Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

IPTL YATOA MILIONI 14.5/- KUSAIDIA UJENZI WA KANISA

$
0
0
Kampuni ya ufuaji umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) imetoa msaada wa Sh milioni 14.5 kwa Jumuiya ya Kanisa la Mtakatifu Petro lililopo Oysterbay jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kusaidia ujenzi wa kanisa hilo.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi kwa jumuiya hiyo, Mwenyekiti Mtendaji wa IPTL, Harbinder Singh Sethi, alisema IPTL imetoa msaada huo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wao wa kuwezesha miradi mbalimbali za kijamii ambayo inagusa maisha ya watu wengi.
 “Jitihada hizi ni moja kati ya mkakati wetu wa utekelezaji wa mpango wetu wa kutumia sehemu ya faida tunayopata kutokana na shughuli zetu, kwa kuiwezesha jamii katika nyanja za kimaendeleo ikiwemo kiuchumi. Misaada kama hii hailengi tu kusaidia vijana wa kitanzania kuendelea kiuchumi, pia misaada kwa taasisi za kidini itasaidia katika kujenga jamii inayo mcha Mungu, hivyo taifa kuwa katika mazingira mazuri ya kupiga hatua kubwa kimaendeleo,” alisema Sethi.
Sethi aliongeza kuwa kampuni yake ina mpango madhubuti unaolenga kusaidia shule, makanisa, misikiti na mashirika mengine yasiyo ya kibiashara na  kuwawezesha vijana kuwa wachangiaji wakubwa kwenye maendeleo ya kiuchumi Tanzania.
Kwa upande wake, Katibu na Mshauri Mkuu wa IPTL, Joseph Makandege, alisema IPTL ikiwa na mpango wake wa kuunga mkono jitihada  za kimaendeleo na kijamii, itaendelea kushirikiana na jumuiya mbalimbali ili kwa pamoja kuona kwamba fursa za kiuchumi zinazojitokeza zinapewa msukumo kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.
“Kama IPTL, tumeona kuwa ni jukumu letu kuisaidia jamii inayotuzunguka. Nina imani mchango wetu kwa Jumuiya ya Mtakatifu Petro utasaidia kuongezea nguvu ujenzi wa kanisa unaoendelea. Lengo letu ni kuona kwamba tunachangia maendeleo ya kiuchumi na bila kusahau jamii  inayotuzunguka zikiwepo jumuiya  za kidini,” alisema Makandege.
Kwa upande wake, Rose Rupia, Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Kanisa hilo, aliishukuru IPTL kwa msaada wake na kusema fedha zilizotolewa zitasaidia kwa kiasi kikubwa kusukuma mbele ujenzi wa kanisa hilo ambao bajeti yake ni zaidi ya Sh milioni 600.
“Naishukuru IPTL kwa kuona umuhimu wa kukubali ombi letu na kuja kutuunga mkono katika jitihada za ujenzi wa kanisa letu. Fedha hizi zitasaidia kusukuma mbele zaidi ujenzi wa kanisa letu, huu ni mfano mzuri wa kuigwa na makampuni mengine na watu binafsi,” alisema Rose.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4529

Trending Articles