Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

WATENDAJI, WATAALAMU SERIKALI WATUHUMIWA KUHUJUMU MAWAZIRI...

$
0
0
Wabunge wakiwa kikaoni mjini Dodoma.
Watendaji na wataalamu wasio waaminifu serikalini wamedaiwa kutumiwa na baadhi ya watu ili kuangusha mawaziri, imeelezwa.

Hayo yalisemwa bungeni jana na Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) alipokuwa akichangia hotuba ya makaridio ya matumizi ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi mwaka wa fedha 2013/14.
Wakati akitoa kauli hiyo, baadhi ya wabunge pia walimtetea Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Joyce Ndalichako kwa utendaji wake na kusema hastahili kuwajibika.
Wengine waliiomba Kamati ya Kutathmini Machapisho ya Kielimu (EMAC) ivunjwe kutokana na hatua ya fedha za rada kutumika kununua vitabu visivyofaa na vinavyopotosha wanafunzi wa shule za msingi.
Nchemba, ambaye alichangia jana, alisema Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inaweza kubadilishiwa mawaziri kila kukicha, lakini tatizo ni baadhi ya watendaji na wataalamu wasio waaminifu.
"Kuna baadhi ya watendaji na wataalamu serikalini ambao si waaminifu wamekuwa wakiwaangusha mawaziri wetu kwa makusudi kwa sababu ya kutumiwa na baadhi ya watu," alisema na kusisitiza kuwa kuwalaumu Dk Shukuru Kawambwa (Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Naibu wake, Philipo Mulugo ni kuwaonea.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakifanya kazi vizuri, lakini baadhi ya watendaji kwa sababu wanazozijua wao na wanaowatuma, wamekuwa wakifanya juhudi kuwaangusha na matokeo yake ni kuonekana hawafai kwa jamii na kusababisha wizara hiyo kubadilishiwa mawaziri mara kwa mara.
Alisifu juhudi za Serikali kuboresha elimu, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa shule za sekondari na kueleza kuwa hata Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) aliwahi kusifu juhudi za Serikali ya Awamu ya Nne kuhusu elimu, hali ambayo iliudhi wakubwa zake kwenye chama na kusababisha awekwe ‘kitimoto’ na kupokwa uwaziri kivuli.
"Kawaambieni hao mnaowatuma kuhujumu mawaziri, kwamba nchi ni Tanzania si CCM," alisema Nchemba bila kufafanua wala kutaja majina yao.
Mbunge wa Kuteuliwa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuna haja ya EMAC kuvunjwa kutokana na kuvipa hati ya ithibati vitabu vya kiada katika shule ambavyo vina upungufu mkubwa.
"Mara nyingi huwa nasema elimu ndiyo mapigo ya moyo na ukitaka kuua Taifa lolote basi ua elimu... tunavuna tulichopanda. Vitabu vinavyotumika kufundisha watoto wetu vina matatizo makubwa na ndiyo sumu ninayoizungumzia.
"Kati ya vitabu vilivyotolewa, kuna kimoja cha darasa la pili kina hesabu inasema 2x7= 15, halafu cha darasa la nne hesabu inasema sifuri ukigawa kwa sifuri sawasawa na sifuri, wakati haiwezekani. Tunajenga Taifa la namna gani?" Alihoji Mbatia.
Pia alieleza kuwa katika vitabu hivyo, kipo cha Uraia ambacho kinatoa tafsiri ya mtaa ambayo ni potofu. "Kitabu cha Uraia darasa la nne kinasema, mtaa huundwa na vitongoji na viongozi wa vitongoji," alisema Mbatia na kueleza kwa kupitisha vitabu ambavyo vimenunuliwa kwa chenji ya rada EMAC inapaswa ivunjwe kwani kilichofanyika ni ufisadi.
Akijumuisha, Naibu Waziri Mulugo alilitangazia Bunge kuwa Serikali imechukua hatua ya kuivunja EMAC kwa kuwa haikuwa inafanya kazi vizuri na hivyo kitaundwa chombo kingine kuchukua nafasi yake, akisema haikuwa inafanya vikao vinavyotakiwa.
Alisema vitabu vyote ambavyo havina ithibati vitakaguliwa kimoja baada ya kingine na kuviondoa mara moja katika matumizi ya shule.
Mbatia alimsifu Dk Ndalichako na kueleza kuwa anastahili kupongezwa kwa kazi nzuri anayofanya katika masuala ya elimu nchini na kuonya wabunge wanaotumia mwavuli wa dini kuhoji masuala ya kielimu kwamba wanaipeleka nchi kubaya na kuwaomba wasigawanyike kwa itikadi za kisiasa au dini na kufanya hivyo ni kuipelekaTanzania mahali pasipofaa.
Mbunge wa Mtambire, Masoud Abdallah Salim (CUF), alipendekeza upelekwe bungeni muswada wa kudhibiti vitabu visivyo na ubora kwa nia ya kuboresha elimu nchini.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi) naye akichangia hotuba hiyo juzi jioni alimfagilia Dk Ndalichako na kusema kuwa wanaotaka awajibike ni wale walioona amedhibiti wizi wa mitihani, kauli ambayo pia ilizungumzwa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) aliyesema Dk Ndalichako ni mfano wa kuigwa katika utendaji Baraza la Mitihani la Taifa.
Mkosamali pia aliwalaumu baadhi ya wabunge kwamba hawaguswi na suala la elimu kwa sababu wengi wao watoto wao hawasomi katika shule za kawaida badala yake wanasoma zile zinazotambulika kuwa zina mchepuo wa Kiingereza.
Baadhi ya wabunge waliochangia jana ambao pia walipongeza utendaji wa Dk Ndalichako ni wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema) na Gosbert Blandes (Karagwe-CCM).

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4500

Trending Articles