hii, ili Wanakagera na Watanzania, waendelee kunufaika na matunda ya Serikali…tena hii ni ahadi yangu niliyoitoa wakati naomba kura mwaka 2005, pia ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2010,”alisema Rais Kikwete.
Alisema lengo la ujenzi wa barabara hizo, ni kuhakikisha nchi  inaunganishwa kwa mtandao wa lami, kwani siku za nyuma wananchi wa Mkoa wa Kagera waliteseka kwa kusafiri umbali mrefu, kwenda Dar es Salaam.
Wakati huo wananchi hao walilazimika kupita Uganda na Kenya kwa siku tatu mpaka tano ili kufika Dar es Salaam, lakini sasa wanauwezo wa kusafiri kwa siku moja tu kutokana na barabara kutengenezwa na kupitika kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, anatarajia ifikapo 2015 kilometa 18,000 za mtandao wa barabara wa Tanzania nzima zitakuwa tayari na kama itashindikana, basi zitabaki kilometa zisizozidi 2,000, ambazo zitakuwa hazijakamika lakini zitakuwa zikiendelea na ujenzi kwa hatua ya mwisho.
Naye Dk Magufuli, alisema wakati wa Uhuru 1961, nchi ilikuwa na mtandao wa barabara za lami za urefu wa kilometa 1,350, lakini katika muda wa Serikali ya Awamu ya Nne tu, chini ya uongozi wa Rais Kikwete, zimejengwa kilometa 11,154 za mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami.
Akitoa historia ya ujenzi barabara ya Kyaka–Bugene, Dk Magufuli alisema mradi huo ulianza 2009 na mpaka kukamilika, katika muda wa miezi 27, utagharimu Sh bilioni 64.9.
Mradi huo kwa mujibu wa Dk Magufuli, unaendelea vizuri ingawa ulikumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya  makandarasi wasimamizi wa mwanzo, Kampuni ya Sai kutoka nchini India kwa kushirikiana na Kampuni ya Data ya Tanzania,  kufukuzwa kazi baada ya muda mfupi tangu kuanza mradi.
Alisema kuwa makandarasi hao walifukuzwa kazi, baada ya kuboronga na kushindwa kufanya kazi kama mkataba unavyoelekeza, wakati tayari walikuwa wamelipwa zaidi ya Sh bilioni moja. Kwa sasa mradi huo unasimamiwa na kikosi cha wataalamu saba kutoka Wakala wa Barabara (Tanroads) Makao Makuu.
Alionya kuwa Wizara yake haitosita kuwachukulia hatu ikiwemo kuwafukuza kazi makandarasi watakaokiuka utaratibu wa kazi, kwani Tanzania sio nchi ya watu kuja kuchota fedha.
Naye Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Makao Makuu, Alon Mfugale, alisema mradi huo wa barabara ya Kyaka –Bugene, unaojengwa na Kampuni ya China Chico kutoka nchini China, umefikia asilimia 38 ya mradi wote mpaka sasa na unagharimiwa na Serikali kwa asilimia 100.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4510

Trending Articles