
Joseph Dominick (33) baada ya kumuua mkewe huyo mwenye miaka 26, alijaribu kujiua kwa kujichoma kisu tumboni, lakini hakufa na amelazwa katika Kituo cha Afya cha Kamasamba wilayani Momba mkoani Mbeya akiwa chini ya ulinzi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Frednand Rwegasira alisema mtuhumiwa alitenda uhalifu huo juzi saa 4:00 usiku akiwa nyumbani kwake kijijini Kawila na chanzo kikielezwa kuwa wivu wa mapenzi uliochanganyika na ulevi wa pombe.
“Mkewe alikufa papo hapo baada ya kuchomwa kisu kifuani ndipo mtuhumiwa naye aliamua kujichoma na kisu tumboni akijaribu kujiua lakini aliokolewa na majirani na kukimbizwa katika Kituo cha Afya alikolazwa kwa matibabu,” alieleza.
Katika tukio lingine, mkazi wa kijiji cha Kalaembe wilayani Kalambo, Braza Simfukwe (43) ameuawa baada ya kushambuliwa kwa kuchomwa kisu tumboni na wadogo zake watatu wa tumbo moja wakigombea mali za urithi zilizoachwa na marehemu baba yao.
Kaimu Kamanda Rwegasira amewataja ndugu hao watatu waliotenda uhalifu huo kuwa ni pamoja na Mogani Simfukwe, Gervas Simfukwe na Kilani Simfukwe ambao wote walitoroka baada ya kutenda uhalifu huo na sasa wanasakwa na Polisi.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda, uchunguzi wa awali umebaini kuwa baada ya baba yao kufariki dunia mwaka jana, Braza alianza kumiliki mali zake alizoziacha ikiwemo nyumba na mashamba, kitendo kilichowachukiza wadogo zake na kusababisha mgogoro mkubwa baina yao.
Inadaiwa Braza alifuatwa na wadogo zake hao watatu wenye hasira akiwa nyumbani kwake kijijini humo na kumshambulia kwa visu ambapo alifikwa na mauti katika Kituo cha Afya cha Matai alikolazwa kwa matibabu.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda huyo, mkazi wa kitongoji cha Bangwe, Manispaa ya Sumbawanga, Malyatanga Mwami (42) alikufa baada ya kuanguka ghafla akiwa njiani kurejea kwake akitoka kunywa pombe za kienyeji kilabuni.
“Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa Mwami alikunywa pombe kwa muda mrefu bila kula …. uchunguzi zaidi wa mkasa huo bado unaendelea," alieleza Rwegasira.
Katika hatua nyingine, Rwegasira alibainisha kuwa mtu mmoja amekufa wilayani Sumbawanga katika ajali ya barabarani iliyotokea saa 1:00, juzi kijijini Miangalua katika barabara ya Sumbawanga – Mbeya.
Inadaiwa ajali hiyo ya barabarani ilihusisha gari aina ya TATA yenye namba za usajili T 568 ATR lililokuwa likiendeshwa na Andrew Mwandembwa (30) mkazi wa eneo la Soweto, Jijini Mbeya lililogongana na pikipiki aina ya T/BETTER yenye namba za usajili T 211 CVD.
Alitamja marehemu kuwa ni Derick Tano 'Laiton' (24) , mkazi wa kijiji cha Miangalua kwamba uchaguzi wa awali umebainisha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa pikipiki ambapo dereva wa gari amekamatwa na atafikishwa mahakamani mara uchunguzi wa awali utakapokamilika.
Rwegasira amebainisha kuwa mkazi wa eneo la Katandala, Manispaa ya Sumbawanga aliyefahamika kwa jina moja la Manson anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 25 ameuawa na kundi la wananchi wakimtuhumu kuwa mwizi. Hakuna yeyote aliyekamatwa kuhusu mauaji hayo na uchunguzi zaidi unaendelea.