Quantcast
Channel: ziro99blog
Viewing all articles
Browse latest Browse all 4588

MASHEKHE WALIPULIWA NA BOMU WAKILA DAKU ARUSHA

$
0
0
Wakati Waislamu wakiwa katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, watu wasiojulikana juzi walivamia nyumba ya Mkurugenzi wa Kanda ya Kaskazini wa Taasisi ya Kiislamu ya Answar Muslim Youth Centre, Shekhe Soud Ally Soud na kurusha kitu kinachodhaniwa kuwa  bomu na kumjeruhi shekhe huyo na mgeni wake kutoka Kenya.
Wawili hao walikuwa nyumbani kwa Shekhe Soud, eneo la Majengo Chini mjini hapa wakipata chakula cha usiku maalumu kwa funga, maarufu kama daku.
Mwingine aliyejeruhiwa amefahamika kuwa ni Shekhe Muhaji Hussein Kifea, raia wa Kenya ambaye amevunjwa miguu yote miwili na pia amepoteza vidole vitatu vya mguu wa kulia.
Tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Liberatus Sabas aliyesema linatokana na mgogoro wa muda mrefu wa ndani kwa ndani wa uongozi wa msikiti na taasisi wanayoiongoza, hali ambayo amedai haiwezi kuhusishwa na tukio la ugaidi.
Hata hivyo, aliahidi jeshi lake kufanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo ili kubaini mtandao mzima wa ulipuaji wa bomu hilo ambalo alisema ni la kutengenezwa kienyeji.
“Sisi tunaingia kazini kufanya uchunguzi na kubaini mtandao mzima uliohusika, lakini tukio hili hatulihusishi moja kwa moja na tukio lile la kigaidi ambalo kesi yake iko mahakamani,” alisema Kamanda Sabas.
Hali hiyo imejitokeza siku chache baada ya Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba kufanya ziara mkoani Arusha kwa lengo la kutoa maamuzi magumu kwa baadhi ya misikiti ya Jiji la Arusha kusimamiwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) ukiwemo msikiti mkuu wa Ijumaa wa Arusha.
Akizungumzia tukio hilo katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru wanakopatiwa matibabu, Shekhe Kifea alisema wakiwa katika mazungumzo huku wakipata daku, walisikia kioo cha dirisha kikivunjwa kwa kitu kilichorushwa na kuwajeruhi.
Anasema Shekhe Soud alikuwa akimsimulia jinsi anavyowindwa na kikundi cha waislamu wenzake kiasi cha kukoswakoswa kuuawa kwa risasi siku tatu kabla ya tukio hilo na ndipo muda mfupi tukio hilo likatokea.
“Mimi nilikuwa ndani ya nyumba ya Shekhe Soud akinihadithia kuhusu anavyowindwa na waislamu wengine huku tukila daku, lakini nadhani watu waliolipua bomu hilo walikuwa nje wakitusikiliza na ndipo tuliposikia kioo kikivunjwa na kisha bomu hilo likatupwa ndani na kulipuka,” alisema Kifea.
Hata hivyo alitoa wito kwa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini kuhakikisha vinapambana na matukio kama hayo, kwa kuwa yanachafua jina la nchi na hususani katika biashara ya utalii inayoliingizia taifa pato kubwa.
Naye Shekhe Soud akiwa hospitalini hapo alisema siku tatu kabla ya tukio hilo alitishiwa kuuawa kwa kurushiwa risasi akiwa maeneo jirani na nyumbani kwake na watu anaoamini ni wale wanaopingana nao kuhusiana na masuala ya kidini na taasisi hiyo anayoiongoza na kwamba aliliripoti tukio hilo katika vyombo vya dola.
Alidai kuwa mbali na tishio hilo la kuuawa kwa risasi, kabla ya tukio hilo kulisambazwa taarifa mbalimbali zilizokuwa zikitishia kumfanyia jambo baya, ikiwemo kumuua ambapo hata hivyo aliwasilisha taarifa hizo polisi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi.
