![]() |
Mzee Nelson Mandela. |
Wakati dunia ikisherehekea miaka 95 ya Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela jana, hali ya kiongozi huyo imezidi kutia matumaini ambapo binti yake, Zindzi Mandela, amesema anaweza kuangalia televisheni na kunyanyua mkono.
Mandela ambaye jana alitimiza miaka 15 ya ndoa yake na Graca Machel, akiwa amelazwa hospitalini kwa wiki sita sasa, lakini bintiye huyo juzi usiku wa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa baba yake, alisema shujaa huyo anaweza kuruhusiwa hivi karibuni.
"Nilimtembelea jana (Jumanne) nilikuta akiangalia televisheni huku akitumia spika za masikioni," alisema Zindzi katika mahojiano na televisheni ya Sky ya Uingereza.
"Alitoa tabasamu zuri, anaitika kwa macho na kutikisa kichwa na kuna wakati ananyanyua mkono kama mtu anayetaka kusalimia."
Alisema baba yake amekuwa akipata nguvu kadri siku zinavyokwenda na anaweza kuruhusiwa kurejea nyumbani wakati wowote hivi karibuni.
Zindzi, ambaye ni binti wa mwisho wa Mandela kwa mkewe wa pili, Winnie, alikiri kwamba kuna wakati familia ilijawa hofu kuhusu hali ya mzee huyo.
"Kuna wakati tulikuwa na hofu kubwa na tulijiandaa kwa chochote kibaya," alisema. "Lakini afya yake imeendelea kutushangaza kila siku."
Mjukuu wa Mandela, Mandla, aliyegeuka gumzo wakati akigombea mahali pa maziko ya kiongozi huyo, alielezea nguvu alizonazo babu yake hospitalini.
"Kwa hali aliyonayo babu sasa, kwamba tuko naye leo wakati watu walitabiri anguko lake, linanifanya nijisikie mwenye furaha hasa kutokana na ari yake ya kupambana, ambayo ameionesha katika maisha yake yote," alisema Mandla.
Kuhusu zawadi ya familia baada ya kutimiza miaka 95, Zindzi alisema walitarajia kumpelekea vyakula anavyopenda na zawadi nyingine, ambayo mwanzoni wengi walidhani asingeweza kuiona.
"Kwa kawaida ni vigumu kubuni zawadi mpya lakini kwa desturi huwa tunapiga picha kubwa za familia na ndugu wa karibu na familia na kumpelekea," alisema Zindzi.
Kauli ya Zindzi ya kutia matumaini ni mfululizo wa kauli za aina hiyo zilizotolewa na aliyekuwa Makamu wake na Rais wa Afrika Kusini baadaye, Thabo Mbeki, mkewe Graca na hata Rais Jacob Zuma.
Mbeki alikaririwa Jumapili na mwanzoni mwa wiki hii na vyombo vya habari akisema Mandela ataruhusiwa kutoka hospitalini hivi karibuni.
Graca Ijumaa iliyopita, aliliambia Shirika la Utangazaji la SABC, kwamba sasa hana wasiwasi kuhusu afya ya mumewe, kama alivyokuwa wiki iliyopita.
Akizungumzia afya ya Mandela mwanzoni mwa wiki iliyopita baada ya kumtembelea hospitalini mara ya pili mfululizo katika siku mbili, Rais Zuma alisema hali ya Mandela inatia matumaini.
"Tumepata matumaini, afya ya Madiba imeanza kuimarika kulingana na matibabu anayopewa, naomba umma uendelee kumwunga mkono kwa kumwonesha upendo unaompa yeye na familia nguvu," ilieleza taarifa ya Zuma.
Awali kabla ya Zuma kumtembelea, Mfalme wa Kabila la AbaThembu, analotoka Mandela, Buyelekhaya Dalindyebo, alimtembelea na kusema afya yake inaendelea vizuri na anatambua wageni.
"Hakuweza kuzungumza, lakini alinitambua na kutoa ishara chache kuonesha kwa macho kuwa alikuwa akinisikiliza," alisema Dalindyebo, ambaye ni mpwawe Mandela.
Hali ya matumaini ya afya ya Mandela, imeamsha upya mzozo wa makaburi, uliofukuta wakati afya yake ikiwa katika hali mbaya.
Wanasheria wa Mandla jana walitarajiwa kwenda mahakamani kufufua upya kesi ya kufukua makaburi ya watoto wa Mandela yaliyokuwa Mvezo na kurejeshwa walikozikwa awali, kijiji cha Qunu.
Mwanzoni mwa mwezi, Mahakama ilimwamuru Mandla, Chifu wa Mvezo alikozaliwa Mandela, aruhusu makaburi hayo yafukuliwe na mabaki ya miili hiyo yakazikwe Qunu, alikokulia Mandela.
Mzozo huo ulidaiwa kusababishwa na wosia wa Mandela kutaka azikwe karibu na walipozikwa watoto wake hao, lakini Mandla aliyahamisha miaka miwili iliyopita kutoka Qunu kwenda Mvezo.
Msemaji wa Mandla, Freddy Pilusa, alinukuliwa jana akisema: "Chifu Mandla, hana nia ya kufukua tena makaburi hayo na kuyarejesha Mvezo.
"Lakini kwa kuwa Mahakama ilitoa amri kwa kutumia taarifa za uongo na za kutengeneza, ni muhimu kupitia upya uamuzi huo ambao tunaona haukutenda haki.
Taarifa zinazodaiwa kuwa za kupika, ni madai yaliyofikishwa mahakamani na familia ya Mandela iliyokuwa ikipingana na Mandla, kwamba hali ya kiongozi huyo, ilifikia kutokujitambua ambako ni endelevu.