Baadhi ya maofisa wa kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na halmashauri nchini wameshutumiwa kuwa wala rushwa kiasi cha kufanya wenye nia na utayari wa kulipa kodi nchini kutofanya hivyo kwa kukosa imani nao.
Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti ya REPOA, Rose Aiko alibainisha hayo Dar es Salaam jana, wakati akitangaza matokeo ya utafiti wa taasisi hiyo kwa ushirikiano na Mtandao wa Watafiti wa Afrika (AFROBAROMETA) kuhusu mtazamo na ufikiri wa watu juu ya kodi na uadilifu wa maofisa wa kodi nchini.
Utafiti huo uliofanywa mwaka jana kwa mara ya tano uligusia maeneo tofauti kuhusu kodi na kuelezwa kulenga kufahamu endapo wananchi wana uelewa wa kutosha kuhusu kodi wanazolipa, sera za kodi na endapo wanapata taarifa kuhusu kodi hizo au la, pamoja na kupata maoni yao kuhusu uadilifu wa maofisa kodi.
"Asilimia 86 ya tuliofanya mahojiano nao walisisitiza kupoteza imani na maofisa kodi nchini kutokana na maelezo kwamba ni wala rushwa." Aiko alisema na kufafanua kuwa hata kama maofisa Kodi kutoka makao makuu ya TRA watajitetea kuwa wanafanya vizuri, maoni ya wananchi kuhusu maofisa kodi yameonesha kuwa kuna mtazamo hasi kuwahusu.
Kwa mujibu wa Aiko, tofauti na ilivyokuwa mwaka 2003 walipofanya utafiti kama huo, wa sasa umezidi kuthibitisha kuwa kuna tatizo miongoni mwa maofisa kodi na juhudi ni lazima zifanyike kumaliza tatizo hilo, ili kurejesha imani ya watu iliyopotea kwa sababu ndio walipa kodi.
"Najua maofisa wa TRA pengine wanafanya kazi yao kama wenyewe wanavyodai, lakini walipa kodi wametoa maelezo yao, wametufunulia uelewa wao na kutuwekea bayana ufikiri na maoni yao juu ya maofisa wetu wa kodi, sisi watafiti tunawasilisha yaliyojiri kutokana na utafiti wetu na ushauri wetu kwa Serikali na maofisa kodi pia tunautoa kulingana na tulichokibaini na wala si vinginevyo,” alisema.
Hata hivyo, Ofisa wa TRA anayehusika na masuala ya utafiti kutoka Makao Makuu ya Mamlaka hiyo, Kailembo Yahya, alikanusha madai hayo ya wananchi kuhusu rushwa na kusema kuwa yanayoelezwa yalikuwa yakitokea zamani na wala si sasa.
Kailembo aliyehudhuria utangazwaji wa matokeo hayo, alisema labda kama rushwa inaliwa na watu wengine nje ya TRA kwa sababu utaratibu wa kufukuza wasio waaminifu na waadilifu na kutolewa kwa adhabu nyingine kama vile kushushwa vyeo, kusimamishwa kazi na kufikishwa mahakamani kumeogopesha wengi na kuwafanya wajirekebishe.
"Utafiti wowote ukifanywa lazima utolewe majibu, hilo mimi siwezi kupingana nalo na majibu si lazima yatolewe kuufurahisha upande mmoja, yanaweza kufurahisha na hata kuumiza upande wowote.
"Lakini kwa hili la wananchi kusema maofisa kodi tumezidi kula rushwa mimi nakataa na kusema ilikuwa zamani si sasa, kwa sababu kila mmoja anaogopa kuharibu kwa sababu hakuna kinachoweza kujificha sasa. Watu wanalipa kodi kwa hiyari, hivyo mazingira ya kuwafanya wakupe rushwa hayapo," Kailembo alisema.
Alieleza pia kuwa hata hiyo zamani maofisa wa kodi hawakuwa washawishi wa kupewa rushwa bali walipa kodi kwa kutojua kwao kuwa kutoa rushwa ni kosa walikuwa wakitengeneza mazingira ili wazitoe na kukwepa kodi.
"Ushahidi mtakuwa mnauona, kwamba kesi nyingi ziko mahakamani na wengine bado wanachunguzwa," aliongeza.
Katika hatua nyingine, utafiti huo ulionesha kuwa nchini bado hali ya upatikanaji taarifa kuhusu aina ya kodi inayopaswa, lini na wapi ni tatizo, kwa sababu wanaozihitaji hawazipati.
Kadhalika ilibainishwa kuwa Watanzania wengi hasa vijijini, hawajui kama wanalipa kodi katika vyakula na bidhaa nyingine ndogo, pindi wanapozinunua kutokana na ukweli kwamba hawana utaratibu wa kuchukua stakabadhi.