“Hii si mara ya kwanza kutishiwa kuuawa…ni kama mara ya tatu sasa na mara zote nimeripoti polisi,” alisema Shekhe Soud.
Naye daktari wa zamu wa hospitali ya Mount Meru, Dk Leo Temba alisema waliwapokea majeruhi hao majira ya saa tano usiku jana wakiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao, akisema Shekhe Kifea alipokewa akiwa amevunjika miguu yote miwili na kupoteza vidole vitatu vya mguu wa kulia.
Alisema kutokana na kuvuja damu nyingi, walimpokea na kumwongezea damu ambayo hata hivyo haikutosha na kulazimika kumwongezea nyingine asubuhi ya jana.
Akimzungumzia Shekhe Soud, alisema alipata majeraha madogo katika mguu wa kushoto na jeraha moja kubwa katika eneo la paja karibu na makalio ambapo hata hivyo naye alilazimika kuongezewa damu kutokana na kuvuja damu nyingi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo alidai kwa mujibu wa maelezo ya Shekhe Soud, siku chache zilizopita alikuwa na mgogoro ndani ya taasisi anayoiongoza hadi kufikia kumfyatulia risasi kwa madai kuwa amekuwa akishirikiana na serikali pamoja na waislamu wenye msimamo mkali.
Aidha, aliahidi kuwa vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinaingia kazini kuanzia sasa kulifanyia uchunguzi tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote wanaohisiwa kuhusika na tukio hilo kwakuwa mmoja wa watu waliowahi kumtishia Soud anashikiliwa na polisi na tayari alishafikishwa mahakamani kuhusiana na ulipuaji wa bomu katika baa ya Arusha Night Park mwanzoni mwa mwaka huu.
Kutokana na kuhusishwa huko kwa mtuhumiwa huyo na tukio hilo ni wazi kuwa tukio hili bado linahisiwa kuhusishwa na tukio la watuhumiwa wa ugaidi, ingawa kupo kutofautiana kwa maelezo baina ya mkuu huyo wa mkoa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, Sabas anayedai tukio hilo halihusishwi na lile la ugaidi.
Polisi waua majambazi
Katika tukio jingine, Polisi jijini Arusha wamewaua watu watatu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi ikidaiwa walikuwa wakijiandaa kuiba kiasi cha Sh milioni 100 kutoka kwenye duka la utengenezaji na uuzaji wa vigae linalojulikana kwa jina la Arusha Islamic Center lililopo eneo la Esso.
Kwa mujibu wa Kamanda Sabas, polisi walipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema juzi kuwa  kuna majambazi wanajiandaa kuvamia duka hilo na kuiba fedha. Majambazi hao ambao hawajafahamika, wametajwa kuwa na umri wa kati ya miaka 25 na 30.
Alisema mara baada ya kupata taarifa hizo polisi walijipanga na kuanza kufanya doria maeneo hayo ndipo walipoliona gari namba T 762 CWE aina ya Toyota Corolla eneo la eneo la relini  na ndipo watu hao walipowashtukia polisi  na kuanza kuwarushia risasi.
Alisema mara baada ya majambazi hao kuanza kuwarushia polisi risasi, polisi nao walijibu mapigo na kuanza kufukuzana nao hadi kwenye kona ya TBL ambapo majambazi wawili walishuka kwenye gari hilo na kuanza kukimbia wakiwa na bunduki aina ya Shotgun yenye namba za usajili A 947514M Action Pump.
Alisema kwenye gari kulikutwa majambazi ambao walidhibitiwa lakini walikufa wakiwa njiani kupelekwa hospitali ya Mount Meru kwa matibabu.
Alisema walipokagua gari hilo walikuta risasi 3 na ganda moja la risasi. Miili yao imehifadhiwa hospitali ya mkoa ikisubiri kutambuliwa.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 4588

Trending Articles