Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4605

WILFRED RWAKATARE NA WENZAKE WAKOSA DHAMANA...

$
0
0
Wilfred Rwakatare akiwa ndani ya basi la mabahusu.
Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Rwakatare na mshitakiwa mwenzake Ludovick Joseph, wameendelea kusota rumande, baada ya ombi lao la dhamana kukwama kwa kuwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo hayupo.

Wakili wa Rwakatare, Peter Kibatala aliwasilisha ombi hilo jana mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidai mashitaka yanayowakabili wateja wake, yana dhamana.
Hata hivyo Hakimu Fimbo alisema hawezi kushughulikia ombi hilo, kwa kuwa yeye si hakimu husika anayesikiliza kesi hiyo, hivyo atarekodi hoja zao katika jalada la kesi, ili Hakimu Aloyce Katemana akirudi azipitie.
Awali akiwasilisha maombi hayo, Kibatala alidai kuwa anaamini kuna nakala ya uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, ambao uliwafutia mashitaka ya ugaidi washitakiwa hao na kubaki mashitaka ya jinai, chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu ambayo yanadhaminika.
Kwa sasa washitakiwa hao, wanakabiliwa na mashitaka ya kula njama ya kutaka kumdhuru kwa sumu Mhariri wa Gazeti la Mwananchi, Dennis Msacky, mashitaka ambayo yana dhamana.
Kibatala alidai kuwa ingawa Hakimu Katemana anayesikiliza shauri hilo hayupo, sheria inairuhusu Mahakama hiyo kutoa dhamana kwa washitakiwa.
Aliongeza kuwa dhamana ni haki ya washitakiwa, hasa ikizingatiwa wameshakaa rumande kwa muda mrefu na Rwakatare hali yake kiafya si nzuri inastahili Mahakama kutoa dhamana, kwa masharti itakayoona yanafaa.
Hoja hiyo ilipingwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Prudence Rweyongeza, aliyedai kuwa ombi hilo, halijawasilishwa kwa wakati mwafaka, kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), bado hajawasilisha taarifa katika Mahakama hiyo.
Hata hivyo, Wakili Kibatala alidai kuwa msimamo wa sheria uko wazi na mahakama za chini, zina uwezo wa kutoa dhamana na madai ya Wakili Rweyongeza, hayazuii dhamana ambayo ni haki ya washitakiwa.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Fimbo alisema Hakimu amerekodi hoja hizo na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 27, itakapotajwa tena.
Wafuasi wa Chadema waliokuwa wamejaa eneo la Mahakama, waliondoka hapo kimya baada ya kupata taarifa ya kukwama kwa dhamana ya Rwakatare.
Mei 8, washitakiwa hao walifutiwa mashitaka ya kupanga njama za kufanya kitendo cha ugaidi cha kumteka Mhariri Msacky, kupanga na kushiriki mkutano wenye lengo la kutenda kitendo cha ugaidi, ambacho ni kumteka na kufanya mkutano wa kigaidi.
Jaji Lawrence Kaduri alifuta mashitaka hayo, kwa kuwa hati ya mashitaka iliyofunguliwa na DPP, haielezi uhalisia wa kosa hilo na washitakiwa wanahusika vipi kufanya ugaidi. 
Jaji huyo alifafanua, kuwa “hati ya mashitaka lazima itoe uhalisia wa kosa husika (ugaidi), ili haki itendeke.”

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4605

Trending Articles