Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4623

KALI YA MWAKA!! KIDHIBITI CHA COCAINE CHAGEUKA CHUMVI POLISI...

$
0
0
Polisi nchini imeendelea kuanikwa, ambapo tofauti na ilivyokuwa ada kwa asasi za kiraia kutoa ripoti ya madudu ndani ya taasisi hiyo muhimu, safari hii Serikali imeyabaini na kuwachukulia hatua wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, alitaja kituko kilichofanyika, kuwa ni kuyeyuka ghafla kwa kidhibiti cha dawa za kulevya aina ya cocaine kilogramu 1.9.
Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, kidhibiti hicho kilikamatwa katika Mpaka wa Tunduma mkoani Mbeya Machi mwaka jana, na kuhifadhiwa katika stoo ya Kitengo cha Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU).
Baada ya kuhifadhiwa, Dk Nchimbi alisema baadaye kilisafirishwa hadi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali mkoani Dar es Salaam, kwa nia ya kupata uthibitisho.
Alisema wakati wa kupimwa, ndipo ilipobainika kuwa ni sukari na chumvi na wala si dawa za kulevya zilizokamatwa.
Dk Nchimbi alisema matokeo hayo yalizua utata, uliosababisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya, kumuandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kumtaka afanyie uchunguzi suala hilo.
“Niliunda timu maalumu ya kufuatilia suala hili na ilijiridhisha kuwa kidhibiti hicho cha chumvi na sukari kilichopelekwa kwa Mkemia Mkuu, si kile cha dawa za kulevya aina ya cocaine, zilizokamatwa na polisi,” alisema.
Baada ya kujiridhisha kuwa kidhibiti ‘kimechakachuliwa’,  Dk Nchimbi alisema Serikali iliamua kuwachukulia hatua watuhumiwa wa sakata hilo.
Aliwataja watuhumiwa hao waliosimamishwa kazi kuwa ni aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Elias Mwita, aliyekuwa Msaidizi wa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Mbeya, Jacob Kiango na aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya, Charles Kinyongo.
Alidai kuwa watuhumiwa hao mwaka jana katika kituo cha Polisi cha Mpaka wa Tunduma mkoani Mbeya, wakishirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), walificha kidhibiti hicho na kuweka chumvi na sukari kama ndio kidhibiti kilichokamatwa.
Alisema maofisa hao wanatarajiwa kupandishwa kizimbani wakati wowote, kujibu tuhuma zinazowakabili.
Aidha, Serikali pia imemsimamisha kazi aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Serengeti, Paul Mng’ong’o, kwa kosa la kuingia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, na kupanga njama ya kuchimba dhahabu.
Njama hiyo kwa mujibu wa madai ya Dk Nchimbi, ilisababisha  bosi huyo wa Polisi ngazi ya Wilaya, kushitakiwa katika Mahakama ya kiraia huko Serengeti.
Dk Nchimbi alisema pia Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Renatus Chalamila, anayesimamia ajira ndani ya jeshi hilo, amepewa likizo ya mwezi mmoja, baada ya kutajwa kuhusika kuwatoza fedha vijana walioomba ajira Polisi, ili awapatie kazi hiyo.  
“Ni Rais pekee ndio anayeweza kumuadhibu ofisa wa Polisi mwenye cheo cha Kamishna, wengine wenye vyeo vya chini wanaweza kuadhibiwa na Waziri au Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP),” alifafanua Dk Nchimbi sababu za kumpa likizo badala ya kumsimamisha kazi Kamishna huyo.
Moja ya athari ya tuhuma dhidi ya Chalamila, Dk Nchimbi alisema Polisi imelazimika kuwaondoa katika mafunzo, askari wanafunzi 95 waliokuwa wamejiunga na Chuo Cha Polisi, baada ya kubainika kwamba walipata fursa hiyo kwa kutoa fedha.
Katika hatua nyingine, Dk Nchimbi alisema aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi mkoani Kagera, Peter Matagi, amesimamishwa kazi kwa tuhuma za kubambikia kesi wananchi.
Alidai kuwa Matagi, alikutwa na hatia ya kukiuka taratibu za kazi, kwa kuwabambikiza kesi zisizo na dhamana wananchi 13 wa Kata ya Nyakasimbi, katika Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera.
Wananchi hao kwa mujibu wa Dk Nchimbi, walikuwa na tuhuma za kuhusika katika vurugu za kugombea ardhi, ambazo haziwiani na aina ya mashitaka waliyoshitakiwa, hali inayoonesha dalili ya kuwepo rushwa.
Wananchi hao inadaiwa walibambikizwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha, na walikaa mahabusu kwa miezi miwili.
Alisema timu ya uchunguzi, iliyoongozwa na yeye mwenyewe, iligundua baadaye kuwa mashitaka waliyoshitakiwa wananchi hao, hayakuwa sahihi na kusababisha Mwendesha Mashitaka Mkuu wa Serikali (DPP), kufuta kesi hiyo.
Dk Nchimbi alisema Matagi mbali na kusimamishwa kazi, atafunguliwa mashitaka ya kijeshi, kutokana na kukiuka utaratibu wa kazi kwa kuwabambikizia kesi wananchi hao.
Alisema vitendo hivyo vinavyofanywa na viongozi wa   Polisi, vinavunja moyo na kuwapa hofu askari wa ngazi ya chini, ambao hushindwa kufanya kazi zao kwa uadilifu unaotakiwa.  
Aliahidi kuwa Serikali itawaunga mkono askari wanaofanya kazi kwa uadilifu, ila watakaoenda kinyume na maadili na taratibu za Polisi, haitasita kuwachukulia hatua za kisheria ikiwemo kuwafukuza kazi.
Hatua hizo zilizochukuliwa na Serikali kwa mujibu wa Dk Nchimbi, ni sehemu ya makubaliano ya maofisa waandamizi wa Polisi nchini, waliokutana hivi karibuni mjini Dodoma.
Alisema lengo ni kulinda maadili ya Polisi na kukabiliana na vitendo vyote vinavyochafua jeshi hilo kwa jamii, ili kutatua kero za wananchi na kuzingatia utawala bora.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4623

Trending Articles