![]() |
Mtoto Adam Alghoul. |
Mtoto Adam Alghoul ameanza maisha yake kwa safari ya ndege- na uraia wa nchi mbili.
Mtoto huyo amekuja duniani kwenye sakafu ya kituo cha mwisho cha kimataifa katika Uwanja wa Ndege wa O'Hare mjini Chicago Jumatano baada ya mama yake kujifungua kabla ya muda wake wakati akijiandaa kushuka kwenye ndege kutoka Abu Dhabi.
Inam Alghoul na mumewe walisafiri maili 7,200 kutoka nyumbani kwao huko Umoja wa Falme za Kiarabu baada ya mwanamke huyo kupata ruhusa kutoka kwa madaktari wawili tofauti ya kusafiri kwenda mapumzikoni katika wiki 31 za ujauzito huo.
Mtoto Adam alikuwa azaliwe Septemba 17, lakini kichanga huyo aliyekosa subira alikuwa na mipango tofauti.
"Maumivu makali mno yalianza ghafla na nikamweleza mume wangu, "Sitaki mzigo. Ita gari la wagonjwa. Sifahamu kilichotokea," alieleza Inam, akikumbukia jinsi alivyowasili uwanjani hapo O'Hare.
Chifu Brian Bell, wa Idara ya Forodha Marekani na Ulinzi wa Mipaka, alikimbilia kwenye uwanja huo wa ndege, ambako mjamzito huyo alipokuwa chumba cha wazazi. Bell naye akajitosa kwenye shughuli hiyo ya kumhudumia mwanamke huyo.
Ofisa huyo wa forodha na mwenzake mmoja wa kike walimlaza Inam chini na haraka wakaona mtoto akichomoza. Haikuchukua muda mrefu, wakamkaribisha mtoto huyo wa kiume katika dunia.
Adam na mama yake walikimbizwa kwenye Kituo cha Afya cha Presence Resurrection, ambako anatarajiwa kubaki kwa mwezi mmoja kwa ajili ya uangalizi maalumu.
Kwa mujibu wa Idara ya Forodha Marekani na Ulinzi wa Mipaka, kwakuwa mtoto huyo alizaliwa kwenye ardhi ya Marekani, sasa ni raia wa Marekani, na pia ni raia wa Abu Dhabi.
Inam si mwanamke wa kwanza kujifungulia kwenye uwanja wa ndege. Habari kama hiyo ilitokea mwaka 2011 pale abiria mjamzito alijifungua mtoto katika bafu la Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baltimore-Washington Thurgood Marshall, mjini Maryland
Madaktari wanasema ni kawaida salama kwa wanawake kusafiri hadi hatua za mwisho za ujauzito. Hatahivyo, baadhi ya mashirika ya ndege hukataa kuwabeba mama wanatarajiwa katika wiki za mwisho kabla ya kujifungua.