![]() |
Wachimbaji wakiwa kazini katika mchimbo ya madini ya Mererani. |
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amecharuka na kuagiza Serikali kuwa na hisa katika migodi yote ya madini itakayofunguliwa kuanzia sasa.
Alisema hisa hizo zitakazoingiwa kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) zitasaidia kuondoa manung’uniko kwa wananchi kuwa nchi inaibiwa katika Sekta ya Madini.
Alisema chini ya mpango mpya katika sekta hiyo, nchi kuanzia sasa itanufaika katika maeneo matatu aliyoyataja kuwa ni kukusanya kodi, kulipwa mrabaha na kupata mapato kutokana na umiliki wa Serikali katika migodi hiyo kupitia hisa.
Waziri Muhongo pia ameeleza nia ya serikali ya kuwabana wachimbaji wadogo wa madini ili waweze kulipa kodi stahili kutokana na sasa wengi wao hasa wa tanzanite katika Migodi ya Mirerani wilayani Simanjiro kuiibia Serikali na kufanya mchango wao katika kodi kuzidiwa hata na walimu na wauguzi wa eneo hilo.
Aidha, amefichua siri kwamba wakati wa kuingia Mikataba ya Madini, Watanzania wamekuwa wanakwenda mikono mitupu bila ya kuwa na rasimu yenye kuwapa dira ya ni nini vipaumbele vya serikali kwenye mikataba hiyo, hatua inayoifanya mikataba hiyo kuwa mibovu.
Waziri Muhongo aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizindua Bodi ya STAMICO itakayoongozwa na Mwenyekiti wake, Rumisha Kimambo.
Alisema katika marekebisho ya sasa shirika hilo litakuja na sura mpya ya kitaifa ambayo haitawabagua Watanzania katika utafutaji na uchimbaji wa madini.
“Tusikubali kutoa hisa kwa halmashauri au vyama vya ushirika, kwani kuna changamoto mbalimbali na itakuwa kugawa nchi kwa sehemu ambazo hazina migodi, sasa Stamico inaingia katika biashara ya madini,” alisema.
Alitoa mifano ya baadhi ya migodi ambayo tayari Stamico imeanza kuingia ubia kuwa ni pamoja na ule wa Geita na aliiagiza Bodi hiyo kusimamia ili mgodi huo uanze uchimbaji haraka.
Aliutaja mwingine kuwa ni ule wa Buhemba ambao Bodi inatakiwa kusimamia mapato ya aina mbili ambayo ni mabaki yenye thamani ya dola za Marekani milioni 70 na mapato ya uchimbaji yanayosimamiwa na Kampuni ya Australia.
Kuhusu Mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, Waziri huyo alisema matatizo yake yamekwisha na malipo yamefanyika na kwamba fedha zilizobaki zitakamilika wiki ijayo ili mgodi huo uanze uzalishaji wa megawati 200 za umeme ambapo utasimamiwa na Kampuni ya China na Stamico.
Alisema pia shirika hilo litashiriki katika uchimbaji wa madini ya Urani ambapo majadiliano yako katika hatua za mwisho na kuagiza Bodi kufuatilia mpango huo.
Kuhusu Mgodi wa Tulawaka uliopo Biharamulo, Waziri alisema muda mfupi ujao wawekezaji wataondoka na Stamico wataendelea kuchimba wenyewe bila kuingia ubia.
Akizungumzia ukwepaji wa kodi katika kampuni za uchimbaji wa madini ya tanzanite katika eneo la Mirerani, Waziri Muhongo alisema kati ya leseni 597 zilizopo ni leseni 119 tu ndizo zilizotoa taarifa kuhusu uchimbaji wake serikalini katika kipindi cha miaka sita.
Alisema hata hivyo kati ya leseni hizo 119 zilizotoa ripoti, 106 zimeeleza kuwa hazikupata faida katika kipindi hicho chote cha miaka sita, huku tatu zikiwa hazikulipa mrabaha kabisa huku 10 zilizosalia zikilipa Sh milioni 34 tu sawa na kulipa Sh 567,000 tu kwa mwaka.
“Ukiangalia takwimu hizo ni wazi muuguzi na mwalimu wa Mirerani wanalipa kodi kubwa serikalini kuliko wachimbaji madini ya Tanzanite, hivyo nawaagiza Bodi kuhakikisha mnabadili takwimu hizo.”
Aliitaka Bodi pia kusimamia sekta ya wachimbaji wadogo na kuhakikisha inabadili hali hiyo ya ukwepaji wa kodi na inatoa mchango mkubwa katika bajeti ya Serikali na kupunguza ufinyu wake.
Alisisitiza kuwa ni lazima Serikali ifike wakati wa kuacha kufukuzana na wauza mchicha na kutafuta fedha katika madini, na kusema leseni zilizopo Mirerani ni mfano tu kuonesha kwamba wachimbaji wadogo hawalipi kodi.
“Hivyo Stamico mbali na kuwapa jukumu la kuwasaidia kwa kuwapatia vifaa, kuwatafutia masoko kwa kuwaunga katika vikundi, pia serikali itaweza kukusanya kodi na kuongeza mapato kwa serikali,” alisema.
Aliigiza Bodi hiyo kusimamia kwa umakini mikataba mbalimbali ili ifanyike kwa umakini na haraka bila kuwepo kwa vitendo vya rushwa, ubabaishaji na wizi.
“Nimebaini katika mashirika mengi kuna udhaifu wa watendaji kwenda kujadili mikataba bila kuwa na vipaumbele na kujadili vya wengine akiona hajaafiki anaenda kurekebisha, jambo ambalo ni sababu ya mikataba kujadiliwa kwa muda mrefu,” alisema.
Alibainisha kuwa ni jambo la ajabu kuona Mtanzania anaingia katika kikao cha kujadili Mkataba akiwa hana nyaraka yoyote na hivyo aliitaka Bodi hiyo kuhakikisha inaoneshwa vipaumbele kabla ya kuruhusu kujadili mikataba.
Mwenyekiti wa Bodi, Kimambo alisema bodi yake itahakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo ili kutimiza malengo ya serikali.
Wajumbe wengine ni Hildebrand Shayo, Mhandisi Rashid Mkemai, Abdalla Mussa, Dk Anderson Mlaki, Chacha Chambiri, Mhandisi Edwin Ngonyani, Alexander Muganda na Dk Godwin Kaganda.