Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4621

AJIFUNGUA MTOTO NDANI YA NDEGE UMBALI WA FUTI 38,000...

$
0
0
KUSHOTO: Purukushani ndani ya ndege kabla Fatoumatta hajajifungua. JUU: Fatoumatta Kaba. CHINI: Mtoto Mamel Joella.
Msichana ambaye alijifungua mtoto wa kiume ndani ya ndege katika umbali wa futi 38,000 alikuwa ameruhusiwa kupanda humo sababu wafanyakazi wa ndege hiyo hawakuweza kuona kama alikuwa mjamzito kutokana na kujizingira nguo nyingi.
Fatoumatta Kaba, mwenye umri wa miaka 17, aliingia chumba cha kuzalia masaa manne ndani ya ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Kusini iliyokuwa ikitokea Johannesburg kwenda Uwanja wa Ndege wa John F. Kennedy mjini New York Jumamosi iliyopita na "kwa misukumo miwili' alijifungua mtoto wake wa kiume Mamel Joella kwa msaada wa daktari wa Kimarekani ambaye alikuwa mmoja wa abiria kwenye ndege hiyo.
Lakini shirika hilo la ndege lilisema wafanyakazi hawakuwa wakijua kama Fatoumatta alikuwa akitarajia kujifungua wakati walipomruhusu kupanda kwenye ndege hiyo, likiongeza kwamba sera za Shirika la Ndege la Afrika Kusini zinakataza wanawake wajawazito kusafiri kimataifa baada ya wiki 35.
"Fatoumatta alikuwa amevalia nguo kwa namna kwamba katika muonekano wa kawaida haikuwa rahisi kugundua kama alikuwa mjamzito," msemaji wa shirika hilo Tlali Tlali alieleza.
Wakati huohuo, daktari ambaye alimzalisha msichana huyo mtoto katikati ya safari ya ndege hiyo amefafanua tukio ambao aliona kichwa kidogo cha kitoto hicho kikitokeza.
Dk Julie Williamson alisema mama huyo kijana alijifungua mtoto wake mdogo wa kiume 'katika misukumo miwili' kabla ya kurejea katika kiti chake kumalizia safari yake.
Dk Williamson alikuwa akirejea nyumbani kutoka katika mkutano wa kitabibu nchini Afrika Kusini ndipo Fatoumatta alipoingia chumba cha kuzalia masaa manne baada ya ndege kuruka.
Huku abiria wakipatwa na hofu kubwa, Fatoumatta alijifungua mtoto wake Mamel Joella bila purukushani, madaktari walisema.
Alieleza: "Wakati kukiwa na mijadala mingi kama ndege ibadilishe uelekeo, alifanya uamuzi kwa niaba yetu kwa kusema, "Sukuma!" Na tulipotazama, mtoto huyo alikuwa akitoka, na alijifungua kwa misukumo miwili."
Shirika la Ndege la Afrika Kusini lilisema mshangao huo wa kujifungua ndani ya ndege uliisha salama katika kesi ya Fatoumatta lakini asingeweza kuwa na bahati hivyo, ndio sababu abiria wanatakiwa kulitaarifu shirika la ndege kama wapo kwenye hatua za mwisho za ujauzito.
"Jukumu la awali linabaki kwa abiria kulitaarifu shirika la ndege kwa hali yoyote ya kiafya," Tlali alisema. "Kama hawatafanya hivyo wanahatarisha kujiingiza wenyewe katika hatari na watoto wao ambao hawajazaliwa hasa kwenye kupata matatizo kadhaa katika uzazi."
Shirika hilo lilisema haikupangwa kubadili sera yoyoye kuhakikisha mwanamke ambaye yuko katika zaidi ya wiki 35 kutopanda ndege bila kukaguliwa tena.
"Hakuna namna yoyote tunayoweza kuwatambua abiria tunaoamini wanaweza kuwa wajawazito. Kuwatazama kwenye mashine maalumu kutaleta kiasi kikubwa cha usumbufu," Tlali alieleza.
"Hakuna shirika lolote la ndege duniani linaloweza kufanya hivyo."
"Kama mtu ni mjamzito wanatakiwa kuwa wamekaguliwa na daktari wanayemtaka na kuonesha uthibitisho kwamba daktari amewapatia ruhusa ya kusafiri."
Tunashukuru, Fatoumatta na mtoto Mamel wanaendelea vizuri hospitali - na msichana huyo jasiri anasisitiza kwamba kujifungua katika umbali wa futi 38,000 haikuwa mateso.
Fatoumatta alisema juzi: "Sikuwa nikihofia kuwa na mtoto, nilikuwa na furaha mno. Najisikia vizuri sasa baada ya kujifungua mtoto huyo. Kila kitu kiko sawa."
Anapanga kuishi na familia yake kwa wiki kadhaa baada ya kuwa ameruhusiwa kutoka hospitali, na kisha baadaye atarejea Afrika kuungana na mumewe, mwanadiplomasia wa Gambia mwenye miaka 38, Abubakary Jawara.
Alieleza hakuwahi kufikiria kuja kuwa kitovu cha mvuto wa hisia kiasi hicho baada ya tukio hilo la Jumamosi.
"Nilitarajia tu kuja hapa na kufurahi na kutembelea familia yangu na kisha kurejea kwa mume wangu," alisema.
Wakati msichana huyo alipokwenda chumba cha kuzalia, mfanyakazi wa ndani ya ndege aliuliza kutumia vipaza sauti vya ndani kama kuna daktari miongoni mwa abiria.
Kwa bahati ya Fatoumatta, ambaye asili yakr ni kutoka Angola, Dk Williamson, alikuwa njiani kurudi nyumbani kwake California kutoka kwenye mkutano wa kitabibu nchini Afrika Kusini, sambamba na Dk Steve Paridon.
Ilikuwa changamoto kubwa kwa Dk Williamson - mama wa watoto wawili ambaye hakuwahi kuzalisha mtoto tangu alipokuwa kwenye shule ya udaktari miaka 15 iliyopita.
Abiria walishangazwa kwamba msichana huyo hakupiga kelele wakati wote wa kujifungua masaa manne ndani ya ndege hiyo katika safari ya masaa 14.
Mtoto wake wa kiume aliyezaliwa haraka akafunikwa kwa mablanketi na kuchukuliwa na mfanyakazi wa ndege huku wakitembea kwenda na kurudi kwenye njia kati ya viti.
Shirika la Ndege la Afrika Kusini, lilifikiria kubadili uelekeo wa ndege hiyo, lakini mara baada ya wawili hao kuonekana kuwa salama waliendelea na safari kama ilivyopangwa, huku Fatoumatta akirejea kwenye kiti chake kwa mapumziko ya safari.
Mara walipotua, mama na mtoto walipelekwa kwenye Kituo cha Afya cha Jamaica huko Queens kwa ajili ya uchunguzi baada ya kuwasili nchini Marekani.
Wifi wa Fatoumatta alikutana nao kwenye uwanja wa ndege na kuwapeleka hospitali ambako walithibitishwa kuwa na afya njema.
Mamel hatoweza kuhesabiwa kama raia wa Marekani sababu ndege hiyo haikuwa katika anga la Marekani wakati mama yake alipojifungua.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4621

Trending Articles