![]() |
John Cheyo. |
Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), amesema kama Bunge limeshindwa kuliokoa Taifa na matatizo ya uvunjifu wa amani nchini, kiasi cha kufikia kumtukana Rais, halina budi kuvunjwa ili kwenda katika Uchaguzi Mkuu.
Akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi jana bungeni mjini hapa, Cheyo alisema amani ya nchi lazima ipatikane kwa bei yoyote ile.
“Mimi ni mzee hapa nchini na pia ndani ya Bunge. Amani ya nchi lazima ipatikane kwa gharama yoyote ile… huwezi kwenda kanisani kuabudu halafu huna uhakika kama wewe na mkeo na watoto wako mtatoka salama.
“Na kama tumeshindwa, na kufikia hatua ya kumtukana hata Rais wa nchi, basi afadhali tuombe Rais alivunje Bunge, ili twende kwenye Uchaguzi Mkuu wakachaguliwe watu wenye ujasiri, ambao watawafanya watu waende kanisani na misikitini kuabudu kwa amani,” alisema Cheyo.
Kauli hiyo inaendana na Azimio la Bunge hivi karibuni, ambapo baada ya kubaini kuwa wabunge ndio chanzo cha uvunjifu wa amani kutokana na kauli zao bungeni, waliona ipo haja ya kuangalia upya sheria ikiwamo ya kinga ambayo inawapa uwezo wa kutoa kauli hizo.
“Pande zote za wabunge zimekuwa zikitoa lugha za chuki ndani ya Bunge kwa kisingizio cha kinga, hili halifai, halifai, halifai, sisi tunaanzisha wimbo humu ndani na watu wanaitika. Tuzuie kauli za chuki ndani na nje ya Bunge,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Anna Abdallah.
Akitangaza Azimio hilo kuhusu kulipuliwa bomu kwa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Arusha Mei 5, Anna alisema wabunge wengi wamekuwa wakitoa lugha za chuki kwa kisingizio cha demokrasia na kuwakumbusha kuwa hakuna demokrasia isiyo na mipaka.
Cheyo pia aliungana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya, ambaye alilazimika kuchambua safu ya uongozi Ikulu, baada ya kusikia kauli ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) bungeni, kuwa Rais Kikwete ni mdini.
Akizungumza bungeni kuhusu kauli hiyo, Profesa Mwandosya alisema baada ya kusikia kuwa kumeibuka kauli hizo za udini, tena dhidi ya Rais Kikwete binafsi, alianza kuangalia Ikulu, ambako ndipo alipo Rais.
Alisema, kwa haraka alibaini kuwa mawaziri wote wanne wa nchi, wanaomsaidia Rais Ikulu ni Wakristo wakati Rais ni Mwislamu.
Mawaziri hao ni pamoja na Profesa Mwandosya mwenyewe; asiye na wizara maalumu; Waziri anayeshughulikia Uhusiano na Uratibu, Steven Wasira; wa Utumishi, Celina Kombani na Utawala Bora, George Mkuchika.
“Makatibu wakuu wote wanaomsaidia Rais ni Wakristo, Katibu wake na wakurugenzi wote akiwamo wa Mawasiliano ni Wakristo, sasa hapo udini uko wapi? Sisi Watanzania ni jambo la ajabu kwetu na la kigeni kuzungumzia udini…hili ni shetani anapita tu, nchi itakuwa imara, hakuna udini,” alisisitiza.
Waziri huyo ambaye ni Mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM), pia alishangazwa na wabunge kuhoji kazi za Usalama wa Taifa pamoja na kuzungumzia masuala ya ulinzi na usalama bungeni, wakati masuala hayo duniani kote yanazungumzwa katika vikao vya siri na si bungeni.
“Mambo ya ulinzi na usalama ni siri, haiwezekani kulizungumzia hapa hata Israel, Marekani mambo hayo yanazungumzwa katika vikao vya ndani,” alisema.