Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4621

KODI ZA PETROLI NA MISHAHARA ZATAKIWA KUSHUSHWA...

$
0
0
Wabunge wakiendelea na kikao mjini Dodoma.
Mjadala wa Bajeti ya Serikali ulianza jana kwa taarifa ya Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambayo imetaka baadhi ya kodi zilizopendekezwa na Serikali kuongezwa katika mafuta ya petroli, zishushwe au kubaki kama ilivyokuwa katika mwaka huu wa fedha.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo kuhusu mapendekezo ya Serikali katika Bajeti ya 2013/14 itakayoanza kutumia Julai mosi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge (CCM), alitaka pia punguzo la kodi ya mshahara (PAYE) la asilimia moja, liongezwe hadi asilimia 3.
“Serikali inapendekeza kupunguza kiwango cha chini cha kutoza kodi ya mapato (ya mshahara) kutoka asilimia 14 hadi 13, hii ni sawa na punguzo la asilimia moja.
Kamati ina maoni kuwa kiwango hiki ni sawa na ongezeko la Sh 1,900 katika mshahara wa kima cha chini kwa mwezi, ambazo ni sawa na Sh 22,800 kwa mwaka.
“Ongezeko hili ni dogo ikilinganishwa na hali halisi ya uwezo wa mfanyakazi ya kununua bidhaa na kuendesha maisha yake. Ni maoni ya Kamati kwamba punguzo lingeongezeka mpaka angalau asilimia 3, ili kuongeza uwezo wa kumudu gharama za ununuzi kwa wafanyakazi,” alisema Chenge.
Kuhusu kodi katika mafuta ya petroli na dizeli, Chenge alipendekeza kusiwepo nyongeza ya aina yoyote ya kodi katika bidhaa hizo.
Katika Bajeti ya Serikali, imependekezwa kuwa ushuru katika mafuta ya dizeli uongezwe kwa Sh 2 kwa kila lita kutoka Sh 215 inayotozwa sasa mpaka Sh 217.
Katika petroli, Serikali imekusudia kuongeza ushuru wa Sh 61 kwa kila lita, kutoka Sh 339 inayotozwa sasa kwa kila lita, mpaka Sh 400 kwa lita.
“Katika eneo hili (ushuru wa mafuta), Kamati inashauri kuwa ongezeko lifutwe. Hivyo kamati itashauriana na Serikali kuhusu vyanzo vingine vya mapato ili kufidia pengo hilo,” alisema Chenge.
Kuhusu mapendekezo ya Serikali kuongeza ushuru katika huduma zote za simu kutoka asilimia 12 ya sasa hadi asilimia 14.5 kwa mwaka ujao wa fedha, Kamati ya Bunge imeshauri mapendekezo hayo ya nyongeza ya asilimia 2.5 lifutwe.
Kwa mujibu wa Chenge, kwa kuwa Serikali itatoza ushuru katika huduma zote za simu badala muda wa maongezi tu kama ilivyo sasa, mapato kutoka ushuru wa simu yataongezeka hivyo hakuna sababu ya kuongeza kwa asilimia 2.5.
Mbunge wa Viti Maalumu, Kuruthum Mchuchuli (CUF), alipendekeza pikipiki za biashara za miguu miwili na mitatu, zisisamehewe kodi, kwa kuwa watakaofaidika sivijana wanaolengwa, bali wamiliki wa usafiri huo.
Mbunge wa Kyerwa, Eustace Katagira (CCM), alipendekeza ushuru wa magari madogo yenye umri wa zaidi ya miaka 10, usiongezwe kwa kuwa ndiyo magari yanayonunuliwa na watu wengi masikini.
Alisema msingi wa kodi ni kutoza wenye kipato kikubwa na kusaidia wenye kipato kidogo na kupendekeza wanaonunua magari mapya ndio watozwe kodi zaidi ya wanaonunua ya zamani.
Kuhusu hoja kwamba magari ya zamani yanaharibu mazingira, alisema si kweli kama inavyosemwa bali yanasaidia vijijini.
Alitoa mfano wa magari ya kazi aina ya Iveco, Mercedes Benz na Lay Land mpya kuwa si za Watanzania masikini kama Mitsubishi Fuso ambazo ni za wazawa na zinasaidia vijijini.
Kuhusu ongezeko la kodi katika utalii, Mbunge huyo alikubaliana nayo, lakini akapendekeza kodi hiyo ianze kutozwa Januari mosi mwakani badala ya Julai mosi mwaka huu, kwa kuwa watalii wa Agosti, wameshatoa malipo yao.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4621

Trending Articles